Msuva aleta shangwe Stars

MCHEZAJI wa kimataifa, Simon Msuva jana alionesha matunda yake ya kucheza soka ya kulipwa katika timu ya Difaa Hassan El-Jadida ya Morocco baada ya kuifungia Taifa Stars mabao dhidi ya Botswana.

Katika mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, Msuva alikuwa mwiba mchungu kwa Botswana na mabao yake hayo yaliipa Stars ushindi wa mabao 2-0.

Kwa matokeo hayo, Stars imejiweka kwenye mazingira mazuri ya kukwea kwenye viwango vya Fifa. Msuva alianza kupeleka shangwe kwa mashabiki wa soka nchini katika dakika ya sita, alipofunga bao la kuongoza akiunganisha pasi ya Mzamiru Yassin kabla ya kuujaza mpira wavuni.

Mchezaji huyo wa zamani wa Yanga, Msuva aliiandikia Stars bao la pili katika dakika ya 62 baada ya kuunganisha vyema pasi ya kichwa kutoka kwa Shiza Kichuya. Katika mechi ya jana, timu hizo zilishambuliana kwa zamu ambapo kuna wakati Botswana walikuja kasi na nusura wapate bao mara kadhaa.

Hata hivyo, Stars jana ilikuwa na nafasi ya kupata mabao zaidi, hasa dakika ya 59, mshambuliaji wake Mbwana Samatta anayecheza soka ya kulipwa KRC Genk ya Ubelgiji nusura apate bao, lakini akiwa na kipa wa Botswana, Mwampule Masule shuti lake lilidakwa.