Simba yapata dawa ya Stand United

KOCHA Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, ameweka wazi mpango mkakati wao utakaowasaidia kupata ushindi katika mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Stand United ambao utapigwa Uwanja wa Kambarage Shinyanga mwishoni mwa wiki hii.

Simba ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Mbao FC kwenye mchezo wa mzunguko wa nne wa ligi hiyo uliopigwa Alhamisi iliyopita Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza matokeo yaliyowashusha hadi nafasi ya nne kwenye msimamo.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Mayanja alisema kuelekea kwenye mchezo huo moja ya mikakati yao ni kuhakikisha wanawatumia washambuliaji wanne, na kucheza kwa kushambulia muda wote wa mchezo jambo ambalo anaamini litawasaidia kupata ushindi.

“Unajua kama tutacheza kwa kuwashambulia wataogopa kuja langoni kwetu hiyo itakuwa faida kwetu lakini sababu ya kutumia washambuliaji wanne ni kutaka kufunga mabao mengi iwezekanavyo kama tulivyofanya kwenye mchezo na Ruvu Shooting,”alisema Mayanja.

Kocha huyo raia wa Uganda alisema, wamedhamiria kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo, na wasingependa kupata sare au kupoteza kwa sasa kwani ushindani umekuwa mkubwa na kila timu imepania kufanya vizuri msimu huu.

Mayanja alisema wanawaheshimu Stand kuwa ni timu nzuri na wana rekodi nzuri hasa wanapokuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani, lakini watajitahidi kuhakikisha wanacheza kwa nguvu na kupata pointi tatu ambazo anaamini zitapunguza presha waliyonayo kwa sasa.

Simba inayofundishwa na Kocha Mkuu Joseph Omog, raia wa Cameroon, inalazimika kushinda mchezo huo, ili kutuliza presha za mashabiki wa timu hiyo ambao wameanza kuutilia mashaka uwezo wake wakidai anapata shida kwenye kusoma mchezo na kufanya mabadiliko hasa baada ya sare ya mabao 2-2 na Mbao.