ELLY DAVID: Mhamasishaji mdogo mwenye ushawishi

NI vijana wachache hapa nchini wenye moyo wa uthubutu wa kiwango cha mhamasishaji Elly David, kijana ambaye pamoja na kutokuwa na nguzo imara ya kusimamia hasa kutokana na uwezo wa kifedha wa familia yake pamoja na umri wake mdogo lakini hakukata tamaa.

Wazo lililoko kichwani mwa kijana huyu ni kwamba vijana wengi hapa nchini wamesongwa na fikra finyu na kutojithamini mambo ambayo yanawarudisha nyuma kushindwa kufikia ndoto zao.

Hii ni mara ya kwanza kwangu kuhudhuria katika mikutano ya uhamasishaji baada ya kujisemea mwenyewe nikaone ni jambo gani huwa linatendeka. Katika mkutano wa wanawake katika kujikwamua uliofanyika Sinza jijini Dar es Salaam anapanda jukwaani kijana mdogo ambaye alikua mgeni mualikwa.

Kijana huyu sio mwingine, ni Elly David, lakini najiuliza kwa muonekano wa kijana huyu ni mdogo atatueleza nini watu tuliokusanyika hapa ambao wengi tumemzidi sana umri. Sikujutia kushiriki mkutano huu kutokana na mada ambazo aliziwasilisha Elly, madini yaliyopo kichwani kwake ni tofauti na mwili wake na pia umri wake jambo ambalo limenifanya nimtafute ili niweze kuzungumza naye kujua alifikaje alipo sasa.

Elly ananieleza kuwa siri ya alipo sasa ni kwamba anapenda sana kazi anayoifanya na hasa anapenda kuona vijana wanafanikiwa na kuondokana na mawazo mgando. Kijana Elly Katalama ambaye anafahamika kama Elly David alizaliwa mwaka 1987.

Jina hilo la David alipewa na babu yake baada ya kuona ujasiri wake toka akiwa mdogo. “Babu yangu alipenda kusema ni jasiri sana ni kama yule Daudi wa kwenye biblia, kuanzia hapo jina likakua na nikazoeleka sasa kama David, nilipojitambua nikajiita Elly David,” anasema.

Elly ni mzaliwa wa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam akiwa ni mtoto wa pili katika familia ya watoto wanne wa Ester Katalama na Andrew Mkasa. Hata hivyo anasema kuchukua jina la upande wa mama yaani Katala ni kwa sababu aliishi zaidi na mama yake.

Anasema alisoma Shule ya Msingi Kinondoni darasa la kwanza hadi la nne kabla hajahamishiwa nchini Uganda mwaka 1994 ambako alirudishwa darasa la pili kwa sababu ya lugha na kujiunga na shule ya msingi Seeta.

“Baba yangu mimi alikua anasema unatakiwa kuwa mwanaume, hapendi madeko nadhani ndio sababu ya kunipeleka shule ya mbali na huko nilisoma shule ya bweni,” anasema.

Elly anasema ilimchukua miaka miwili bila kuiona familia yake hivyo alipewa mtu wa kumuangalia ambaye alikua akiishi huko Uganda aliyekuwa akitumiwa fedha za matumizi akifunga shule anakwenda kukaa kwake.

Anasema sababu nyingine iliyofanya apelekwe Uganda ni utundu. “Niliendelea kua mtundu mpaka huko Uganda, nakumbuka siku moja nikiwa kwa yule mlezi tulipofunga shule nilichoma moto uzio wa miti wa nyumba ya mtu na ilikua makusudi tu niangalie kama utawaka,” anasimulia Elly.

Kutokana na tukio hilo ambalo lilihatarisha nyumba ambayo kidogo iungue, mwenyeji wake alikasirika sana akawaambia wazazi wake watafute sehemu nyingine ya mtoto wao kufikia anapofunga shule wakati huo akiwa darasa la nne, hivyo ilibidi itafutwe familia nyingine ambako atakua anaenda kuishi kipindi cha likizo.

Akiwa darasa la tano alihamishiwa shule nyingine inayoitwa Mukono na baadaye kujiunga na Shule ya Sekondari ya Kikristo ya Seroma wakiamini kuwa atabadilika na kuacha utundu lakini baadaye alihamishiwa Shule ya Lake Side ambako alimaliza kidato cha nne.

Mama yake Elly kwa sasa ni mshauri katika masuala ya mahusiano akifanya makongamano mbalimbali ya wanawake hapa nchini na baba mchungaji. Baada ya kumaliza kidato cha nne alipelekwa shule ya sekondari Mulusa Luweero-wobulenzi iliyoko nje ya jiji la Kampala akisoma masomo ya sanaa (arts).

