Bosi Tasma alia kufungiwa

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (Tasma), Nassoro Matuzya amepinga vikali hatua ya kufutwa katika chama hicho na kufungiwa miaka mitatu kujihusisha na mchezo wowote hapa nchini.

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lilitangaza wiki iliyopita kumfuta Matuzya na kumfungia kujihusisha na michezo kwa miaka mitatu baada ya kushindwa kuwasilisha taarifa ya michezo licha ya kutokufanya hivyo mara kadhaa.

Kaimu Msajili wa Michezo, Ibrahim Mkwawa alikaririwa akisema kuwa BMT imeamua kumpa adhabu hiyo Matuzya baada ya kushindwa kuripoti taarifa ya fedha ya Tasma.

Matuzya akizungumza jana alisema anasikitishwa na hatua hiyo, kwani ilichukuliwa na msajili kwa kusikiliza maneno ya uongo kutoka kwa viongozi wengine wa Tasma.

Alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi, kwa nini hakuwasilisha ripoti ya fedha na kujieleza kama alivyotakiwa na Msajili, alisema kuwa Kamati ya Utendaji ya Tasma ndio ilitakiwa kujieleza kuhusu hilo na sio yeye kama Matuzya, licha ya kuwa ni katibu mkuu.

“Unajua mimi niko pale kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya Tasma, hivyo kamati yetu ilitakiwa kuwajibika lakini sio mimi kupewa adhabu mwenyewe,“ alisema Matuzya.

Alisema Msajili alitoa adhabu hiyo kwa jazba baada ya kupewa maneno ya uongo, kwani angeweza kuiita kamati nzima ya utendaji ya Tasman na kupata ukweli kamili.

Alipoulizwa kama atakata rufaa kupinga adhabu hizo, alisema kwanza atakutana na wanasheria wake na kujua nini kinaendelea kabla ya kukata rufaa.

Alisema anamshangaa Msajili kuchukua hatua hiyo, kwani inawakosesha wachezaji huduma muhimu kutoka kwake.

“Msajili amekosea sana kunifungia, kwani anawakosesha wachezaji huduma yangu muhimu na ya nadra sana niliyokuwa naitoa kwao,“ alisema Matuzya.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tasma, Katibu Mkuu ndio mwenye wajibu wa kuandaa ripoti ya fedha kwa kushirikiana na mhazini na vile vile ndiye atajibu hoja zote za fedha.