Wakongwe, chipukizi timu ya madola Kenya

KENYA imechagua wachezaji wake wanaounda kikosi cha timu ya taifa ya riadha itakayoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Gold Coast, Australia Aprili.

Kikosi hicho cha Kenya kina mchanganyiko wa wanariadha wazoefu na chipukizi, kilichaguliwa mwishoni mwa wiki baada ya kumalizika kwa jaribio kwenye Uwanja wa Moi Kasarani.

Mashindano hayo ya kuchagua kikosi cha Madola yalishirikisha wachezaji chipukizi waliofanya vizuri huku ikishuhudiwa baadhi ya wakongwe wakiachwa.

Pamoja na baadhi ya wanariadha muhimu kukacha jaribio hilo kwa sababu tofauti tofauti, Kenya bado imechagua timu nzito yenye uwezo wa kuongoza kwa mara ya tatu mfulilizo katika Michezo ya Madola.

Hata hivyo, Riadha Kenya (RK), inatakiwa kuweka njia nzuri zaidi ya kuwashawishi nyota wake kushiriki mashindano hayo. Bingwa wa Olimpiki na Dunia wa mbio za meta 3,000 kuruka gogo na maji Conseslus Kipruto na bingwa wa dunia wa meta 5,000 Hellen Obiri wamo katika timu hiyo.

Kipruto ataungana na bingwa wa medali ya shaba wa Afrika wa mbio za kuruka gogo na maji wa meta 3,000 Abraham Kibiwott na bingwa wa vijana wa mbio hizo Amos Kirui wataiwakilisha Kenya katika mchezo huo.

Kenya ndio bingwa mtetezi wa mbio za kupokezana vijiti za meta 3,000 kwa wanaume na zile za wanawake za meta 5,000 baada ya kushinda katika Michezo ya Glasgow 2014.

Wakenya Jonathan Muia na Mercy Cherono ndio walioshinda mbio hizo.