Mwanamke shupavu aliyekataa kifo

HUJAFA hujaumbika, ndio msemo wa wahenga ukiwa na maana pana sana. Ukiwa mzima unatembea na kufanya shughuli zako wapaswa kumshukuru Mungu kila sekunde unayotumia pumzi yake bure.

Grace Rweyemamu ndilo jina lake, katika mahojiano yake na HabariLeo anaeleza safari yake ya maisha tangu akiwa chuo kikuu hadi alipopata ugonjwa wa ajabu wa uvimbe mkubwa ndani ya kichwa.

“Baba yangu ni mwanajeshi, kutokana na kuhamishwa huku na kule nikajikuta nasoma shule nyingi tofauti za msingi, lakini shule ya mwisho nilimalizia Ubungo Kisiwani, nikachaguliwa kusoma sekondari ya Zanaki ambayo nilisoma kidato cha kwanza hadi cha nne.

“Kidato cha tano na sita nilisoma Makongo na Chuo Kikuu nilisoma UDSM. Nilisomea Biotechnology lakini baada ya kumaliza chuo mwaka 1999 nilichelewa sana kupata kazi,” anaanza kwa kusema Grace.

“Ilibidi nianze kufanya kazi za kujitolea kwenye mashirika ya kimataifa kama Shirika la Kimataifa la Kazi (ILO), na baadaye nikaamua kujiendeleza, kwa kusoma Shahada ya Pili ya Afya ya Umma, lengo langu lilikuwa ni kufanya kazi kwenye mashirika ya kimataifa.

“Mume wangu nilimfahamu akiwa chuo, tulikuwa tunasali ‘fellowship’ pamoja lakini hatukuwa na mahusiano yoyote ya kimapenzi. Baada ya kumaliza chuo tulikaa kama miaka miwili ndipo tukajikuta tunaingia kwenye mahusiano.

“Tulimaliza chuo mwaka 1999, mwaka 2012 ndipo tukaanza mahusiano ya kimapenzi na mwaka 2013 mwezi wa nane tukafunga ndoa,” anasema.

Matatizo ya kuumwa “Baada ya kuolewa, mwaka wa kwanza wa ndoa hata kabla hatujasherehekea ‘anniversary’ yetu, nikaanza kuumwa sana, nikaenda hospitali wakanipima wakasema ni homa ya tumbo (typhoid), lakini nilipokuwa nachomwa sindano mwili ulikuwa unaishiwa nguvu, nachoka sana yaani nilikuwa naona kifo. Nilipona lakini ilichukua muda sana kukaa sawa.

“Dawa zilikuwa zinanichosha nikasema labda kwa vile sikupenda kula nikahisi labda ni sababu, lakini nilipokuja kuugua mara ya pili kila hospitali niliyokwenda waliniambia typhoid na malaria, wengine waliniambia ‘infection’ sikujua kama ni uvimbe wa ubongo...pamoja na kumaliza dozi nikaenda hospitali nyingine waliniambia kiwango changu cha typhoid ni kidogo na hata wakati ule nilitumia dawa na sindano za typhoid wakati sio kilichokuwa kinaniuma,” anasema.

Anasema alikuwa ni mtu wa hospitali, kuna wakati anakuwa sawa. Mwaka wa tatu wa ndoa yake, akiwa ameshaanza masomo ya Shahada ya Pili, akiwa mwaka wa pili, usiku ghafla alianza kutapika, alitapika sana, mume wake akamwambia waende hospitali, akamwambia yuko sawa.

“Lakini kila baada ya muda natapika, ikabidi nipelekwe hospitali usiku huo, kupimwa nikaambiwa ni ‘infection’, kulipokucha mama akaja akashauri twende hospitali nyingine. Nikaambiwa nina malaria, nikaanza dozi ya sindano ya siku tano ya malaria na powersef. Baada ya kumaliza dozi nikapata nguvu kidogo nikaenda chuo... nakumbuka tulikuwa kwenye majadiliano na wenzangu wakaniambia Grace haupo sawa rudi nyumbani ukapumzike, nikarudi nyumbani. Siku hiyo hiyo usiku nikazidiwa hapa zimeshapita wiki tatu tangu nimalize dozi ya malaria na typhoid,” anasema.

