Yanga yakaa penyewe

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga jana walikwea kileleni mwa msimamo baada ya kuifunga Kagera Sugar mabao 2-1 ugenini Uwanja wa Kaitaba, Bukoba. Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 12 sawa na Azam iliyotoka sare ya bao 1-1 na Mwadui ya Shinyanga.

Azam ilikuwa na uwezo wa kuongoza ligi kama ingeshinda mchezo wa jana, lakini sare imeifanya ilingane pointi na Yanga na izidiwe idadi ya mabao ya kufunga ambapo Yanga imefunga sita na Azam matano.

Mabao ya Yanga jana yalifungwa na Obrey Chirwa dakika ya 39 na Ibrahim Ajibu dakika ya 47 huku kila mmoja akimchangia mwenzake pasi la bao. Bao la kufutia machozi la Kagera likifungwa na Jaffar Kibaya dakika ya 52.

Hata hivyo, kuendelea kukaa kileleni kwa Yanga kunategemea matokeo ya mechi ya Simba na Mtibwa Sugar leo ambapo zote zina pointi 11 hivyo timu itakayoshinda itaongoza na endapo zitatoka sare ina maana zitaungana na Yanga na Azam kwenye pointi 12 na mwenye uwiano mzuri wa mabao ndiye atakayekaa kileleni.

Kagera Sugar inaendelea kushika mkia kwa pointi mbili baada ya kupoteza michezo minne na kupata sare mbili ikiwa haijashinda mchezo hata mmoja. Michezo mingine iliyochezwa jana ni Singida United iliyopata suluhu ugenini Uwanja wa Mabatini dhidi ya Ruvu Shooting, Ndanda FC ilitoka sare ya bao 1-1 nyumbani Nangwanda Sijaona dhidi ya Majimaji.

Kikosi cha Kagera Sugar: Juma Kaseja, Mwaita Gereza, Adeyoum Ahmed, Juma Shemvuni, Juma Nyosso, Ally Iddi, Venence Ludovic, Ozuka Okochukwu, Jaffar Kibaya, Omar Daga na Christopher Edward/Themi Felix.

Yanga SC: Youthe Rostand, Juma Abdul, Gardiel Michael, Andrew Vincent, Kelvin Yondani, Said Juma ‘Makapu’/Raphael Daudi, Pius Buswita, Papy Tshishimbi, Obrey Chirwa/Maka Edward, Ibrahim Ajib, Geoffrey Mwashiuya/Emmanuel Martin