RIDHIWANI KIKWETE: Mtoto wa Rais aliyejitenga na mali na kugeukia siasa

SIASA si jambo ambalo kila mtu anaweza kulifanya kama ambavyo mtu hawezi kuamka tu na kuamua kuwa mwanaharakati.Ili uwe mwanasiasa ni lazima, aidha uwe umekulia katika mazingira ya kisiasa, umeipenda tangu utotoni au kujifunza shuleni, lakini kwa kuipenda.

Ni wachache sana ambao wanaamua kuacha moja kwa moja kujishughulisha na mambo yao na kujikita kwenye masuala ya siasa tu. Ridhiwani Kikwete ni mtoto wa kwanza wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete, ni mwanasheria wa kujitegemea ambaye anamiliki kampuni ya uwakili, lakini pia ni mfanyabiashara, hata hivyo mambo yote hayo ameamua kuyaweka pembeni kwa sasa kuamua kuwatumikia wananchi wake wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani na kuachana na masuala ya kutafuta mali.

Baada ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Saidi Bwanamdogo kufariki mwaka 2014, Ridhiwani aliomba ridhaa ya kuongoza jimbo hilo katika uchaguzi mdogo na alishinda kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)na kuwatumishi wanaChalinze kwa mwaka mmoja kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambako alifanikiwa kushinda tena ubunge wa jimbo hilo.

“Ukichanganya vitu hivi viwili, yaani kuwa mwanasheria na wakati huo huo kuwa mbunge au mfanyabiashara haitawezekana, mimi nimeamua kusimama kwenye ubunge tu kuwatumikia wananchi wangu wa Jimbo la Chalinze,” anasema.

Anasema katika mali za familia, yeye ni kiongozi akiwa mtoto wa kwanza,lakini imekuwa tofauti kwani wadogo zake ndio wanaoendesha shughuli hizo kwa kuwa yeye wanamuelewa kuwa sasa ana jukumu la kutumikia wananchi wa Chalinze. “Familia yanguina miradi kadhaa ambayo nimewaachia wadogo zangu wafanye kwasababu nimeamua kufanya kazi ya siasa ambayo naipenda kwa dhati na hasa kuwatumikia wananchi wenye shida…,” anasema.

Alianza lini siasa?

Akielezea historia yake ya kisiasa, anasema damu ya siasa ilichemka baada ya kucheza gwaride mbele ya Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere akiwa ni kijana wa miaka sita na baadaye kuendelea na kushiriki gwaride hilo mpaka alipohitimu shule ya msingi.

Anasema hata hivyo alipoingia Chuo Kikuu alijiunga rasmi na siasa na kwamba moto aliopata kutokana na siasa za chuoni, ndio huo umemchochea hadi leo na haujawahi kuzimika. Hata hivyo, anasema hajawahi kushawishiwa na baba yake, Dk Kikwete kugombea nafasi yoyote katika siasa, lakini wakati wote amekuwa akimsaidia kwa kumshauri na kumtia moyo ili aweze kufanikiwa.

“Mzee wangu amekuwa akinisaidia sanaili nitimize majukumu yangu, nikitaka kugombea najipima mwenyewe kwanza, japo huwa namwambia,lakini hajawahi kunikatalia, kama ningekuwa simfurahishi namjua mzee wangu angeniambia,” anasema Ridhiwani. Mbunge huyo wa Chalinze anasema amekuwa pia daraja zuri kati yake yeye kama mbunge na wananchi, “mzee ni mtu wa watu, anaposikia jambo lolote ambalo halijakaa vizuri basi ataniita na kuniambia, bwana hili rekebisha halijakaa vizuri, kwahiyo amekuwa akinisaidia sana.”

Ridhiwani anasema sasa yeye nikiongozi na Kikwete(Baba) ni mwananchi wake kwasababu anaishi kama mwananchi na anafurahi kuendelea kuchota busara za kiongozi huyo. Anasema kuna maneno watu wanasema yeye ni mtoto mpenzi wa Dk Kikwete, “matarajio ya mzazi ni kumuona mtoto wake anafanikiwa, kwahiyo kwa kuniona nafanikiwa katika jambo ninalolipenda anafurahi sana… hapo ndipo watu wanatafsiri ananipenda sana mimi,lakini ni kama tu mapenzi ya mzazi kwa mtoto.”

Kwanini kipenzi cha baba? Kijana huyo aliyezaliwa Aprili 16, 1979 katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, anasema wakati anazaliwa wazazi wake walikuwa wakiishi Arusha, lakini baba akiwa vitani Uganda na alipopata habari za kuzaliwa kwa mtoto wake wa kwanza, alirejea kuja kumwona.