Anasema wao ni watu wa maombi, macho yalikuwa yanaona nusu, akawa anahisi akili inataka kuchanganyikiwa, mtu anazungumza namsikia tofauti na yanayoongelewa, sauti ikawa kama inaingiza maneno kama yanapeana wigo.

“Nina kaka yangu ni mchungaji aliniombea kwenye simu, nilitapika sana, na kabla ya kutapika nilikuwa napata maumivu makali sana ya kichwa, niliombewa sana kisha nikapelekwa hospitali nikiwa nimebebwa. Gari ikijitikisa kidogo naumwa sana, ni Mungu tu tukaenda Hospitali ya Sali zamani ilikuwa ikiitwa AMI, nikapimwa wakaniambia ninaonesha nina upungufu na baadhi ya homoni ambazo zinatokana na aidha goita au uvimbe kwenye ubongo, moja kwa moja nikasema ni uvimbe kwenye ubongo wala sikulinganisha na kitu’’, anasema.

Anaongeza kuwa, alishauriwa kufanya kipimo cha MRI, wakaenda kukifanya siku ya Jumamosi, Jumapili alizidiwa sana wakati huo anaishi Kijitonyama. Wanafamilia walikusanyika kwa ajili ya maombi na kuwa alikuwa na majibu, ingawa hakuwa amesomea, na maombi yalikuwa kama ni uvimbe kwenye ubongo basi Mungu auyeyushe.

“Jumatatu tukaenda kusomewa majibu na daktari akatutazama usoni akatuonesha mimi na mume wangu, kuwa mnaona hapa huu ni uvimbe kwenye ubongo tena mkubwa sana umeshikana na ubongo na umekaa sehemu ya maji unazuia maji yasipite ndio maana natapika, inabidi utolewe. Nikamuuliza hakuna dawa, akasema hakuna, lazima utolewe. Nikamuomba aniandikie rufaa niende India, alikataa kwa madai kuwa hata hapa nchini wana uwezo wa kufanya upasuaji wa aina hiyo na yeye ndiye angeufanya, na pia kutokana na tatizo langu sikutakiwa kusafiri kwani nisingeweza kuhimili presha ya ndege na ningefia angani,” anasema.

Kwa mujibu wa Grace, walipokea maelezo hayo yeye na mume wake, mioyo yao ilishuka sana, walikosa amani, tumaini. Ni kweli alikuwa anaumwa lakini hakutegemea kuwa na tatizo kubwa kama hilo, ukizingatia kwa wakati ule hali yake haikuwa mbaya kiasi hicho.

“Na daktari alisisitiza ni lazima nifanye huo upasuaji haraka, kwani muda wowote naweza kuzimia na nikafa, na akasema muda wowote nikijisikia vibaya nipelekwe ‘emergency’ ila mioyo yetu haikuwa na amani kabisa kufanya upasuaji ule mkubwa hapa nchini. Mungu hamtupi mja wake, bahati nzuri, tukampata profesa mmoja wa ‘Neurosurgeon’, akatushauri akasema, kwa Tanzania tuna wataalamu lakini vifaa vyetu bado kidogo na akatushauri kama tunaweza kwenda nje ni vema, akatuandikia rufaa. Ikasaidia, bima ikaweza kulipa, bima ya mume wangu na yangu yote ya mwaka mzima na haikutosha ikabidi tujichange tena ndugu, jamaa na marafiki ikapatikana Sh milioni 10, ndipo nikaenda kwenye matibabu,” anasema.

“Sasa kwenye MRI ulionekana uvimbe mkubwa sehemu mbili na mwingine mdogo ambao ulikuwa unahusika na macho, kuna mama mmoja ni daktari wa wanawake, akasema wanangu Mungu amewafanyia njia, nendeni India na atakuponya, na ndio alinipa dawa ambayo ilinisaidia maumivu ya kichwa nikiwa kwenye ndege,” anaongeza.

