Goms yatinga fainali Ndondo

TIMU ya soka ya Goms United ya Dar es Salaam imefanikiwa kufuzu fainali ya Ndondo Super Cup baada ya kuifunga Itezi ya Mbeya kwa mabao 3-2 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Bandari, Temeke, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo ambao ulishuhudiwa na mashabiki wengi, Goms ilikuwa ya kwanza kupata bao mapema dakika ya tatu lililofungwa na Hamza Alaba.

Lakini dakika ya saba Danis David aliisawazishia Itezi bao hilo na dakika ya 20 wakaongeza bao la pili lililofungwa na Salum Upuu na kufanya kipindi cha kwanza kumalizika kwa 2-1.

Kipindi cha pili kila timu iliingia ikiwa na kasi na kuanza kushambuliana kwa zamu, lakini Itezi walionekana kuwa na kasi ya mchezo lakini makosa ya kufanya faulo karibu na eneo ya goli yaliwagharimu baada ya Goms kutumia faulo na kusawazisha bao lililofungwa na Chinedu Michael dakika ya 70.

Bao hilo liliamsha nderemo kwa mashabiki wa Goms na kuanza kushangilia na kutoa kejeli kwa Itezi, hali iliyowapa nguvu wachezaji wao na kufanikiwa kuongeza bao la ushindi dakika ya 78 lililofungwa na Hamza Alaba.

Goms ambao ni washindi wa pili wa mashindano ya Ndondo mkoa wa Dar es Salaam, wanasubiri mshindi kati ya Misosi ambao ni mabingwa wa Ndondo mkoa wa Dar es Salaam na Mnadani ya Mwanza kucheza fainali keshokutwa.

Akizungumza baada ya mchezo kumalizika nahodha wa Itezi, Romario Albert alisema mechi ilikuwa nzuri na walitawala mchezo kwa kipindi kirefu lakini walifungwa na kuwaomba wana Mbeya kuendelea kuwasaidia.

Nahodha wa Goms, Paul John alisema waliruhusu mabao mawili kipindi cha kwanza kutokana na kuidharau Itezi, hivyo kipindi cha mapumziko kocha alibadilisha mbinu na kufanikiwa kushinda.

“Pia aliwataka mashabiki wa Goms kukaa mkao wa kula kwani safari hawarudii makosa kwa sababu mara ya kwanza tuliteleza lakini safari hii wapo vizuri.