Simba yaiwinda Mtibwa Sugar

MIAMBA ya soka Tanzania Bara, Simba jana waliingia kambini kujiandaa na pambano lao la Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar Jumapili Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam. Mchezo huo unatarajiwa kuwa wa vuta nikuvute kutokana na timu hizo kulingana kwa pointi 11, na idadi ya michezo lakini Simba wako kileleni kutokana na wingi wa mabao ya kufunga.

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, amepania kushinda mchezo huo kujihakikishia kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ambayo ina ushindani mkubwa msimu huu. “Ni mchezo mgumu, tunacheza na timu nzuri yenye wachezaji wengi wenye vipaji lakini kucheza nyumbani ni faida ambayo tutaitumia kuhakikisha tunaibuka na ushindi,” alisema.

Kocha huyo raia wa Cameroon, alisema maandalizi yao kuanzia Jumatatu yameenda vizuri na wachezaji wapo katika ubora wa juu kitu kinampa matumaini ya kuibuka na ushindi. Omog alisema amekuwa akizungumza na wachezaji wake baada ya mazoezi na kuwaeleza ugumu uliopo Ligi Kuu na kuwataka kila mmoja acheze kwa kujitoa kuipa timu ushindi.

Alisema asingependa kuona wanapata hata sare katika mchezo huo kwani kutawaondoa katika nafasi yao kama Azam FC, Singida United na mahasimu wao, Yanga wakishinda keshokutwa.

Omog alisema kikosi chake kitakachocheza na Mtibwa Sugar kitakuwa na mabadiliko kidogo katika baadhi ya nafasi ili kuongeza hamasa ya kushinda mapema tofauti na mechi nyingine.

Tayari kinara wa mabao, Emmanuel Okwi raia wa Uganda amesharejea kambini kujiunga nao kwa mchezo huo unasubiriwa kwa hamu kubwa na wadau na mashabiki wa timu hizo mbili.