Mitumba, maua na mito vilivyomnyanyua Evely

KADRI siku zinavyozidi kwenda mbele wanawake hapa nchini na wengine duniani kote wamekuwa wakijihusisha katika masuala kadhaa yahusuyo ujasiriamali na maendeleo kwa ujumla.

Wakati wengi wakiwa wanajihusisha na biashara za kawaida kama vile kuuza vyakula na biashara ndogo, wapo wengine ambao wamekuwa wakifanya biashara kubwa. Hata hivyo, wanawake wanaofanya biashara hizo kubwa, wengi walianzia kwenye biashara za kawaida, lakini wakapanda siku hadi siku hadi kufikia hatua ya kufanya biashara kubwa.

Evelyne Rukanda ni mmoja kati ya wanawake ambao walianza kwa kujihusisha na biashara ndogondogo lakini sasa biashara yake inazidi kukua kwa kasi. Mafanikio hayo sasa yamemfanya mjasiriamali huyo kufikia hatua ya kumiliki duka kubwa la samani huku akiwa ameajiri vijana 11 wanaoafanya kazi mbalimbali, hatua iliyoweza kubadili kabisa mtazamo wake kimaisha akianzia katika ujasiriamali mdogo wa nguo za mitumba.

Evelyne ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akiwa amesoma na kutunukiwa Shahada ya Masoko na Biashara. Alianzisha biashara ndogo baada tu ya kumaliza elimu yake hiyo ya Chuo Kikuu mwaka 2012.

Tofauti na wengi wanavyofikiria kuwa mhitimu wa elimu ya Chuo Kikuu ni lazima aweze kufanya kazi za ofisini, kwa dada huyo si hivyo kwani yeye mara tu baada ya kuhitimu bila kupoteza muda alianza kuuza nguo za mitumba na kushona mito na kuuza mitaani.

Yeye mwenyewe anasema alipohitimu na kurejea nyumbani alianza kuuza nguo alizokuwa anazinunua kwa rejareka Mtaa wa Kongo jijini Dar es Salaam na baadaye kuziuza kwa watu mbalimbali.

Anasema aliendelea kuuza nguo hizo hadi pale alipopata mtaji wa kubadilisha biashara na kuamua kuingia kwenye shughuli ambazo aliona fika kuwa ndizo ambazo Mungu amemuandalia.

Anasema aliamua kuanza kutengeneza maua na mito na kisha kuuza kwa watu mbalimbali wakiwamo majirani na watu wake wa karibu kabla ya kuanza kuwauzia wateja wengine baadaye.

“Biashara hii niliona inanifaa kwani tangu nikiwa mdogo na kuwa binti wa makamo nilikuwa napendelea zaidi mambo ya upambaji na hasa kuona nyumba na sehemu wanazokaa watu zimepangwa vizuri.”

Kuhusu bei, Evelyne anasema alikuwa akitengeneza mito mikubwa na midogo na kisha kuiuza kwa Sh 15,000 hadi Sh 25,000 na kwamba mbinu aliyoitumia ilikuwa ni kuiweka katika mitandao ya jamii mito aliyoitengeneza kwa mara ya kwanza na alifanikiwa kwani alianza kupigiwa simu na wateja tangu siku ya kwanza ya biashara hiyo.

Kuhusu usambazaji, mjasiriamali Evelyne anasema alipokuwa anapata wateja alikuwa anawakimbizia mito kwa kutumia usafiri wa bodaboda na hivyo alikuwa anawafikia kwa wakati kabla hawajabadili mawazo kuhusu matumizi ya fedha zao. kupanuka kibiashara kwani wengi waligeuka kuwa mabalozi wangu.”

Evelyne ambaye ameolewa akiwa na mtoto mmoja anasema hamu yake ya kujiongeza katika ujasiriamali haikuishia hapo kwani baada ya siku nyingi kupita aliibua tena fursa, na ndipo alipoitupia macho biashara ya kutengeneza samani akifungua kampuni yake ya Evelyne Furniture.

Anasema kampuni hiyo ilileta kivitendo dhana ya kutoa huduma ya kupamba nyumba na hasa kwa kutumia utaalamu wa ubunifu wa upambaji wa ndani maarufu kama Interior Design.