Nilivyofika India nilifanyiwa vipimo na daktari alitukalisha akasema mimi ni kama kalamu, kalamu ikiandika vizuri usisifie kalamu, sifia aliyeandika, kama akiandika vibaya usilaumu kalamu, anapaswa alaumiwe mwandishi, nyuma yake kuna Mungu, akifanya upasuaji ukafanikiwa ni Mungu sio yeye na usipofanikiwa sio yeye wa kulaumiwa ni Mungu.

“Akasema ana uzoefu wa upasuaji wa watu 5,000 na hajawahi kufa mtu mikononi mwake, katika wagonjwa wake wote upasuaji ulienda salama, hilo lilitupa tumaini… lakini baadaye alikuja kumwambia mume wangu hajawahi kukutana na kesi kama yangu, ni kesi mpya, hatari ya kufa kikawaida ni asilimia moja hadi mbili, lakini kwangu ilikuwa ni asilimia mbili hadi nne...akasema kuna hatari ya kupooza, hatari ya kupoteza macho, na kuna hatari ya kupoteza kumbukumbu au vyote kwa pamoja baada ya upasuaji lakini ni lazima uvimbe utolewe,” anasema na anaongeza kuwa, daktari alisema uvimbe umeshikana na ubongo kama doa kwenye nguo kwa hiyo hawawezi kukata ubongo ili kutoa uvimbe lazima watoe nusu asilimia 30 au 50. Daktari alimtaka mume wangu asaini kukubaliana na chochote endapo kitatokea, na pia wakamchukua ‘video concert’ mara mbili wakihakikisha anakubaliana na maelezo yao na kukubali upasuaji huo kufanyika ‘at his own risk’.

“Unaweza kufikiri alikuwa katika hali gani baada ya kutoka kwa daktari, siku moja kabla ya upasuaji, huku akilazimika kutoniacha peke yangu hata dakika moja, na pia kutonionesha hali ya kunitia wasiwasi,” anasema.

Grace anasema alijaribu kumhoji maswali kadhaa daktari, ili kujiandaa kisaikolojia kwa kile anachoenda kukabili, ila aliyajibu kisiasa sana. “Naingia kwenye upasuaji saa sita mchana, nimenyoa kipara, nywele zangu nilizokaa nazo kwa miaka zaidi ya saba, sijui nini kitatokea nikiwa ‘theatre’, sijui upasuaji utachukua saa mangapi, sijui kama viungo vyangu vyote vitatoka salama, niliwahi kusikia kuna mtu alifanyiwa upasuaji wa kichwa akatoka kipofu.

“Nawawazia ndugu zangu, wazazi na mume wangu, na watu wanaonipenda watakuwa kwenye hali gani nikiwa chumba cha upasuaji . Sijui ni baada ya muda gani nitakuwa sawa tena. Nimekatiza masomo yangu ya Shahada ya Pili kwa sababu ya ugonjwa, na sijui nitaweza kuendelea nayo baada ya muda gani. Nayaona maisha yangu mikononi mwa wataalamu ambao hata wao wanakiri kuwa tatizo hilo ni kubwa mno kuwahi kukutana nalo katika uzoefu wao,” anasema.

Hata hivyo, nyumbani walipopata hiyo taarifa walibadilisha maombi, mama alizungumza na kaka yangu mchungaji, akasema Mungu ameruhusu huo upasuaji basi afanyiwe huo uvimbe utolewe wote.

“Kabla sijaondoka Tanzania, Mungu aliniambia nitaponywa na mikono ya madaktari, nilimuamini Mungu sana na nilimwambia bado ninahitaji viungo vyangu vyote sitatoka na ulemavu.

“Nilipangiwa tarehe ya upasuaji, nakumbuka niliingia theatre Julai 26, mwaka 2016, upasuaji uliongozwa na Dk Jagdish uliofanyika kwa saa 13. Nakumbuka usiku wa kumkia siku ya upasuaji nyumbani kwetu hakuna aliyelala, walikesha kwa maombi… madaktari wangu hatimaye baada ya saa 13 walitoka na kumjulisha mume wangu wamefikia uvimbe, na wamefanikiwa kutoa uvimbe wote, wakasema hawawezi kujua kama ni saratani au sio, mpaka waupime, nilikuwa na wasiwasi sana na saratani lakini Mungu alisaidia baada ya kupima, haikuwa saratani.