”Lakini kwasababu kipindi kile kilikuwa ni cha Vita ya Kagera, mama alirudi nyumbani kwetu Bagamoyo kwasababu ya hali ya ujauzito wakati mzee amekwenda kupigana vita ya kumuondoa Nduli Iddi Amini,” anasema na anaongeza kuwa baada ya kupata taarifa ya kuzaliwa kwake kama mtoto wa kiume na hasa akiwa ni mtoto wa kwanza katika familia, baba yake alirudi Bagamoyo kumuona mtoto na alifurahi sana.

“Hii nilihadithiwa tu kwamba familia ilikuwa na furaha kubwa baada ya mimi kuzaliwa, naambiwa hata bibi yangu mzaa baba alitoa fedha ya chakula akamnunulia mama yangu kanga, fikiria maisha ya wakati huo bibi anajishughulisha na kilimo tu, na kwetu huku Pwani kununua kanga ni jambo kubwa sana,” anasema.

Anasema mwaka 1983 alikwenda kuishi Arusha tena na wazazi wake, lakini mwaka 1985 babu yake Mrisho Kikwete ambaye ni baba yake na Dk Kikwete aliomba arudishwe Bagamoyo hivyo alirudi na alianza shule ya awali.

Alisoma shule ya awali shule ambayo ilikuwa kwaajili ya Jeshi la Polisi na anakumbuka alikuwa akifundishwa na mtu anayemkumbuka kwa jina moja la mama Mayala. Anasema wakati huo wote baba yake alikuwa ni mwanajeshi anafundisha Chuo cha Jeshi Monduli, lakini baadaye mwaka 1984 wazazi wake walitengana ingawa mwaka 1981 alikuwa ameshazaliwa mdogo wake, Salama Kikwete ambaye sasahivi ni daktari.

Mbunge huyo anasema mwaka 1985 yeye akiwa na umri wa miaka sita zilifanyika sherehe za miaka minane ya CCM ambayo ilifanyika kitaifa Bagamoyo na anakumbuka mama mmoja ambaye alikuwa Katibu uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ambaye pia alikuwa akisimamia kikundi cha chipukizi, kwa jina la mama Martha Thomas alikusanya vijana wengi wa Bagamoyo kwaajili yagwaride, yeye akiwa miongoni mwao.

“Ilikuwa ni hivi tukitoka saa saba shule tunakuta ugali, tukishakula ikifika saa tisa tunakwenda kucheza CCM ambapo kulikuwa na mabembea na saa 11 jioni tunakwenda madrasa,” anasemana anaongeza kuwa mama huyo alikuwa anawepeleka kwenye ukumbi wa jengo hilo la CCM na kuanza kuwafundisha kama masomo ya ziada tena bila malipo yoyote.

Anasema ni hapo alipata nafasi ya kucheza gwaride mbele ya Rais wa wakati huo, Mwalimu Nyerere jambo ambalo lilimhamasisha sana kuwa na hamu naye siku moja aje kuwa mwanasiasa. “Kwa kweli kwangu ilikuwa kama ndoto, ilikuwa furaha kubwa mno na sisi watoto unajua ni kikosi cha kwanza baada ya brassband na mimi nilikuwa kiongozi wa kundi letu lile,” anasema.

Kwa kumbukumbu zake jioni ya siku hiyo aliambatana na babu yake kwenye hafla ya chakula cha jioni na Mwalimu Nyerere ambaye alialika wazee wa Bagamoyo, babu yake alikuwa ni mstaafu baada ya kutumikia serikali alikuwa Mkuu wa Wilaya katika wilaya kadhaa ikiwa ni pamoja na wilaya hiyo.

“Babu yangu alinitambulisha kwa Mwalimu Nyerere kwamba ni mtoto wa Jakaya, alionesha anamjua sana baba yangu nikashangaa sana, babu yangu ni mwanajeshi anafahamika vipi kwa Rais, lakini baadaye nilikuja kuambiwa kuwa baba aliwahi kufanya kazi Ikulu kabla sijazaliwa,” anasema Ridhiwani. Anasema mama Martha amechangia kwakiasi kikubwa kumfanya kukipenda Chama cha Mapinduzi.

“Unajua kwetu Pwani huku wanawake ndio wanalima, bibi atakwenda shamba na babu alikuwa anasuka majamvi, babu alikuwa anaona sehemu nzuri nitafurahi ni pale CCM, na aliyenifanya niipende hasa CCM ni huyu mama kwa sababu alikuwa akitufundisha masomo ya ziada, anatupa pipi na biskuti, watoto tukajikuta tunafurahi kuwa karibu na chama.”

