Mayay amfagilia Karia

ALIYEKUWA mgombea wa nafasi ya urais wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Ally Mayayi amesema atamsaidia Rais aliyeshinda uchaguzi huo Wallace Karia kuendeleza mchezo huo.

Mayay alisema jana lengo lake na Karia lilikuwa moja kuendeleza mpira wa Tanzania hivyo kushindwa kwake haimaniishi kuachana na jitihada za kuendeleza mchezo wa soka.

“Nampongeza Karia kwa ushindi, binafsi nimeridhika kwa sababu uchaguzi ulikuwa ni wa haki na huru. Nitaendelea kubaki kwenye mchezo wa mpira ili kutoa ushauri wangu kwa manudaa ya taifa letu,” alisema Mayay.

Mchezaji huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars’, alisema amewataka wanamichezo wenzake walioshindwa kwenye uchaguzi huo kuvunja kambi zao na kuongeza nguvu kwa kuwapa ushirikiano viongozi wapya wa TFF.

Alisema ana imani kubwa na Karia na timu nzima iliyoingia madarakani, hivyo kitu cha msingi kinachotakiwa ni viongozi hao kupewa ushirikiano ili waweze kutimiza majukumu yao.