“Baada ya kumaliza kidato cha sita sasa nilirudi nyumbani ili niweze kumsaidia mama, nilikua napenda sana kujiingiza kwenye vikundi vya vijana hasa mambo ya ukimwi na vilabu vya vijana,” anasema Elly. Anasema alipokua sekondari alianza uhamasishaji vijana na huko ndiko alikopata hamu ya kazi anayofanya sasa.

“Nilikua napenda sana mijadala, nakumbuka kidato cha sita shule nilisoma bure kabisa baada ya kwenda kuiwakilisha shule kwenye shule nyingine, niliwakilisha vizuri na shule yetu ilishinda, nikipewa mada nakuja na mjadala mzuri sana mpaka walimu wanapenda,” anasema.

Elly anasema kipindi hicho mama yake ambaye alikua akimsomesha alikua katika kipindi kigumu hivyo ulipaji ada haukua mzuri. Anaongeza kuwa alikua mdogo na pia hakua na ujuzi wowote zaidi ya lugha ya kiingereza ambayo alikua akiimudu vizuri pamoja na elimu ya kidato cha sita hakua na ujuzi mwingine.

Alitafuta kazi kwa miezi kadhaa bila kupata, mama yake alimuuliza ndoto yake ni kufanya kazi gani ambapo alimjibu kuwa ni kuona vijana wanakua bora na anaongeza kuwa kwa kuwa hakua na fedha ya kwenda chuo, alianza kujisomea vitabu mbalimbali vya maendeleo, malengo na kujitambua.

Elly anaendelea kusimulia kuwa mama yake alimshauri kwanini asitumie ‘passion’ yake kuwanufaisha watu wengine jambo ambalo na yeye aliona ni zuri hivyo alianza kulifanyia kazi.

“Kwanza ilikua ni ngumu sana kwangu, nikaanza kuita vijana ambao ni marafiki zangu tunakaa chini ya miti au nyumbani tunakaa na kuzungumza , mama akaogopa sasa akasema sasa nitamletea wezi nyumbani,” anasema.

Anasema mwaka 2009 mama yake wakati mwingine alikua akimsaidia kukodi ukumbi ambapo Elly alialika vijana bila kiingilio chochote na kuanza kuzungumza nao na wakirudi majumbani mwao wanawaeleza wazazi wao mambo mazuri ambao anazungumza nao.

“Wazazi wakaanza kunipenda kwa ababu nilikua nikizungumza na vijana wao namna ya kujilinda na ugonjwa hatari wa Ukimwi, kujituma kwa kufanya kazi yoyote... siku moja kijana mmoja akaniuliza Elly wewe unajituma lakini huna kitu nini tutaiga kutoka kwako? hii iliniumiza sana kichwa,” anasema Elly.

Anasema kauli hiyo ilimfanya afikirie zaidi, alianza kuchapisha misemo yake mbalimbali kama vile ‘bila juhudi ndoto zitabaki usingizini’, ‘maisha ni mipango’ anavikata kata na kuviuza mwenge.

“Siku moja mama alinipa Sh 5000 nikachapisha vikaratasi na kuanza kuviuza kwa Sh 200, kuuza ilikua ni ngumu sana pia kwa sababu watu walikua hawaelewi nafanya nini, siku moja mama mmoja akaniuliza unakosa nini?

Lakini kuna watu walikua wananunua kwa kunionea huruma tu,” anasema. Alihama mwenge na kwenda Ubungo barabarani karibu na mataa ya kuongozea magari ambapo aliendelea kuuza vikaratasi vyake vyenye misemo mbalimbali vya kuhamasisha katika maisha.

“Lakini mama alikua hana amani ananiambia pale kuna vijana mbalimbali pamoja na vibaka naweza kupata tatizo lolote,” anasema. Elly anasema aliamua kufanya kazi hiyo kwa sababu nia yake ilikua kuwasaidia vijana kujikomboa katika maisha na kwa kuwa hakua na uwezo wa kufanya jambo lolote hivyo aliamua kutumia njia hiyo, “sikua na mtaji wa biashara na sikua na wazo lolote la biashara mimi nia yangu ni kusaidia vijana.”