Anasema aliipenda kazi hiyo kwa vile ilikuwa inakwenda sambamba na kazi za awali za kutengeneza mito na maua na wengine walikuwa wanahitaji kupewa ushauri wa mpangilio wa nyumba.

Anasema ilifika wakati ambapo aliamua kutengeneza kabisa sofa kwa ajili ya kuwauzia wateja wake ambao waliipenda sana huduma hiyo. “Nilipoona nazidi kupata kazi nyingi nikaamua kuondoka nyumbani kwa wazazi kule Ubungo na kwa hiyo nikaamua kufungua ofisi Namanga hapo nilikuwa nauza mito na maua na kutoa ushauri wa upambaji wa nyumba kabla ya kuanza kutengeneza masofa,” anasema.

Evelyne anafafanua kuwa kwa kuwa yeye ni mtu anayependa kuona fursa na kuzikimbilia, hatua hiyo imemsababisha kuwa mtu wa kufikiria kesho kila kukicha na hivyo anapoanzisha kitu anakuwa akiyaona mafanikio ya kesho si leo.

Anasema biashara ya kutengeneza masofa nayo ilipokelewa vizuri na wateja ambao walianza kutoa oda kwa wingi na hivyo ilimlazimu kuajiri vijana ili kuwezesha kazi kufanyika kwa kasi na ufanisi.

“Katika hili nilibaini kuwa Mungu alikuwa akinielekeza kwenye nchi yangu ya ahadi, kwani nilijaribu kutathimini nilipoanzia kwa kuuza nguo, kuuza mito, kuuza maua na sasa kutengeneza na kuuza samani. Kwangu haya ni mafanikio makubwa.”

Mapema mwaka huu aliamua kuhamisha biashara zake eneo la Namanga na kuhamia katika eneo kubwa lililopo karibu na Mikocheni Macho ambapo kwa sasa ameweka bidhaa zake anazotengeneza zote kwa pamoja kuanzia, mito, maua na fenicha ili kumvutia mteja kuona kazi zake kwanza.

Ni mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya Baba Niyoshima Rukanda na Mama Theresia Rukanda wazaliwa wa Ngara mkoani Kagera. Ndugu zake wengine wa tumbo moja ni Grace, Steven, yeye (Evelyne), Joyce na kisha Benard.

Anawashauri wanawake kutochagua kazi na hasa wahitimu wa elimu ya ngazi yoyote kuanzia ya sekondari, vyuo na hata vyuo vikuu huku akiwataka kujenga zaidi hali ya kujiamini katika kujiajiri.

Anasema biashara inaweza kuanza kidogo na kisha ikaja kuwa kubwa kwa kuwa kwenye biashara kunakuwa na faida ambapo inaweza kutumiwa vema na kumletea mhusika mafanikio.

Anasema kwa upande wake hakutaka kuajiriwa kabisa kwa kuwa alikuwa akiamini kuwa kwenye kujiajiri kuna mafanikio makubwa zaidi ikilinganishwa na kuajiriwa. “Unajua kwenye kujiajiri unakuwa unatumia nguvu zako kwa ajili ya kunufaisha biashara zako ikilinganishwa na kuajiriwa unakuwa unatumia nguvu zako kuendeleza vitu vya wengine sasa kwa nini vijana tusijipiganie siye kwanza,” anasema.

Evelyne ni mtaalamu pia wa kutumia gitaa huku pia akiwa ni fundi wa kuimba nyimbo za aina mbalimbali. Hupendelea masuala ya mitindo hasa mavazi na mengineyo. Ni mke wa Mkandarasi Victor Makula, wakiwa wamebarikiwa mtoto mmoja wa kike, huku akijinasibu kuwa hana shida katika kutenga muda wake wa kazi na kuihudumia familia yake.

“Kama ikiwa ni muda wa kuwa na familia ni muda wa familia ninapika na kuwahudumia mume na mtoto wangu. “Nikifika tu nyumbani huwa masuala ya kazi ninayaweka pembeni kabisa, nakuwa mtu wa familia yangu tu. Mume wangu anatambua kazi yangu na ananiunga mkono kwa hali na mali,” anasema.