EVANGELINE MEENA: Mchoraji na mchongaji mwenye ndoto za kimataifa

UMBO, sura na kimo chake kinaweza kukuaminisha kabisa kwamba ni mwanamitindo ama mshiriki wa mashindano ya ulimbwende, ndivyo anavyoonekana mwanadada Evangeline Meena.

Evangeline mwenye umri wa miaka 23, ni mwanadada mrefu, mwenye sura nzuri, umbo zuri na mcheshi ndio maana kwa mtazamo wa haraka utasema ni mwanamitindo au mlimbwende, lakini tofauti na mtazamo huo binti huyu ni msanii na mbunifu wa sanaa za mikono. Mwenyewe anasema ‘I am an Artist and Designer’.

Nilipata fursa ya kufanya mahojiano naye katika ofisi za makao makuu ya Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN) linalochapisha gazeti hili na magazeti dada ya HabariLeo toleo la kila siku, Daily News, Sunday News na SpotiLeo eneo la Tazara, Dar es Salaam hivi karibuni baada ya kuvutiwa kuona binti mdogo akifanya kazi ya sanaa kwa mapenzi yake yote.

Ukikutana na Evangeline na kuzungumza naye utakubaliana nami kuwa ni kitu anachofanya kwa mapenzi yote kwa lugha ya kiingereza tunasema, ‘with passion’, kwa jinsi anavyoelezea kwa shauku na mwenye ndoto ya kujiona akifika mbali na sanaa yake. Kazi anayofanya binti huyu ni uchoraji picha, kubuni mapambo kutumia mbao, nyuzi na misumari.

Picha na mapambo hayo unaweza kuweka ukutani, kwenye kumbi na kadhalika, lakini pia anachonga majina au maneno ambayo unaweza kuweka ukutani au mlango au sehemu yoyote. Mbali na uchoraji na uchongaji, lakini pia anafanya kazi ya kushauri watu jinsi ya kuzipamba nyumba zao, ofisi na kadhalika pamoja na kuwauzia mapambo ama picha wanazoweza kuweka kunogesha mandhari.

“Nafanya ‘home decor’ huwa namshauri mtu jinsi ya kuweka mazingira mazuri ya nyumbani kwake, ili hata mgeni anapoingia avutiwe na namna nyumba ilivyopangiliwa vizuri kuanzia samani hadi mapambo na vitu vingine vilivyomo katika nyumba,” anasema. Evangeline anasema kazi za uchoraji na uchongaji huzifanya mwenyewe nyumbani na kwamba ni kitu alichokuwa akipenda na kutamani tangu akiwa na umri mdogo.

Msanii huyu, elimu ya msingi ameipata jinsi ya kufanya sanaa yangu na kuiboresha, ndoto yangu ni kuliteka soko la kimataifa,” anasema kwa kujiamini. Hata hivyo, kwa mtazamo wake anasema jamii haiichukulii sanaa hiyo kama kitu makini ndio maana hupuuzia, tofauti na wageni kutoka nje ambao huthamini sanaa.

Anasema kwa mtazamo wake na tangu alivyoanza kushughulika na sanaa hiyo, anaona kama wanawake ni wachache na anaongeza kuwa yeye kwa kuwa aliipenda kazi hiyo, aliguswa akajitosa Mwenge, akawa anauliza maswali kwa wazoefu na kisha aliamua kutoka na kitu chake.

Katika kila kazi au jambo hakukosekani changamoto, ndivyo ilivyo pia kwa Evangeline na kazi zake kama anavyoeleza. Anaainisha kwanza wateja wagumu; hapa anafafanua kuwa wateja ni wagumu kuelewa na inakuwa ngumu kuwaelekeza na matokeo yake mara nyingine husababisha kutopata wanachohitaji na humuongezea yeye ugumu katika kuifanya kazi.

Pili suala la mawasiliano; kuna kikwazo katika lugha, maana kuna baadhi ya wateja hawazungumzi kiingereza wala kiswahili hapo maelewano yanakuwa ni shida. Jambo lingine ni kukabiliana na mabadiliko; inakuwa vigumu kubadilisha ubunifu baada ya mteja kubadilisha maamuzi ya oda aliyotoa awali na matokeo yake kama msanii anapata hasara.

Suala lingine ni uwezo wa kubuni; ndio inahitajika ubunifu wa hali ya juu na kwamba saa 24 mbunifu anatakiwa kufikiria ubunifu na chochote na kazi yoyote atakayoletewa mbele yake awe na uwezo wa kuifanya, yaani akili yake wakati wote iwe katika uwezo wa kubuni rangi na mapambo.

Jambo la tano ni kuwa na ujuzi mpya na utaalamu; mrembo huyu anasema ipo haja ya kusoma zaidi ili kupata mawazo mengi mapya, kuongeza uelewa wa sanaa na kuwa msanii mwenye weledi. Lingine ni mtaji; Evangeline anasema fedha za kuanzia ni kidogo, lakini vitu na matumizi ni makubwa, jambo linaloleta matatizo makubwa kwa msanii mchanga.