Anasema kilochomtoa Ubungo ni siku moja baada ya kupigwa sana akidhaniwa kuwa ni mwizi baada ya mama mmoja kuibiwa pochi yake na kijana asiyefahamika. “Kidogo niuawe, baada ya kibaka kuiba na kukimbia, shati lake wanadai lilifanana na langu, nilipigwa sana mpaka baba mmoja alikuja kuniokoa akasema huyu kijana huwa namuona hapa kila siku anauza vikaratasi vyake, kunikagua wakanikuta na makaratasi yake na Sh 2000,” anasema Elly.

Anasema baada ya kuokolewa mwanaume mmoja alimshauri kuwa nia yake ni nzuri lakini eneo analofanyia kazi sio sahihi, akampa Sh 20,000 na toka siku hiyo aliamua kurudi Mwenge.

Elly anasema siku moja ilisimama gari na akumuona mzungu ameshuka kwenye gari na kumfuata na kuanza kumuhoji kama anauza karatasi hizo na pia kama ameviandika yeye, vikaratasi hivyo vilikua vya kwenye lugha ya kiswahili na vingine kingereza.

“Huyu ndiye aliyebadili maisha yangu, najua naweza nisipate nafasi ya kumuona tena, aliniambia kitu unachokifanya sijawahi kuona mtu wa umri wako anakifanya... alinishangaa sana,” anasema.

Kijana huyo anasema yule mzungu alivutiwa na kitu ambacho alikua akikifanya hivyo alimualika kwenda kuzungumza na vijana Arusha katika mkutano ulioandaliwa na taasisi anayoiongoza ambako walimpenda pia na kurudisha sifa kwa yule mzungu.

“Hiyo ilikua ni mwaka 2010, nilizungumza na vijana karibu 400 ambao walikua wameathirika na virusi vya Ukimwi hivyo ilibidi nitafute maneno ya kuwafariji,” anasema Elly. Anasema baada ya mkutano huo alikutana na watu mbalimbali na pia makampuni ya kimataifa ambayo yalipenda kazi zake na anaongeza kuwa aliporudi yule mzungu aliamua kumsaidia, hivyo alimuuliza kama yuko tayari kwenda Marekani kujifunza zaidi au ampe fedha ambazo ni Sh milioni tano.

“Yule mzungu aliniuliza, nikupe Sh milioni tano ambazo nitampa mzazi wako au nikupe ‘exposure’ ambapo utaenda Marekani kusoma, nikachagua kusoma,” anasema Elly. Anasema mwaka 2011 alimpeleka Marekani kwa miezi mitatu, huko alikuwa akizungumza na vijana wa makundi tofauti tofauti na sehemu tofauti kuwahamasisha mambo mbalimbali ya maisha.

“Kila mtu anahitaji kujitambua, kujiheshimu na kujishughulisha, hivyo ni vitu ambavyo nilikuwa nikizungumza na vijana hao nchini Marekani na walinipenda sana, nilikua na mada zangu kama nne ambazo hata ukiniamsha usiku naweza kuzizungumzia,” anasema.

Elly anasema huko Marekani alifikia kwa jamaa za yule mzungu na baada ya muda huo alirudi nchini hata hivyo baada ya miezi miwili alialikwa tena Marekani kwa ajili ya kazi hiyo hiyo. “Mara nyingi katika mikutano hiyo nilikua silipwi zaidi ya kunilipia gharama za msingi kama vile safari, malazi na chakula, lakini wakati mwingine walikua wakinipa fedha kidogo walikua kama wananisaidia,”anasema.

Anasema katika safari hizo alikuwa akikutana na watu mbalimbali na pia kujenga urafiki na watu wengi hasa watu wazima. “Watu wazima wengi walikua wakinialika pia kuzungumza na watoto wao, na watoto walikua wakinisikiliza sana wazazi wanafurahi,” anasema.

Elly anasema katika safari hiyo ya pili alikutana katika jukwaa moja na mzungumzaji kutoka Singapore ambaye alimualika nchini kwao kwenye mkutano wake mwaka 2012 ambapo alikwenda na kufanikiwa kufanya kazi hiyo. Anasema baada ya hapo alianza kualikwa katika mikutano nan chi mbalimbali kuzungumza, mwaka 2013 alifanikiwa kufungua ofisi yake kwa ajili ya kuwashauri watu.

“Nikawa nafurahi sana sasa kwamba sasa nina ofisi yangu, nakaa tu kwenye ofisi yangu... ile tu mtu akiniuliza uko wapi namwambia niko ofisini ilikua ikinifurahisha sana,” anasema. Anasema ofisi aliyokuwa akiitumia ilikuwa chumba kimoja, baadaye aliomba msaada kwa wale rafiki zake wazungu ambao walimsaidia akaweza kupata ofisi kubwa zaidi eneo la Mbezi Beach ambako anaendelea na kazi mpaka sasa.

