Ismail Juma afariki, kuzikwa leo Babati

MWANARIADHA wa kimataifa wa Tanzania, Ismail Juma amefariki dunia kwa ajali ya gari Babati mkoani Manyara na anatazamiwa kuzikwa leo.

Juma alifariki juzi baada ya pikipiki aliyokuwa akiendesha kugongwa na Lori aina ya fuso katika barabara ya Babati-Dodoma juzi na kufariki hapo hapo. Kocha wa mchezaji huyo, Denis Malle akizungumza kwa simu na mwandishi wa habari hizi alisema jana kuwa, mwili wa Juma unatarajia kuhifadhiwa katika makaburi ya Gendi kilometa chache kutoka mjini Babati leo saa 7:00 mchana.

Alisema kuwa Juma ambaye alikuwa hajaoa alikuwa akiishi katika familia yake na alikuwa na mipango mikubwa ya maendeleo yake na ile ya kuendeleza familia yake. Alisema kuwa mwanariadha huyo ndiyo kwanza alianza kufaidi matunda ya mbio, kwani Kampuni ya Adidas ilimpatia bonas ya dola za Marekani 5,000 kwa kutumia viatu vya kampuni hiyo na kushika nafasi ya tatu katika mbio za marathon za Prague, Jamhuri ya Czech.

Malle alisema kuwa yeye ndiyo alimpatia fedha hizo na alikwenda Babati kununua mbegu za mahindi na wakati akizipeleka nyumbani kwao, Fuso hilo lilimgonga na kumuua. Alisema kuwa zawadi ya ushindi huo inatarajia kufika mwishoni mwa mwezi huu, huku Novemba 15 alitakiwa kwenda Nairobi, Kenya kuingia mkataba mpya na Adidas.

Alisema kifo cha mwanariadha huyo ni pigo kubwa kwa taifa, familia yake na medani ya riadha kwa ujumla kwani alikuwa kijana mdogo na ndiyo kwanza alikuwaakianza kuchipukia na kufanya vizuri katika mbio mbalimbali.

Juma hivi karibuni alivunja rekodi ya taifa ya mbio za nusu marathon baada ya kukimbia kwa dakika 59:30 na kuipiku ile ya awali ya dakika 59:52 iliyokuwa ikishikiliwa na Dickson Marwa.

Pia mwanariadha huyo tayari jina lake liliwasilishwa katika Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kwa ajili ya maandalizi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Gold Coast, Australia Aprili Wakati huohuo, TOC imetuma salamu za rambirambi na kusema kuwa imeguswa na na kusikitishwa na kifo cha mwanariadha huyo kilichotokea huko Gendi, Wilaya ya Babati.

Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi alisema kuwa inamtambua Juma kama mwanariadha mahiri ambao majina yao yaliwasilishwa ofisini kwake kwa ajili ya maandalizi ya kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola. “TOC inatoa masikitiko yake kwa msiba huu mkubwa kwa familia ya Ismail, Riadha Tanzania na Michezo kwa ujumla,” alisema Bayi jana. “Bwana ametoa, Bwana ametwaa,jina lake lihimidiwe”