Mwadui yaishangaza Simba

KOCHA Mkuu wa vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba Pierre Lechantre amestushwa na kiwango kilichooneshwa na timu ya Mwadui na kusema kuna haja ya kuongeza juhudi za mapambano ili kutwaa ubingwa msimu huu.

Kwa mara ya kwanza tangu alipoanza kuifundisha Simba, Mfaransa huyo alijikuta katika wakati mgumu na kushuhudia kikosi chake kikiondoka na pointi moja baada ya sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga.

Akizungumza na gazeti hili kocha huyo aliyetua Msimbazi kurithi nafasi ya Joseph Omog, alisema hakuamini kama Tanzania kuna timu zinauwezo mkubwa kama ule wa Mwadui na baada ya kugundua hilo amepanga kuongeza mazoezi ya kimbinu ili kuweza kushinda mechi zao za ugenini.

“Ukweli mambo yalikuwa magumu kwetu sikuamini kile ambacho kinatokea uwanjani na tulikuwa na bahati kwa sare ambayo tuliipata lakini nimeona ugumu halisi uliopo kwenye ligi ya Tanzania na ninalazimika kulipanga vizuri jeshi langu ili kuhakikisha tuna kuwa mabingwa,” alisema Lechantre.

Mfaransa huyo alisema anatambua sare hiyo imewapa nguvu wapinzani wao Yanga ambao wanawafukuzia kwa karibu, lakini atahakikisha hawafanyi tena kosa na kucheza kwa nguvu na kushinda kila mechi iliyopo mbele yao.

Kocha huyo amesema mabadiliko hayo amepanga kuyaanza mara baada ya kurudi Djibout, ambapo wanakwenda kurudiana na Gendarmarie ukiwa ni mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirisho Afrika CAF.

Pamoja na sare hiyo, Simba wameendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 42, katika michezo 18 waliyocheza sawa na Yanga ambayo inashika nafasi ya pili na pointi 37 na Azam ipo katika nafasi ya tatu na pointi 34 hiyo ikiwa ni kabla ya mchezo wake wa jana jioni dhidi ya Lipuli FC.