Moyes ajiunga na ‘Wagonga Nyundo’

Kocha wa zamani wa Sunderland, Manchester United na Everton amepewa mkataba wa miezi sita kuifundisha West Ham United inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

Mwenyekiti wa ‘Wagonga Nyundo’ David Sullivan ametangaza uamuzi huo leo baada ya kumfukuza kocha Slaven Bilic Jumatatu, wiki hii baada ya timu hiyo ya jijini London kupokea kipigo cha 4-1 kutoka kwa Liverpool.

Hata hivyo, West Ham inakuwa klabu ya nne inayoshiriki Ligi Kuu England kufundishwa na Moyes, ambaye aliirithi mikoba ya Alex Ferguson bila mafanikio na kufutwa kazi.

“Tunahitaji mtu mwenye ujuzi na uzoefu wa Ligi Kuu na wachezaji na tunaamini kuwa David (Moyes) ni mtu sahihi ambaye atabadili hali ya mambo,” mwenyekiti wa West Ham amenukuliwa na tovuti ya klabu hiyo.