Yanga Krismasi shwari

YANGA imefuzu hatua ya 32 ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kuifunga Reha FC mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana.

Mabao ya Yanga yalifungwa na kiungo Pius Buswita dakika ya 82 akiunganisha pasi ya Amisi Tambwe, kabla Tambwe hajafunga bao la pili kwa pasi ya Buswita. Baada ya mabao hayo, Reha walionekana kukubali matokeo na Yanga wakaanza kucheza kwa uhuru uwanjani, wakigongeana pasi za kuwaburudisha mashabiki wao.

Katika mchezo huo, Reha walionekana kuwa wagumu karibu muda wote wa mchezo na hasa kipindi cha kwanza ambapo walicheza kwa kujihami zaidi wakifanya mashambulizi ya kushtukiza lakini Yanga waling’amua janja hiyo na kubadili maarifa kipindi cha pili na kushambulia kwa nguvu zaidi.

Reha ambayo ilikuwa chini ya kocha Ivo Mapunda, kipa wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ilikuwa ngumu kufungika, na kipa wake Idrissa Ramadhani alikuwa nyota kwa kudaka kwa ustadi.

Mabadiliko ya kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa ya kumpumzisha Emmanuel Martin na kumuingiza Said Mussa aliyekuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kilichoshiriki fainali za Afrika nchini Gabon Mei mwaka huu, yalifufua matumaini.

Said aliongeza nguvu safu ya ushambuliaji wa Yanga akishirikiana na Yussuf Mhilu, Tambwe na Buswita na kupatikana mabao mawili ya haraka haraka. Kikosi cha Yanga: Youth Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Nadir Haroub, Andrew Vincent, Papy Tshishimbi, Yusuph Mhilu, Raphael Daud, Amis Tambwe, Pius Buswita na Emmanuel Martin/Said Mussa dk 69.

Reha FC: Idrisa Ramadhan, Brian Khiza, Japhary Athuman, Abdul Hassan, Ambele Daud, Zuberi Makame, Rajabu Mohamed, Silvanus Sostenes/Mohamed Abdallah dk58, Bazo Sentumbi/ Mohammed Hassan dk 64, Salum Athuman na Idrisa Omary.