Mwakyembe aagiza Bodi ya Filamu ilinde maadili

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk.Harrison Mwakyembe, ameiagiza Bodi ya Filamu Tanzania kuandaa mara moja mikakati madhubuti ya kuhakikisha inasimamia kikamilifu tasnia ya filamu nchini ili kulinda maadili na tamaduni za taifa pamoja na kusimamia wizi wa kazi za wasanii.

Mwakyembe alisema kuwa bodi hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa na anautambua mchango wao lakini kuna baadhi ya vitu anaona haviendi sawa.

Akizungumza wakati wa kupokea taarifa ya utendaji wa bodi hiyo Dar es Salaam jana, Mwakyembe alisema kuwa bodi hiyo imeundwa kwa lengo kuhakikisha tasnia ya filamu inasonga mbele bila kumong’onyoa maadili ya taifa.

Alisema kuwa kwa sasa nchi ipo kwenye kipindi cha muingiliano wa kitamaduni kutoka mataifa mbalimbali na filamu nyingi kutoka nje zimekuwa zikiingia nchini hivyo kama hapatakuwa na umakini wa kudhibiti wa hali ya juu basi nchi itapoteza utamaduni wake.

Alisema kuwa kuanzia sasa anatoa agizo na anataka litekelezwe mara moja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Kamati ya Maudhui pamoja na Bodi ya Filamu Tanzania kukaa na kupanga madaraja ya filamu na mpaka kufikia mwanzoni mwa Juni yaanze kutumika kote nchini.

“Bado zipo filamu ambazo hazina daraja hazioneshi zinatakiwa ziangaliwe na watu wa umri gani, hivyo naagiza TCRA, Kamati ya Maudhui na Bodi ya Filamu mwisho mwezi wa sita kuanzia hapo ni marufuku kwa TV au jumba la sinema kuonesha filamu ambayo haina muda,” alisema Mwakyembe.

Aliongeza, kutokana na kuwepo kwa vibanda vya kuoneshea sinema kiholela ambavyo vingine vinatumika kuoneshea picha chafu zisizozingatia maadili na watazamaji wake baadhi wakiwa watoto hivyo bodi hiyo kuanzia sasa ianze kuandaa rasimu ya kuzuia tatizo hilo ambapo mpaka kufikia Mei mwaka huu iwe tayari ameshakabidhiwa mezani kwake.

“Vyombo vinavyohusika na usimamizi wa kazi za wasanii COSOTA, Bodi ya maudhui na Bodi ya Filamu nataka mkae kwa pamoja na kuangalia njia za kudhibiti wizi wa kazi za wasanii.

“Naagiza mjadili na ndani ya wiki moja iwe tayari mniletee ripoti Dodoma ili kuangalia hatua ya kuchukuliwa wale ambao wenye kesi za wizi wa kazi za sanaa, haiwezekani watu wakakamatwa na kesi zikakaa muda mrefu kwa maelezo ya zuio, hakuna zuio la muda mrefu ambalo halipatiwi ufumbuzi,” alisema Mwakyembe.