Yanga wauza mali, bao 7 zaivuruga Msimbazi

UONGOZI wa Yanga umewatangazia wadau wote nchini kujitokeza makao makuu ya klabu hiyo Jangwani kwa ajili ya mnada wa mali zake. Yanga imetangaza jana kuwa inauza magari yake manne, Honda CVR T 176 AVV, Toyota Coaster, T 515 AZM, basi Mitsubishi lenye uwezo wa kubeba abiria 65 lenye namba T 272 AHJ na Toyota Prado lenye namba za usajili T 547 BAC ambayo imesema yote hayatembei.

Taarifa ya zabuni ya Yanga iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana imewataka wanaotaka kununua magari hayo kulipa ada ya zabuni ya Sh 50,000. Magari yote yamelipiwa ushuru.

Ingawa Yanga imekuwa na matatizo ya fedha, ni kawaida kwa kampuni au klabu kuuza mali zake chakavu ambazo haizitumii kwa wakati huo. Wakati huohuo, timu ya soka ya Yanga imewasili salama Morogoro na jana ilianza mazoezi kwa vipindi viwili asubuhi na jioni kujiandaa na Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.

Yanga imepiga kambi ya siku 10 Morogoro kujiandaa na Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, utakaofanyika Agosti 23, Uwanja wa Taifa. Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina alisema wanajifua mazoezi mara mbili kwa siku ili wachezaji warudi mchezoni baada ya likizo.

Alisema mazoezi yao ni ya ufundi uwanjani kwani kabla ya kuondoka Dar Es Salaam, walifanya mazoezi ya kuongeza nguvu Gym. Alisema wamepanga kuitumia kambi hii kujiandaa na mechi mbili za kirafiki Agosti 6 na Singida United na Rayon Sport ya Rwanda.

Alisema Donald Ngoma na Thabani Kamusoko hawajaripoti tangu walipoenda mapumziko na kipa Beno Kakolanya ambaye ni mgonjwa. Wakati huohuo, klabu ya Simba imekanusha taarifa kuwa imecheza mechi ya kirafiki Afrika Kusini ilikopiga kambi na kufungwa mabao 7-0.

Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema jana habari za Simba imefungwa na timu ya daraja la kwanza ya Royal Eagles ni uzushi. “Simba haina rekodi za ovyo kama hizo kokote inapocheza duniani na haijawahi kufungwa na klabu yoyote idadi ya magoli kama hayo kama zilivyo klabu nyingine nchini hususan klabu ambayo mashabiki wake ndio waliozusha hilo,” alisema.

Alisema dunia ya leo ni ya teknolojia na kama ingekuwa ni kweli, hakuna ambaye asingeiona taarifa kutoka mitandaoni au vyombo vya habari vya Afrika kusini. Aliwataka mashabiki wajue siku za kambi yao Afrika Kusini Makocha wamejikita kutengeneza stamina ya wachezaji wao.

Alisema baada ya hapo, watacheza mechi mbili na Orlando Pirates na Bidverst kabla ya kurejea Agosti 5 kwa Simba Day Agosti 8 kucheza na Rayon Sports ya Rwanda.