Simba mbele kwa mbele

VINARA wa soka Tanzania Bara, Simba wameondoka nchini jana jioni kwenda Djibouti, kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gendarmerie Nationale utakaofanyika Februari 21.

Katika mchezo huo, Simba itamkosa nahodha wake John Bocco ambaye alifunga mabao mawili katika mchezo wa kwanza uliomalizika kwa ushindi wa 4-0, kutokana na majeraha ya kifundo cha mguu wa kushoto aliyoyapata kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mwadui FC ambapo alishindwa kuendelea na mchezo na kutolewa nje.

Akizungumza na gazeti hili Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pierre Lechantre, alisema pamoja na kumkosa Bocco, lakini ana matumaini makubwa ya ushindi kutokana na maandalizi waliyofanya pamoja na ari waliyokuwa nayo wachezaji wake.

"Maandalizi yamekamilika, tumejipanga kuhakikisha tunacheza kwa nguvu bila kujali kama tunaongoza kwa mabao manne najua mchezo utakuwa mgumu, lakini lazima tusonge mbele kutokana na ubora wa timu yangu,” alisema Lechantre.

Mfaransa huyo alisema amesafiri na kikosi cha wachezaji 19 wenye uhakika wa kucheza na wa 20 ni Bocco ambaye ameamua kwenda naye ili kuendelea kuangalia maendeleo yake kama anaweza kuwa fiti siku ya mchezo Jumatano.

Kocha huyo ambaye amekabidhiwa kikosi cha Simba siku chache zilizopita ameoneshwa kudhamiria ushindi kutokana na ahadi ambayo ameitoa kwa viongozi na mashabiki wa timu hiyo siku aliposaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo.

Simba itashuka kwenye dimba la Stade du Ville, ambalo linabeba watazamaji 40,000 na kocha huyo amepanga kuwaanzisha washambuliaji wake wote wawili Emmanuel Okwi na Nicholaus Gyan baada ya Laudit Mavugo kubaki Dar es Salaam kutokana na kuwa majeruhi.

Wachezaji waliosafiri na kikosi cha Simba Makipa ni Aishi Salum Manula na Emanuel Elias Mseja. Mabeki Mohamed Hussein, Erasto Edward Nyoni, Shomari Kapombe, Ally Shomary, Yusufu Mlipili, Murshid Juuko na Kwasi Asante.

Viungo ni Mzamiru Yassin, Bukaba Paul, Shiza Kichuya, James Kotei, Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla, na Jonas Mkude.

Washambuliaji ni Emmanuel Okwi, Moses Kitandu, Nicholas Gyan na John Raphael Bocco.

Simba inahitaji sare au ushindi ili kusonga mbele raundi ya kwanza ya michuano hiyo, ambapo huenda ikakutana na Al Maasry ya Misri baada ya timu hiyo kupata ushindi wa mabao 4-0, dhidi ya Green Buffalo ya Zambia kwenye mchezo wa kwanza.