Yanga yaipania Singida United

YANGA leo imakutana na Singoda United katika mchezo war obo fainali wa Kombe la FA kwa kuumana na Singida United huku ikiwataka mashabiki wake kuondoa wasiwasi, kwani kila kitu kipo poa.

Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka nchini kutokana na ubora wa timu hizo, unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Katika kuonesha kuwa Yanga wamepania kufanya kweli, timu hiyo iliamua kwenda kuweka kambi ya takrtiban siku nne mkoani Morogoro kwa ajili ya mechi hiyo, ambapo jana ilielezwa kuwa walianza safari ya kuifuata Singida.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ameliambia HabariLeo kuwa timu hiyo imefanya maandalizi ya kutosha kuelekea katika mechi hiyo na dhumuni ni kuhakikisha wanaibuka na ushindi na kusonga mbele hivyo wanaingia mkoani humo wakiwa kamili kwa ajili ya vita hiyo.

“Kikosi kimejiandaa vya kutosha, kulikuwa na programu nyingi za kujipanga kwa ajili ya mchezo huo, ambapo mambo yamekwenda vizuri na timu ikiwa kamili tangu kwenye maandalizi Morogoro tayari kwa mchezo huo, ambao tunahitaji ushindi, tusonge mbele na kufanikisha tunalolihitaji,” alisema Mkwasa.

Mbali na ubora wa vikosi hivyo, lakini kutoshana nguvu kwa timu hizo mara mbili zilipokutana msimu huu, imekuwa sababu kubwa ya kutaka kujua nani atachanga karata zake vizuri safari hii kwa kumtoa mwenzake na kutinga nusu fainali ya michuano hiyo, ambayo bingwa ataiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mechi hizo mbili za awali, ya kwanza ilikuwa ya Ligi Kuu, ambapo Singida ililazimishwa suluhu katika uwanja wake wa nyumbani kabla ya kukutana tena kwenye Kombe la Mapinduzi katika hatua ya makundi na matokeo yalikuwa sare ya 1-1.

Upande wa pili, Mkwasa pia amezungumzia mipango inayoendelea katika kujiandaa kuwasoma wapinzani wao Welayta Dicha kutoka Ethiopia watakaoumana nao April 7, mwaka huu kuwania kufuzu kuingia kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Tunaendelea na maandalizi kama kawaida, tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye Shirikisho pia. Kocha Lwandamina (George) amekwenda Ethiopia ikiwa ni sehemu ya kuwafahamu vizuri wapinzani wetu na hiki ni kitu cha kawaida tu katika kutafuta ushindi, hufanyika duniani kote,” alifafanua Mkwasa.

Wakati Yanga ikiyaeleza hayo, Kocha Mkuu wa Singida, Hans van Pluijm ametamba kuwa wamejiandaa vya kutosha kuifunga Yanga huku akieleza jinsi gani anawafahamu wapinzani wake hao.

“Naifahamu Yanga, ni timu kubwa na yenye wachezaji wenye uzoefu wa hali ya juu na wameshiriki michuano hii kwa muda sasa. Kwa kulitambua hilo pamoja na maandalizi mengi ya kutosha tunayoyafanya kwa ajili ya mechi hiyo lakini nidhamu ya mchezo juu ya wapinzani wetu ni suala la msingi.

“Tunahitaji kuvuka kwenye hatua hii na kwenda nusu fainali tukiwa na lengo la kupata mafanikio zaidi katika kombe hili ndiyo maana kumekuwa na maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunapata ushindi katika kila mchezo ulio mbele yetu,” alisema Pluijm kocha wa zamani wa Yanga.