Mambo yaiva ujio viongozi Fifa

MAANDALIZI ya ujio wa viongozi wa Shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA) yamekamilika na wanatarajiwa kuingia nchini kuanzia leo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harisson Mwakyembe alisema serikali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wamejipanga kwa ujio huo ambapo baada ya kutangulia baadhi ya viongozi wa Fifa, rais Gianni Infantino atawasili usiku wa kuamkia keshokutwa.

“Wageni wataanza kuingia kesho (leo) na usiku wa kuamkia tarehe 22 atakuja Rais wa Fifa na asubuhi nitamfuata hotelini kwenda naye Ikulu kuzungumza na Rais,” alisema Mwakyembe.

Akifafanua zaidi Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred alisema Fifa wanakuja kufanya mkutano wao nchini ambapo kutakuwa na agenda kadhaa moja wapo ni kuhusu maendeleo ya soka la wanawake, vijana na Club Licensing.

“Soka ya vijana ni agenda yetu hata sisi kama nchi na kwa bahati nzuri Tanzania tumepata nafasi ya kuwasilisha mada kuhusu tunavyoendesha soka ya vijana”.

“Jambo lingine litakalojadiliwa ni kuhusu miradi ya maendeleo ya Fifa na vyote hivyo ni vipaumbele vya wanachama ambao ndiyo sisi,” alisema.

Rais Infantino pia ataambatana na rais wa Shirikisho la Soka AFrika, (CAF) Ahmad. Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kupata ugeni wa Fifa.