Ridhiwani anasema akiwa Bagamoyo wakati wote huo alikuwa akiishi na babu na bibi zake ambapo babu yake alikuwa na wake wanne. “Wakati naishi na babu na bibi, inafurahisha sana, babu alikuwa ana wake wanne kwahiyo wakati mwingine mimi nalala kwa bibi huyu, nahamia kwa bibi huyu, nyumba sasa ikawa na wanaume wawili kwenye nyumba moja,” anasema.

Anasema mwaka 1986,Dk Kikwete alichaguliwa kuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nachingwea, aliwachukua yeye na dada yake Salama na kwenda kuishi na baba yao ambapo alianza darasa la kwanza Shule ya Msingi Matangini na baadaye kuhamia Masasi alikosoma Shule ya Msingi Mkomaindo.

Ridhiwani anasema aliendelea kushiriki gwaride na kujifunza itikadi za CCM mpaka mwaka 1989 ambapo walihamia rasmi Dar es Salaam akiwa na baba yake ambaye wakati huo alikuwa ameshakuwa Mbunge na pia Naibu Waziri wa Maji, alianza kusoma Shule ya Msingi Forodhani darasa la tatu mpaka la saba.

Anasema akiwa shule hiyo ya Forodhani aligombea uenyekiti wa chipukizi na ujumbe wa mkutano mkuu wa chipukizi taifa mwaka 1992 akapata nafasi ya ujumbe hivyo akaenda Mbeya kwenye mkutano na hiyo ikawa mara yake ya kwanza kusafiri peke yake, ujumbe huo ulikoma mwaka 1997.

“Nakumbuka koti langu la kwanza katika maisha yangu, nilikuwa sijawahi kuvaa koti, alininunulia baba baada ya kumwambia nakwenda kwenye mkutano Mbeya, akaniambia kuna baridi sana huko bwana twende tukanunue koti,” anasema. Ridhiwani anasema baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Shabaan Robert ambapo hakutaka tena kujihusisha na gwaride na baadaye alisoma kidato cha tano na sita Shule ya Sekondari ya Mkwawa, Iringa.

Anasema akiwa Mkwawa alikwenda kuonana naRais wakati huo Benjamin Mkapa, yeye alikwenda kama kijana aliyeshiriki kumpokea Rais wakiratibiwa na Rajab Luhavi ambaye sasa ni Balozi nchini China. “Jioni tuliitwa na tukashawishiwa sana tuendelee kufanya shughuli za siasa, lakini sikuendelea niliogopa masomo yalikuwa yamepamba moto, hivyo mimi niliendelea na shule yangu na baadaye kumaliza na kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Sheria,” anasema.

Ridhiwani anasema akiwa chuo chachu mpya ya siasa iliibuka tena baada yakushiriki katika harakati za kuwapata viongozi wa chuo. “Tulipofika Rais wa Chuo alikuwa Kitila Mkumbo ambaye sasahivi ni Katibu Mkuu, zikatokea fujo fujo pale, viongozi wanachaguliwa na kutolewa, lakini baadaye taarifa zimeshasambaa kuna watoto wa mwaka wa kwanza hapa wamekuja sio mchezo, kweli walitutafuta na tulisaidia sana kwenye siasa za chuo,” anasema.

Ridhiwani anasema baadaye alichaguliwa kuwa Waziri Msaidizi waSerikali ya Wanafunzi na waziri wake alikuwa Mbunge wa Kawe wa sasa, Halima Mdee wakishughulika na wanafunzi wa kimataifa na siasa. “Serikali yetu ilikuwa balaa, katibu wa serikali ya wanafunzi alikuwa Mbunge huyu wa Kigoma, Kabwe Zitto na spika alikuwa Mwanasheria Albert Msando, ilikuwa hatari sana,” anasema.

Anasema mwaka wa pili aliamua kugombea nafasi ya uenyekiti wa kitivo cha sheria na akashinda na baadaye pia akaanza kujihusisha na siasa kwa ujumla ambapo aliteuliwa katibu uhamasishaji wa CCM wilayani Bagamoyo. Ridhiwani anasema wakati huo mbunge wa Jimbo la Bagamoyo alikuwa Kikwete ambapo kamati yake ilimsaidia kuanzisha ujenzi wa shule za sekondari za kata.

“Unajua ujenzi wa shule za kata kwenye serikali ilikuja kuanzishwa baadaye, lakini Kikwete alikuwa ameshaanza katika jimbo lake na tulianza kwenye kata ya Mbwewe tukajenga shule ya kwanza,” anasema na kuongeza kuwa baadaye mwaka 2008 aligombea ujumbe wa Baraza Kuu la CCM taifa.

