Rayon Sport kucheza Simba Day

TIMU ya soka ya Simba itacheza na Rayon Sports ya Rwanda mchezo wa kirafiki kusherehekea Simba Day Agosti 8 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo utatumiwa kutambulisha nyota wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Simba imewaalika Rayon Sports waje Agosti 7. Barua ya Simba ilisainiwa na Katibu Mkuu wao, Dk Arnold Kashembe.

Rayon inayofanya vizuri nchini Rwanda na ni bingwa wa Ligi ya huko, imekubali kuja. Katika kusherehekea ubingwa wao, hivi karibuni waliialika Azam FC kucheza nao na kutoka na ushindi wa mabao 4-2. Rayon Sports ilimaliza ligi na pointi 73.

Ilifuatiwa na APR na Polisi zenye pointi 58. Simba inatarajiwa kuwatambulisha wachezaji wapya Haruna Niyonzima, Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Jamali Mwambeleko, Emmanuel Mseja, Said Mohamed na Emmanuel Okwi.

Katika hatua nyingine, kiungo wa Simba, Said Ndemla anatarajiwa kwenda kufanya majaribio katika klabu ya AFC ya Sweden. Ataondoka baada ya Simba kumruhusu. Mwaka jana walimgomea Ndemla kwenda AFC.