Mbao zaikwama Simba

TIMU ya soka ya Simba imeshindwa kuimeza Mbao Fc ya hapa baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara uliochezwa Uwanja wa CCM, Kirumba, Mwanza.

Huo ni mchezo wa kwanza Simba kuruhusu mabao kwenye nyavu zake ikipoteza rekodi iliyoanza nayo katika michezo mitatu iliyopita, iliyoshinda bila kuruhusu bao lolote ikifunga 10. Pia huu ni mchezo wa pili wa ugenini kupata sare baada ya awali kupata 0-0 kwa Azam FC.

Kutokana na sare hiyo ya mabao 2-2, Simba inaendelea kuwa ya pili kwa kufikisha pointi 8 na mabao 12 ya kufunga na mabao 2 ya kufungwa. Inaifuatia Mtibwa Sugar inayoongoza ligi hiyo yenye timu 16 kwa pointi tisa. Hata hivyo, msimamo huo huenda ukabadilika kesho wakati timu nyingine zitakazopocheza mechi za ligi.

Mabao ya Simba yalifungwa na Shiza Kichuya na James Kotei huku ya Mbao FC yakifungwa na Habibu Kiyombo na Emmanuel Mvuyakure. Simba ilianza kwa kasi mchezo huo ambapo katika dakika ya 16, Kichuya aliwaamsha mashabiki kwa bao la kwanza alilofunga kwa kichwa baada ya kupata pasi ya Erasto Nyoni.

Hadi mapumziko, Simba ilikuwa mbele kwa bao hilo ikiongoza kwa mashambulizi na kupata nafasi ambazo haikuzitumia vyema. Kipindi cha pili, dakika ya 46 Mbao waliingia kwa kasi na kusawazisha bao lililofungwa na Habibu Kiyombo kwa shuti la mbali, mita 18.

Dakika moja baadaye, ya 47 Simba ilifunga bao la pili kupitia James Kotei kwa shuti kufuatia pasi ya faulo iliyopigwa na Erasto Nyoni. Mbao FC haikukata tamaa badala yake iliendelea kushambuliana kwa zamu na dakika ya 81 Mvuyakure aliisawazishia kwa shuti la umbali wa mita 18 nje ya eneo la penalti la Simba.

Bao hilo liliwakera mashabiki wa Simba walioanza kuondoka uwanjani wamekata tamaa. Mshambuliaji wake mahiri, Emmanuel Okwi na kiungo mshambuliaji aliyesajiliwa kwa fedha nyingi kutoka Yanga, Haruna Niyonzima hawakufua dafu huku Niyonzima akielezwa kutogusa mpira muda mrefu kipindi cha kwanza.

Kwa kukataa kufungwa, Mbao wameendeleza rekodi ya kuwa wagumu kufungwa na Simba na vigogo wengine wa soka nchini, Yanga. Mwaka jana, Mbao FC ilifungwa na Simba kwa shida zilipokutana mara tatu katika mechi mbili za Ligi Kuu Mwanza na Dar es Salaam na pia katika fainali ya Kombe la Shirikisho Dodoma.

Michezo mingine ya ligi inatarajiwa kuchezwa kesho ambapo mabingwa watetezi, Yanga wanatarajiwa kuwakaribisha Ndanda FC kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Mbao FC: Kelvin Igendelezi, Boniface Maganga, Abubakari Ngalema, Yusufu Mgeta, Yusuph Ndikumana, Sadala Lipangile, Ibrahim Njohole/Emmanuel Mvuyakure dk. 63, Hussein Kasanga, Moses Shabani/ Ndaki Robert dk. 58, Said Said/HerbetLukindo dk. 37naHabibuKiyombo, Simba: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohamed Hussein, Juuko Murshid, Method Mwanjale, James Kotei, Mzamiru Yassin, Nicolaus Gyan/Juma Luizio dk. 75, John Bocco, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya/Haruna Niyonzima dk. 45