Wachezaji judo wakamatwa JNIA

WACHEZAJI 10 wa mchezo wa judo wa Tanzania wanashikiliwa na polisi baada ya kukamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kutaka kuondoka nchini kinyemela.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Dk Yusuph Singo, wachezaji hao walikamatwa JNIA usiku wa kuamkia jana kabla ya kupanda ndege kwenda Italia, ambako haijulikani walikuwa wanakwenda kushiriki mashindano gani. Alisema kuwa msafara huo wa watu 10 ulizuiwa baada ya kutokuwa na kibali kutoka katika chama cha taifa cha mchezo huo wala kile cha BMT.

Hata hivyo, haikujulikana walitaka kupanda ndege gani na walikuwa wakienda Italia kushiriki mashindano yapi. Singo alisema wachezaji hao ambao majina yao hayakupatikana, wamezuiwa katika Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege JNIA Terminal Three kwa mahojiano zaidi.

Mkurugenzi huyo wa michezo alimtaja mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Bundala kuwa naye anashikiliwa na polisi kwa kuwa yeye ndiye alikuwa akiratibu safari hiyo. Hata hivyo, juhudi za kumpata Kamanda wa Kanda ya Viwanja vya Ndege nchini, Robert Mayala kuzunguzia suala hilo zilishindikana baada ya kutopokea simu yake kila alipopigiwa.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja awali akizungumza na gazeti hili alisema kuwa Bundala amekuwa akijishughulisha na judo wakati alifungiwa maisha kujihusisha na mambo ya judo. “Hawa watu wa judo wanashangaza sana wanamuachia shughuli zao Bundala wakati alishafungiwa maisha kujihusisha na mchezo huo,” alisema Kiganja kwa njia ya simu. Juhudi za gazeti hili zinaendelea kumsaka Kamanda Mayala ili kupata taarifa kamili za wachezaji hao.