BMT yamfungia Katibu Mkuu Tasma

BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limemfuta na kufungia kujishugulisha na shuguli zozote za kimichezo kwa miaka mitatu, Katibu Mkuu wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Wanamichezo (Tasma), Nassoro Matuzya.

Akizungumza na HabariLeo, Kaimu Msajli wa Michezo Ibrahim Mkwawa alikiri kumfungia Matuzya baada ya kushindwa kuwasilisha ripoti ya fedha ya Tasma licha ya kutakiwa kufanya hivyo mara kadhaa.

Katika barua yenye kumbukumbu namba BMT/C.3/44/vol.3/21 iliyoandikwa Februari 15 na kusainiwa na Mkwawa na nakala kwa mwenyekiti wa Tasma, iliweka wazi kuwa BMT imeamua kumfungia Matuzya baada ya kushindwa kuwasilisha masuala ya fedha ya Tasma.

“Utakumbuka Oktoba 11, 2017 kwa kutumia mamlaka niliyonayo ya kifungu cha 20 (3) cha Sheria za Baraza la Michezo la Taifa ya 1967, kama ilivyorekebishwa 1971 niliagiza kufanyika kufanyika ukaguzi wa akaunti ya Tasma kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na viongozi wenzio wa chama.

“Baada ya ukaguzi huo ilibainika pasipo shaka Tasma inaendesha shuguli zake bila akaunti kufuatia kufungwa kwa akaunti 01J1027507900 iliyopo CRDB benki.

“Kwa mujibu wa Katiba ya Tasma, Katibu Mkuu ndiyo mwenye wajibu wa kuandaa ripoti ya fedha kwa kushirikiana na mhazini na vile vile ndiye atajibu hoja zote za fedha. “Kitendo cha kufungwa kwa akaunti ya chama ni ukiukwaji wa ibara ya 38(6), (7), na 48 ya katiba ya Tasma.

“Aidha, imebainika kuwa kutokana na kutokuwepo kwa akaunti inayotambulika ya chama, fedha zinazopatikana zinakusanywa moja kwa moja na Katibu Mkuu, Dk Nassoro Matuzya na haziende kwenye chama.

“Kufuatia ukaguzi huu uliofanyika kwa siku 16, kuanzia tarehe 17 Oktba, 2017 hadi Novemba 3, alipewa muda ili atoe maelezo yake kimandishi, jambo ambalo hakulitekeleza.

“Januari 29, 2018 nilimuandikia tena barua ya kutoa maelezo kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kukiuka Katiba ya Tasma na sheria, hiyvo kwa mamlaka niliyopewa na kanuni ya 10 (1) (b) na (c) ninakufuta uongozi na ninakufungia kujishugulisha na shuguli zozote za uongozi wa chama chochote cha michezo nchini kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Februari 15.”

HabariLeo, lilifanya jitihada za kumsaka Dk Matuzya ikiwa ni pamoja na kumpigia simu yake ya kiganjani mara kadhaa, lakini iliita bila majibu. Matuzya pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Riadha Tanzania (RT).