Simba yatamba kuimaliza Gendermarie

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya kombe la Shirikisho Afrika, Simba leo wako ugenini Djibout kucheza mechi ya marudiano ya michuano hiyo dhidi ya Gendarmarie ya huko.

Simba inashuka kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi mnono wa mabao 4-0 waliopata wiki iliyopita kwenye Dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Vinara hao wa Ligi Kuu Bara, wanahitaji sare tu ili kusonga mbele au kama kufungwa basi wafungwe si chini ya mabao 3-0.

Kama Simba itavuka kwenda hatua inayofuata kuna uwezekano mkubwa wa kukutana na miamba wa Ligi Kuu ya Misri timu ya Al Masry ambao wao wanatarajiwa kushuka dimbani kesho kuvaana na Green Buffaloes ya Zambia ambayo kwenye mchezo wao wa awali waliifunga mabao 4-0.

Simba wamesafiri na wachezaji wao wote muhimu wa kikosi cha kwanza wakiwemo washambuliaji wao hatari, John Bocco na Emmanuel Okwi ambao wanatarajiwa kuongoza mashambulizi kwenye mchezo huo.

Akizungumza na gazeti hili saa chache kwamba ya safari hiyo juzi, Kocha wa Simba Mfaransa, Pierre Lechantre alisema, kwenye michuano hiyo amepanga kufanya makubwa ili kuandika historia ndani ya Simba kwa kuifikisha timu hiyo kwenye hatua ambayo haijawahi kufika au hata kuifanya itwae ubingwa.

Alisema kuwa hesabu zake kwenye kombe hili amezipiga mapema na anataka kuhakikisha kwenye hatua hizi za awali hapotezi matumaini, hivyo atakuwa akitoa vipigo na kujipa uhakika mapema ili hata akifika kwenye hatua ya makundi timu zingine ziwe zinamuogopa.

“Simba kwa miaka mingi haijafanya vizuri kimataifa basi mimi nataka kuandika historia ndani ya timu hii, nitahakikisha naifikisha mbali na hilo ndilo lengo langu kuu,” alisema Lechantre.

Simba inashiriki michuano ya kimataifa kwa mara ya kwanza baada ya karibu miaka mitano, kutokana na kukosa nafasi ambapo kwa kipindi chote hicho Azam na Yanga ndizo zilizokuwa zikipokezana ushiriki.