MISHI SINGITA Mwongoza watalii mwanamke anayetikisa

WANAWAKE nchini na duniani kote wamekuwa wakisisitiza usawa wa kijinsia katika sekta mbalimbali ikiwamo kwenye suala zima la ajira. Katika sekta ya ajira wanawake kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakatisha tamaa na kujikuta baadhi ya ajira wakizikwepa na hivyo zinakuwa ni za wanaume zaidi.

Lakini hiyo si kwa mwanadada Mishi Singita ambaye licha ya kuwa kazi ya kuwaongoza na kuwaelekeza watalii mbugani imekuwa ikidhaniwa kuwa ni ya wanaume zaidi lakini yeye amedumu katika kazi hiyo na kwa sasa anawakilisha vema.

Mishi ameweza kufanya kazi hiyo ya kuwaongoza watalii hasa kwenye mbuga kubwa kwa mafanikio makubwa hata kuliko wanaume ambao wanadhaniwa kuwa wana uzoefu mkubwa na ndio wanaofaa kutokana na kuwepo kwa misukosuko mingi iliyopo.

Jinsi alivyopata kazi Mishi ambaye ni mama wa mtoto mmoja anasema kuwa tangu akiwa mtoto mdogo alikuwa akipenda zaidi masuala yanayohusiana na wanyama na mambo mengine yahusuyo sekta ya utalii.

Anasema mara alipomaliza kusomea kozi ya Uhasibu katika Chuo cha Uhasibu Arusha aliamua kutafuta kazi huku kipaumbele chake kikubwa kikiwa ni kuomba kupewa kazi ya Uhasibu katika hoteli mbalimbali.

Anasema hata hivyo haikuwa rahisi kwake kupata kazi aliyokuwa akiitarajia na badala yake alijikuta akipata kazi kwenye Kampuni ya Habari na Matukio iliyokuwa ikijihusisha na uaandaji wa majarida yenye kueleza matukio mbalimbali ya mkoani Arusha yakiwemo masuala yahusuyo utalii. Anasema aliweza kufanya kazi hiyo kwa bidii na ufanisi huku akijikita katika uandishi wa masuala ya wanyama kwa muda mrefu hadi baadaye alipoamua kuacha kazi hiyo.

Anasema mara baada ya kuacha kazi hiyo aliamua kurejea katika fani yake ya uhasibu ambapo alifika katika Hoteli ya Singita Grumeti Reserve kujaribu bahati yake na kuomba kazi ya uhasibu ambayo hata hivyo hakufanikiwa kuipata.

Anasema kuanzia hapo ndoto yake ya kuona anafanya kazi ya Uhasibu aliyoisomea ilianza kutoweka, lakini kwa sababu alikuwa akijua matumizi ya kompyuta na pia alikuwa akiimudu vema lugha ya Kiingereza alipewa kazi nyingine hotelini hapo.

“Niliweza kupewa kazi ya kuwa naingiza taarifa za wanyama wa aina mbalimbali kwenye kompyuta huku nikiwa na jukumu pia la kutafsiri lugha katika mawasiliano ya maofisa wa hoteli na watu waliokuwa wakihusika na kukabiliana na ujangili. “Wakati nikijihusisha na kazi hii pia nilikuwa natumia muda wangu kujifunza masuala mbalimbali yahusuyo wanyama na utalii pia.

Kwa vile suala la wanyama na utalii lilikuwa ndani ya damu yangu niliweza kufanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa na hivyo niliweza kuwavutia mabosi wangu,” alisema. Anasema siku moja ilitokea nafasi ya kuongoza watalii (tour guide) ambayo ilitangazwa ndani kwa ndani na hivyo kuwapa fursa ya wafanyakazi wa ndani ya hoteli hiyo kuomba. “Nakumbuka siku hiyo nilikuwa naendelea na kazi yangu ya kawaida ya kuhifadhi taarifa za wanyama ndipo nilipoona tangazo kuwa anatafutwa tour guide.

“Kwangu niliona tangazo lile kama muujiza kwa kuwa wakati wote nilipokuwa nafanya kazi ya kuingiza taarifa za wanyama kwenye kompyuta na kutafsiri lugha kwa wazungu waliokuwa wakiwafundisha vijana kupambana na ujangili, nilijikuta nikivutiwa sana na kazi ya kuwaongoza watalii.

“Kifupi ni kwamba wakati nikizunguka kwenye kufanya kazi za kutafsiri nilijifunza mengi zaidi huku pia nikiwa najiona kabisa kuwa nina kitu cha zaidi cha kuweza kufanya kwenye sekta nzima ya utalii.

“Nilikuwa najiuliza sasa kama nahusika na sensa ya wanyama hadi kujua samba wangapi wamezaliwa au wamekufa na si simba tu hata wanyama wengine wengi tu ni kwanini nisiwe muongoza watalii.”

Anasema baada ya kuzingatia hoja hizo zote aliamua kuomba nafasi hiyo ya kuwa tour guide na haraka akaandika barua na wakubwa wake walivutiwa na hatua hiyo na kisha haraka walimkubalia.

