Yanga yaua, Simba leo

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, Yanga wameanza vizuri mzunguko wa pili baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Lipuli katika mchezo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa.

Ushindi huo umefuta ubabe wa Lipuli iliyowasumbua katika mchezo wa raundi ya kwanza uliochezwa Dar es Salaam, ambapo walitoka sare ya bao 1-1 lakini pia, iliondoa ile dhana ya kutokufungwa kwenye Uwanja wa Samora.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Papy Kabamba Tshishimbi na Pius Buswita. Ushindi huo wa Yanga unafikisha jumla ya pointi 31, hivyo, itaendelea kubaki nafasi ya tatu iwapo kama Azam itakuwa imeshinda mchezo wake dhidi ya Ndanda uliotarajiwa kuchezwa jana jioni.

Kabamba alifunga bao la uongozi dakika ya 19 akimalizia mpira wa Emmanuel Martin aliyekuwa akijaribu kufunga, lakini ulikokolewa na kipa wa Lipuli, Aghaton Anthony na kumkuta mfungaji aliuejaza wavuni.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Yanga iliyocheza kwa kasi kubwa huku ikijiamini ilikuwa ikiongoza bao 1-0. Bao hilo la ushindi lilipatikana baada ya kuingia kipa chipukizi Ramadhan Kabwili dakika chache kufuatia kutolewa kwa kipa namba moja, Youthe Rostand aliyeumia.

Kipindi cha pili licha ya Lipuli kuchangamka walishindwa kuzitumia nafasi kadhaa walizopata lakini Yanga ilitengeneza nafasi ya pili na kuitumia ipasavyo baada ya kufunga bao la pili dakika ya 55 lililofungwa na Buswita aliyepata pasi ya Obrey Chirwa.

Hadi dakika 90 zinamalizika Yanga ilitoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-0. Hata hivyo, kipindi cha pili walicheza zaidi kwa kujihami huku Lipuli ikishambulia zaidi bila mafanikio.

Michezo mingine iliyochezwa jana ni Singida United ilishinda mabao 3-2 dhidi ya Mwadui, Tanzania Prisons ilishinda 2-0 dhidi ya Njombe Mji na Mbeya City ikishinda ugenini 2-1 dhidi ya Majimaji. Wakati huohuo, Simba leo inashuka dimbani kucheza na Ruvu Shooting jijini Dar es Salaam.