Anasema kilichomrudisha kwenye siasa kwa nguvu kubwa ni siasa alizokuwa anazifanya akiwa chuo kikuu na kwamba yeye ni muasisi wa shirikisho la vyuo vikuu. Kwa mujibu wa Mbunge huyo kijana, akiwa na vijana wenzake waliwahi kukutana na Rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa kuzungumzia ni jinsi gani ya kuboresha mfumo wa siasa za vyuo vikuu, anasema wakiwa chini ya mlezi wao mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru walifanikiwa kufungua tawi la Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Anakumbuka kipindi alichoishi na Zitto bweni moja chuo kikuu, “sasa huyu mwenzetu wakati wote anahubiri Chadema, sisi mioyo yetu ina CCM, tukaona tusipofanya shughuli ya kukitangaza chama chetu tutapoteza vijana wengi, hata hivyo alikuwa ameshakusanya vijana wengi.”

Ridhiwani anasema akiwa na vijana wenzake ameshiriki kukusanya mali za chama hicho.Akiwa mwenyekiti kamati ya uchumi ya UVCCMna mjumbe wa kamati ya utekelezaji, anasema alishiriki kuhakikisha wanazikusanya mali za chama nchi nzima.“Mimi nikiwa kama mwanasheria wenzangu wakanipa jukumu la kuweka mikataba vizuri, niliunda kamati yangu kwa kushirikisha wanasheria wa chama na wanasheria wengine na viongozi wa umoja wa vijana, tuliweza kufanikiwa kwa kiasi kukubwa katika jambo hilo,” anasema.

Anasema walifanya kazi ya kurekebisha mikataba, kutambua mali na kuziorodhesha mali zote nchi nzima baada ya kutembelea mikoa mingi yenye miradi shughuli iliyofanyika mwaka 2008 na 2009. Ridhiwani anasema mali ambazo zilikuwa na migogoro na hasa kwenye viwanja waliweza kutatua migogoro hiyo, kutafutia hati viwanja na pia kuondoa migogoro na utata uliokuwepo katika maeneo hayo.

Anasema pia awalifanikiwa kuanzisha miradi mipya ya chama ikiwa ni pamoja na jengo linalojengwa sasa la Umoja wa Vijana lililopo Upanga, Dar es Salaam. “Jambo ambalo linabaki kuwa kumbukumbu nzuri kwangu ni ile kupita nchi nzima na kufanya rejea ya mali za umoja wa vijana, kuondoa migogoro na kupata hati za mali za chama,” anasema.

Ridhiwani anasema nje ya siasa yeye ni mtu wa marafiki kama alivyo baba yake, na katika marafiki hachagui ni wa aina gani ingawa watu wanamhusisha na tuhuma mbalimbali ambazo wanahisi wanafanya. “mimi sichagui rafiki bwana na ndio maisha amenilea mzee wangu, sijawahi kuchagua rafiki, na siwezi kukataa urafiki na mtu, kama kuna mambo mabaya wanafanya mimi siwezi kuyajua, mambo mengi wanazungumza kunihusu mimi na wengi wa watu hao hata hawanifahamu,” anasema.

Ridhiwani ni baba wa watoto watatu ambao niAziza, Aiman na Jamil anasema anapenda kuangalia mpira, kucheza na watoto wake pamoja na watoto wa wadogo zake. Anasema mtu anayemvutia katika siasa na uongozi ni baba yake, Dk Kikwete ambaye amemlea katika misingi ya siasa mpaka sasa anaendelea kumsimamia na kumshauri.

“Amenifundisha kupenda watu, kuishi na watu, kuhudumia watu na ni matokeo yanalipa leo, amekuwa mfano wa uongozi kwangu kuwa kiongozi wa kuacha alama na kumbukumbu katika vichwa vya watu, kwangu mimi Dk Kikwete bado anaendelea kuwa kiongozi bora ninayemuangalia katika siasa za sasa,” anasema.

Ridhiwani anasema Mwalimu Nyerere ni mfano anaoutazama katika maisha yake pia, kwasababu ameleta msingi wa amani, ushirikiano na kuwaunganisha watanzania kuishi kama familia moja na pia alikua ni kiongozi anayekubaliana na maamuzi ya watu wengi na alikubali kukosolewa.

Ubunge wa Salma Kikwete Anasemakuteuliwa kwa mama yake, Salma Kikwete na Rais Magufuli kuwa ni jambo jema kwake. “Kuwa bungeni na mama ni jambo jema, kila mtu ana jambo lake mimi ni Mbunge wa Chalinze na yeye wa kuteuliwa, lakini nitaendelea kujifunza kutoka kwake,” anasema.

Ridhiwani anasema Salma ni mama yake aliyemlea na siku zote wamekuwa wakishirikiana kwa mambo mengi kama familia.