Anasema, alipoambiwa kuwa amekubaliwa alijiona ni zaidi ya mwenye bahati kwa kuwa kwanza ilikuwa ni siku ambayo alikuwa akiisubiri kwa hamu. Anasema baada ya kukubaliwa haraka alikimbilia kwenye gari ambalo kwa muda huo ndilo alikuwa akitakiwa kulitumia kama mtu wa kuwaongoza watalii ili kuanza kazi mara moja.

Maisha yake kazini Mwanadada huyu anasema kuwa siku hiyo alipoambiwa amekubaliwa na kwenda kwenye gari alikumbuka kuwa anajua kuendesha gari ila alilokuwa akijua kuendesha lilikuwa ni yale ya automatic gear.

Anasema kuwa kwa kawaida waongoza watalii wapo wa aina mbalimbali, wapo ambao wanakuwa pembeni mwa dereva na wanawaelekeza watalii lakini kwa upande wake yeye ni dereva na yeye ni mwongoza watalii.

Anafafanua kuwa alikuwa akijua fika kuwa hiyo ndio kazi ambayo angepata ya kuwa anawaongoza watalii na wakati huo huo kuwa dereva wa gari. Anasema kuwa alilazimika kujifunza kuendesha gari hilo lisilotumia gia automatic na haikumchukua muda akaanza kazi kama kawaida. Anasema kwa kuwa taarifa za wanyama na namna ya kuwaongoza watalii alikuwa akijua kwa upande wake haikumuathiri kufanya kazi hiyo.

Anasema aliendelea na kazi yake hiyo kwa miaka kadhaa na mwanawe wa kwanza amempata akiwa kwenye kazi hiyo na kwamba hata alipopata ujauzito aliendelea na kazi bila kusimama hadi siku za kujifungua zilipokaribia.

“Unajua kuna wakati unaweza kuwa unapenda kitu na unakifanya kwa mapenzi yote na hicho ndio kilichonitokea mimi. Kutokana na kuipenda kazi hii kuna wakati hata sikuona kama ninatakiwa kupumzika niliendelea kupiga kazi,”anasema.

Anaongeza kuwa kuna wakati yeye mwenyewe aligeuka kuwa sehemu ya utalii kutokana na watalii wenyewe kumgeukia na kuanza kumuhoji kuhusiana na uwezo wake huo wa kazi na vile ambavyo anaimudu vema akiwa mwanamke huku wengine wengi wakiwa ni wanaume. Anasema kuna wakati gari lilikuwa linapata pancha wakiwa porini na hivyo kumlazimu kuanza kubadilisha tairi na kisha kuendelea na kazi yaka kama kawaida.

Mishi anasema si pancha peke yake kwani wakati mwingine gari uharibika vitu mbalimbali na kutokana na kuwa na maarifa ya ufundi hulazimika kushuka chini, kutengeneza na kuendelea na safari za kitalii.

Kuhusu mambo anayoyapenda; Mishi anasema anapenda kuangalia filamu hasa za kimarekani na kuna wakati watalii wengine wanakuja kama watu wa kawaida kumbe ni waigizaji wa filamu.

“Kuna siku nilienda kuwachukua wageni kwenye eneo la hoteli na kuwapakia kama kawaida yangu nikijua ni watalii kama walivyo watalii wengine, lakini mara nilipowasha gari na nilipogeuka nyuma ili kuwasalimia niligundua ni waigizaji wakubwa wa Hollywood nchini Marekani. “Ingawa nilishituka lakini sikutaka kuwaonesha kuwa nimewatambua kwa vile nafanya kazi kwa kuzingatia taaluma,” alisema.

Anaweka wazi kuwa watalii wa ina hiyo wapo wengi huku wengine wakiwa wanatumia majina feki kwenye kufanya booking za hoteli na wakiwa huko mbugani huonekana kuyafurajia zaidi maisha yao ya utalii. Mambo ayapendayo Mishi anaweka wazi kuwa akiwa mbugani hupendelea zaidi kuwaona simba wanavyofukuza wanyama wengine na kisha kuwapata na kuwaua.

Anasema kwa kawaida si kitu kizuri kufurahia tukio kama hilo ila kutokana na ukweli kuwa hutokea mara chache basi imekuwa ni kama kitu ambacho wadau wengi wa utalii wanapenda kuwaona.

Anasema, anapendelea pia kucheza michezo kama vile mpira wa mikono, kupika, kusoma vitabu na mambo mengine ya kujiendeleza kimaisha. Pia anasema hupendelea kuzungumza na wasichana hasa wa shule za msingi na sekondari ambapo huwasihi kujiendeleza kimaisha na kuzingatia masomo.

Anasema kwa vile hivi sasa anachukuliwa kama mfano kwa watu wa eneo hilo analofanyia kazi, basi akipata muda huzungumza na wasichana wakubwa na kuwaelewesha mambo mbalimbali ya kimaisha.

“Huwa nina waasa kutochagua kazi ya kufanya na wawe wabunifu na wenye nidhamu zaidi katika kazi zao huku wakijenga tabia ya kujichunga na kujilinda zaidi kimaisha,”anasema.