Yanga, Simba hatarini kushushwa daraja

ZIMEBAKI siku tisa kabla ya dirisha la usajili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza na la pili kufungwa. Muda huo umebaki huku vigogo vya soka nchini Yanga na Simba havijakamilisha usajili wake na kuwa hatarini kushushwa daraja la kwanza kwa kutofuata kanuni.

Dirisha la usajili lilifunguliwa rasmi Juni 15, mwaka huu na sasa linaelekea mwisho lakini hadi jana, hakuna timu hata moja ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyosajili kupitia mtandao wa usajili wa wachezaji.

Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jonas Kiwia alisema jana timu tatu za madaraja ya chini ndio zimekamilisha mchakato huo. Kiwia alisema iwapo Yanga, Simba na timu nyingine za Ligi Kuu na daraja la kwanza zitashindwa kukamilisha mchakato ndani ya siku zilizopangwa, zitashushwa daraja kwani hazitaruhusiwa kushiriki ligi husika.

“Hakuna timu hata moja za Ligi Kuu iliyosajili kupitia mtandao, tunazihimiza kuanza usajili mapema kuepuka usumbufu baadaye wa kushushwa daraja,” alisema. Alisema imejengeka tabia kwa timu za Tanzania kila msimu kuchelewa kumaliza usajili mapema na kusubiri dakika za mwisho ambapo kuna athari kubwa.

Alitaja athari mojawapo ni kukwama kwa mtandao kwani kila timu inakimbizana na muda wa kufungwa kwa dirisha hilo. Kiwia amesema ni muhimu timu zote za ligi hizo kuanza mchakato huo mapema kukwepa adhabu ya kushushwa daraja.

Timu nyingi bado zinakimbizana kusajili wachezaji wakisubiri baadhi ya wachezaji ziliowasajili kumaliza mikataba walikotoka. Wachezaji wengi mikataba yao na timu za zamani inatarajiwa kuisha mwishoni mwa mwezi huu, mwezi ujao na Oktoba.

Mbali ya Yanga na Simba, nyingine ni Mtibwa Sugar, Azam, Majimaji Songea, Lipuli, Mbao FC, Kagera Sugar na Mwadui, Ruvu Shooting, Mji Njombe, Ndanda, Singida United, Stand United, Mbeya City,