Changamoto ya saba ni kazi nyingi ambapo anaeleza kuwa anapata kazi nyingi za kutengeneza na kutakiwa kuziwasilisha kwa mteja kwa wakati, mara nyingine anachoka kwani anatumia nguvu nyingi na akili. Vitendea kazi navyo ni changamoto kubwa kwake, kutokana na upungufu huo mara nyingine humuwia vigumu kukamilisha kazi kwa wakati.

Kitu kingine ni ‘too many distraction’, kwa sababu anafanyia kazi zake nyumbani, anapata usumbufu mwingi, kelele kutoka nje, kwa hiyo anashindwa kumakinika kwenye kazi. Mwisho anasema muda; mara nyingine muda hautoshi kufanya kazi zote za watu na kukamilisha kwa wakati.

Hizo ni changamoto ambazo anazokutana nazo Evangeline katika shughuli zake za kila siku, lakini anasema kamwe haziwezi kumrudisha nyuma na zaidi kila siku anafikiria namna mpya ya kukabiliana nazo na ndio maana moja ya malengo yake ni kutafuta wasaidizi, lakini pia kupata sehemu bora zaidi ya kufanyia kazi zake.

Je, gharama za kazi zake zikoje? Evangeline anasema kwa picha za kuchora anazoziita kuwa ni ‘Abstract Paints’ ambazo anaeleza kuwa ni ngumu kutengeneza, huwa zinaanzia shilingi 250,000 na kuendelea.

“Hizi ni picha complicated kidogo, unatumia rangi… mfano unaweza ukamwagia rangi mbalimbali, ukazivuruga, zikatoka namna fulani hivi, ni ngumu kueleza kwa maneno ndio maana nasema complicated,” anasema.

Kwa picha anazoziita ‘Fine Art’ anasema hizo huchorwa, taswira inaweza ikawa mtu au mnyama zenyewe anaanzia shilingi 100,000 na kuendelea wakati kazi anazotumia mbao huanzia shilingi 30,000 na bei huongezeka kulingana na ukubwa wa maneno na mbao.

“Unajua mtu akiniona hivi nilivyo haamini naweza kufanya kazi hizi za mikono…lakini mimi nanunua mbao, nazikata, naranda, napiga msasa, kisha napaka polishi na kisha naanza kutengeneza kutumia nyuzi na nyingine rangi kulingana na mteja anataka nini,” anasema.

Anatoa ushauri kwa vijana wenzake kuwa wakifuate kile wanachopenda kufanya kama ni sanaa, michezo na kadhalika na kwamba bila wenyewe kuchukua hatua hawawezi kufikia malengo yao. “Usione aibu kwa kile unachopenda kufanya, kuwa tayari, washirikishe watu, wala usisikilize watu wanasema nini.

Mimi watu walikuwa hawanielewi, sikuona aibu, nilijitosa nikaenda Mwenge, nikauliza kila nilichotaka kufahamu na leo hii nafanya kile nikipendacho… hata wazazi mwanzo hawakunielewa lakini baada ya kuona ninachofanya wamenikubali,” anasema.

Ushauri wake kwa wazazi, anasema wazazi wawe marafiki na mtoto au watoto ili kumfahamu na kujua anapenda au wanapenda nini, kutambua vipaji vyao na kama kuviendeleza waviendeleze pamoja na kuwatia moyo ili watimize ndoto zao.

Evangeline mwenye ndoto ya kuona anafika mbali zaidi kwenye kazi zake za sanaa na ubunifu anafungua kampuni yake itakayojulikana kama Deal Designer Design ambao kwa maelezo yake inaeleza yeye ni nani hasa.

Mrembo huyu anayeishi Kimara Baruti, Dar es Salaam ni mtoto wa Godwin Meena (mstaafu) anayejishughulisha na kazi zake binafsi na Esther Godwin ambaye ni mjasiriamali. “Tuko watoto saba, mimi ni mtoto wa sita na katika watoto wa kike mimi ni wa nne,” ndivyo anavyoielezea familia yake.

Anasema akiwa hafanyi kazi zake za sanaa na ubunifu, hupenda sana kusoma vitabu, kuogelea, kucheza na kusikiliza muziki. Huyo ndiye Evangeline, msanii na mbunifu wa kazi za mikono ambaye anasema anafanya kazi yake hiyo kwa juhudi na maarifa kwa sababu ukweli ni kuwa anafahamu familia yake ilivyojitoa sana kwa ajili yake kupata elimu nzuri na kumuunga mkono kazi zake za sanaa, hivyo atakapofanikiwa watajivunia kuwa na msanii ndani ya familia.