GEOFFREY MWAMBE: Tumaini jipya sekta ya uwekezaji nchini

KIJANA msomi aliyebobea katika masuala ya uchumi, Geoffrey Mwambe, ndiye Mkurugenzi Mpya wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC). Anakuwa Mkurugenzi wa tano kushika washifa huo moja kwa moja, wa kwanza akiwa Sir George Kahama aliyefuatiwa na Samuel Sitta, Emmanuel Ole Naiko na Julieth Kairuki.

Raymond Mbilinyi na Clifford Tandari waliwahi kukaimu nafasi hiyo kwa nyakati tofauti. Ameshika wadhifa huo baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli Mei 17 mwaka huu akitokea Manyoni mkoani Singida alikokuwa Mkuu wa Wilaya ili kuziba nafasi ya Tandari aliyekaimu nafasi hiyo kwa takribani mwaka mmoja, lakini sasa akipangiwa majukumu mengine ya kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro.

Mara baada ya kuanza majukumu yake katika taasisi hiyo yenye majukumu ya kuishauri Serikali kuhusu masuala ya uwekezaji; kuchochea uwekezaji wa ndani na wa nje; kuwezesha wawekezaji wa ndani na wa nje na pia kuchochea na kusaidia ukuaji Ujasiriamali Mdogo na wa Kati (SMEs) nchini, Mwambe amekuwa na la kusema.

Katika mazungumzo yaliyozaa makala haya, anasema moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha nchi inanufaika na wawekezaji. Aliongeza kuwa, kamwe hatavumilia kuona wawekezaji wa ndani na kutoka nje ya nchi wasio na nia njema kwa maendeleo ya taifa wakipata nafasi ya kutimiza azma yao.

vivutio vya utalii kwa pamoja. Kwa mambo hayo, anaamini ataweza kutekeleza vyema majukumu aliyopewa na Rais Magufuli na hata kumtangaza kuwa Mkurugenzi mpya wa TIC. Lakini kwa Mwambe, zaidi ya kuaminiwa na Rais Magufuli, pia ni mchapakazi aliyejipambanua katika sehemu zote alizowahi kufanya kazi.

Akiwa mwanafunzi wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwambe alifanya vyema katika masomo yake na baada ya kuhitimu alibaki chuoni hapo kufundisha huku akiendelea na masomo ya ngazi ya Shahada ya Pili katika uchumi.

Anakumbuka miongoni mwa aliowafundisha ni pamoja na wachumi na wanasiasa mahiri kwa sasa, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, lakini pia Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini na kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo.

Umahiri wake katika uchumi ulimpa fursa za kuajiriwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambako alikuwa mchumi mwandamizi kwa miaka kumi kabla ya kuhamishiwa iliyokuwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki alikokuwa Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji.

Kote alipata mafanikio makubwa na hata kuwa mfano wa kuigwa. Ndiyo maana haikushangaza kuona mara kwa mara akiiwalisha nchi katika mikutano mbalimbali ya wataalamu wa uchumi.

Akiwa mchumi, ana ushauri gani juu ya ushiriki wa Tanzania katika Mkataba Ushirikiano wa Kibiashara baina ya Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na wenzao wa nchi za Umoja wa Ulaya (EU)?

“Kwa hili naomba niseme kwamba lilishatolewa msimamo na Mheshimiwa Rais Magufuli kuwa kwa sasa nchi yetu haijawa tayari kusaini hadi masuala ya msingi katika rasimu ya mkataba ule yapatiwe ufumbuzi.

“Na msimamo huu ulibainishwa wazi na timu ya Tanzania kwenye majadiliano ambapo ripoti ya mwisho ya majadiliano yaani Joint Conclusion mwaka 2014 mjini Brussels, Ubelgiji ilionesha maeneo ambayo Tanzania haijaridhika nayo,” alisema Mwambe, baba wa watoto watatu ambaye ni mzaliwa wa Masasi, mkoani Mtwara.

Kuhusu TIC TIC ilianzishwa mwaka 1997 kwa Sheria ya Uwekezaji Tanzania ili iwe “Taasisi kuu ya Serikali ya kuratibu, kuhimiza, kukuza na kuwezesha uwekezaji nchini na kuishauri kuhusu sera ya uwekezaji na masuala yanayohusiana na uwekezaji”.

Inashughulika na uwekezaji wote wenye mtaji usiopungua Dola za Kimarekani 300,000 (Sh milioni 630) iwapo mmiliki ni raia wa kigeni au Dola za Kimarekani 100,000 (Sh milioni 210) iwapo mmiliki ni raia wa Tanzania.

Ni taasisi yenye jukumu la kusaidia wawekezaji wote kupata vibali, idhini na kadhalika ambavyo vinatakiwa kwa mujibu wa sheria nyingine ili kuanzisha na kuendesha uwekezaji nchini