Elly anasema mwanzoni alikuwa akitoa huduma bure kwani alitaka kwanza watu waelewe kitu anachokifanya na pia mikutano mingi aliifanya bila kulipwa. “Wakati mwingine nilikua nashindwa kwenda mikoani kwa sababu hawagharamii, kweli wananialika kwenye mikutano lakini wanaamini nina fedha, wachache walikuwa wananitumia nauli na mama yangu alikua akisisitiza walipe kabisa na nauli ya kurudi ili asipate shida huko anakoenda,” anasema.

Mwaka 2013 Elly anasema alianza kuandika makala kwenye moja ya magazeti ya kila siku, katika makala hizo ambazo nyingi ni za maisha alikuwa akipata simu nyingi za watu ambao walikua wanapenda makala zake.

“Kuna mtu mmoja nakumbuka alitoka mkoani akaja kunitafuta akaniambia yeye na mke wake makala zangu zimewasaidia sana, akanipa Sh 500,000, lakini baadaye gazeti lile lilisitisha kuchapisha makala zangu,” anasema.

Elly anasema mpaka sasa anaendelea kupokea mialiko kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya Afrika kwa ajili ya kwenda kwenye mikutano kuzungumza na watu mbalimbali kuwahamasisha ka- Nyota/ Mapishi tika maisha.

Anasema mwaka 2013 hadi 2015 alisoma masuala ya saikolojia katika Chuo kimoja nchini Marekani na anaongeza kuwa kwa sasa ana mpango wa kuanzisha kipindi kwenye televisheni. Elly anasema anafurahia sasa kwani ni tofauti na maisha aliyokua akiishi awali ambapo alikuwa hajui atafikia vipi ndoto yake.

Aidha, Elly anasema pamoja na kwamba yeye ni kijana mwenye umri mdogo kuliko wahamasishaji wengine lakini anaamini anakitu cha ziada ambacho ni cha tofauti na wenzake wanaofanya kazi hiyo.

“Nimepata bahati ya kuzungumza na watu mbalimbali, mataifa tofauti, wenye elimu zaidi yangu... kuweza kuwaweka chini wakanisikiliza mimi pamoja na umri wangu kuwa mdogo kwangu ni fahari kubwa na ni hatua ya kujipongeza,” anasema Elly.

Aidha, anasema alipofika katika kuelekea katika ndoto zake panampa hamu zaidi ya kufanya jitihada ili aweze kuiwakilisha nchi yake vizuri pamoja na Bara la Afrika kwa ujumla. “Mimi napenda sana kusoma, nikisafiri wakati wa kurudi, sanduku moja najaza vitabu, nanunua vitabu mbalimbali, ofisini ni vitabu, chumbani kwangu ni vitabu, kwenye gari najaza vitabu... kila muda ninaoupata ni kusoma vitabu,” anasema.

Elly anasema pia ndoto yake ya kusaidia vijana bado anayo, “najisikia vibaya sana kuona vijana wamekaa tu hakuna wanachofanya, vijana wengi wako hai lakini hawana matumaini... matumaini yanaletwa na ndoto zao wenyewe.”

Anasema uitikio pia wa watu, “waafrika wengi hatupendi sana elimu, itisha sherehe yoyote ya vinywaji, chakula muziki weka na kiingilio watakuja wengi, lakini itisha watu bila kiingilio kwa ajili ya kutoa elimu watu hawaji.”

Anasema katika vitu ambavyo hawezi kuzungumzia ni ndoa, na hiyo ni kutokana na umri wake na pia hana uzoefu katika jambo hilo. “Kuna watu wenye ndoa wanakuja ofisini kwangu niwasaidie, nawaambia jamani jambo hilo siwezi, lakini wananiambia kama naweza kusaidia kwenye uhusiano kwa nini nishindwe kwa wanandoa, lakini huko nimekataa kabisa,” anasema.

Elly anasema katika ratiba yale ya siku anaamka saa tisa au saa 10 alfajiri kila siku kwa ajili ya kusoma akiamini akili inakua imetulia, na hiyo ni baada ya kusali kwani amekulia katika familia inayosali sana ikizingatiwa ni mtoto wa mchungaji. Kijana Elly anasema anapenda kusafiri kujifunza mambo mbalimbali na pia anapenda kutoka na kwenda sehemu tulivu ambako atakaa na kutafakari kwa utulivu.