Simba haikamatiki

VINARA wa Ligi Kuu Bara, Simba imeendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Njombe Mji kwenye dimba la Sabasaba mkoani Njombe.

Simba ilibuka na ushindi huo ukiwa ni mchezo wa kiporo cha muda mrefu, hivyo kuongeza pengo la pointi tatu dhidi ya wapinzani wao, Yanga. Katika mchezo huo, Njombe Mji ilionekana kuanza vizuri kwa kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Simba, hali iliyowapa wakati mgumu mabeki wa Simba kuhakikisha wanawazuia Ditram Nchimbi na Mustapha Bakari, ambao walionekana moto ndani ya dakika 10 za kipindi cha kwanza. Utulivu wa mabeki wa Simba ulikuwa na faida kwa upande wao baada ya kuwadhibiti vyema wachezaji hao.

Mbinu ya kutumia mipira mirefu iliwapa faida baada ya dakika ya 17 mshambuliaji John Bocco kuipatia timu yake bao la kuongoza kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango David Kisu, baada ya kupokea mpira uliopigwa na beki Yusuph Mlipili. Vijana wa Alli Bushiri waliendelea kucheza mpira wa pasi fupifupi huku wakifanya mashambulizi mfululizo, ambapo mpaka dakika ya 25 Njombe ilikuwa na kona tatu wakati mbili kwa wapinzani wao.

Pamoja na usumbufu wa washambuliaji wa Njombe lakini umakini ulikuwa mdogo, ambapo hata hivyo hawakuweza kuona lango la wapinzani wao na kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa nyumba kwa mbao 1-0. Kipindi cha pli kilianza kwa Simba kutawala mchezo na kufanya mabadiliko ya kumtoa Okwi na kuingia Mavugo, kabla ya dakika ya 60 kutoka James Kotei ambaye aliumia na kuingia Salim Mbonde ambaye alirejea kwa mara ya kwanza.

Baada ya mabadiliko hayo dakika nne baadaye mshambuliaji John Bocco alikwamisha tena bao la pili akipokea krosi safi ya Shomary Kapombe na kufanya mchezo huo kumalizika mabao 2-0. Nahodha wa Kikosi cha Simba, John Bocco alizungumza baada ya mchezo alisema anawashukuru mashabiki na uongozi wa timu hiyo kwa kuwapa sapoti ya kila hatua na sasa wanajipanga kushinda kila mchezo ili kutimiza ndoto yao ya kuchukua ubingwa.