APR matumaini kibao Shirikisho

WACHEZAJI wa timu ya APR FC wana matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo wao wa marudiano dhidi ya Anse Réunion huko Shelisheli leo wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho la Afrika huko Stade Linite, Victoria. Kikosi cha APR kiliondoka juzi Jumapili kwenda Shelisheli na tayari kimeshawasili kisiwani humo tayari kwa mchezo huo wa marudiano.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika mjini hapa, APR iliibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 mbele ya mashabiki wao dhidi ya Anse Réunion.

Mabao ya APR yaliwekwa kimiani na kiungo Djihad Bizimana, 21, aliyefunga katika dakika ya 12, 70 na 90 wakati Isaa Bigirimana alifunga bao jingine katika dakika ya 78. Wakati timu hiyo ya jeshi ikijiweka vizuri kampeni zake za Afrika.

“Tunajua kibarua tutakachokuwa nacho katika mchezo wa marudiano dhidi ya Anse Réunion, hadi sasa kazi imefanyika nusu lakini tumejiandaa vizuri. Tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunashinda mchezo wa marudiano," alisema Jimmy Mulisa.

APR inatakiwa kuhakikisha haifungwi zaidi ya mabao manne katika mchezo huo wa marudiano ili kuhakikisha inaitoa Anse Réunion katika mchezo huo wa leo Shelisheli.

Wakenya Anthony Ogwayo, Oliver Odhiambo na Stephen Yiembe ndiyo waamuzi watakaoamua katika mchezo huo.

Endapo APR itafanikiwa kusonga mbele kutoka katika raundi hii, watakabiliana na Djoliba ya Mali, ambayo haijagusa mpira baada ya timu ya Liberia, Elwa United kujitoa katika mashindano hayo katika dakika za mwisho kutokana na ukata.

Tangu ilipoanza kushiriki kwa mara ya kwanza mashindano makubwa ya klabu Afrika mwaka 1997, APR haijawahi kucheza hatua ya makundi.