“Ule uvimbe mdogo walisema wangenifanyia upasuaji mwingine ambao ulikuwa ugharimu fedha nyingi ambazo hatukuwa nazo, hata hivyo baadaye walikuja kunipima mara tatu wakashangaa hawauoni tena, kwa hiyo huo ni muujiza ambao Mungu amenitendea,” anaongeza Grace.

Anasema alikuwa na matumaini makuu katika Kristo na ndipo alielewa lile andiko, "Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu. …nina hakika juu ya kile alichoniambia Mungu, Shalom –Nothing – shalom nothing less, nothing broken’ ninaamini hakuna kitakachopungua wala kitakachovunjika.

Grace anasema alielekea katika chumba cha upasuaji, huku akisogezwa na kitanda kinachotembea na ndani yake alisikia nafsini kwake sauti ikimuambia ,

“Grace, utapewa dawa ili ulale, usisikie maumivu yoyote.”

“Nakumbuka vizuri naambiwa kuvuta ile hewa iliyowekwa puani mwangu, na baada ya kuvuta mara ya pili, nikasinzia. Mimi ni mtu ambaye mara nyingi sana huota nikilala.Nikisinzia usingizi mzito, basi nitaota ndoto nyingi zisizo na maana, ambazo ninapoamka sizikumbuki. Baada ya kusinzia wakati wa upasuaji, nilikuwa nikiota ndoto kama nikiwa katika usingizi wa kawaida mzuri na mzito sana,” anasimulia.

Madaktari baada ya upasuaji walisema ningeamka baada ya saa 24 , lakini cha ajabu niliamka ndani ya saa sita na nilipoamka ilikuwa ni historia nyingine. Alikuwa amezungukwa ma mashine za kupumulia na mipira ya kujisaidia, mipira ya chakula, mipira puani yaani ugonjwa ulikuwa kama ndio unaanza upya.

“Mashine ndio ilikuwa tumaini langu, nakumbuka nilipozinduka namsikia daktari anamwambia mume wangu, mke wako yupo katika hali ya kujitambua na baada ya muda mfupi tutamtoa hiyo mashine ya kupumulia,” anasema.

Grace kwa imani anasema, alijua Bwana ameshafanya kile alichoahidi, yaani operesheni imeenda vizuri na kuwa Godfrey, mume wake alifika na kumpa pole nyingi mno na yeye alikuwa akinyoosha mkono juu na kujaribu kumuonesha kwa ishara kuwa ni Mungu. Hata hivyo anasema hakuwa tena Grace aliyelala katika chumba cha upasuaji akiwa mzima na mwenye nguvu, ambaye wangetembea watu wangeuliza ‘ni nani mgonjwa kati ya mimi na mume wangu.’

“Wakati huu upumuaji wangu ulitegemea mashine ya ‘Oksijeni’ kwa asilimia zote. Sikuweza tena kuzungumza kwani mpira ulipita puani na mdomoni. Kichwa changu kilikuwa kimefungwa kitu ambacho kilishikilia sehemu ya nyuma ambayo nilipasuliwa…sijui katika macho yangu kulikuwa na nini lakini nilihisi kama nimevalishwa kitu na sikuweza kuona kwa uzuri sana, na kuna wakati walinifuta kwa kitambaa chenye maji machoni na kuniuliza kama naona.

“Nilichotaka kujua ni kwamba naweza kufungua macho na kutazama nikaona, sikujali kuwa ni kwa kiasi gani naona, ila kujiona kuwa si kipofu, nilijua kuwa Bwana amelinda macho yangu, muda ulivyozidi kusogea, macho yangu yalipunguza sana kuona, nikawa nikiona kama mtu anayetaka kufumba macho kabisa, kiasi cha kunitia hofu kuwa huenda nikifumba macho sitaweza kufumbua tena, na kuna wakati jicho moja halikuweza kuona kabisa, nikawa nikitumia jicho moja, lakini nafsini, nilihakikishiwa kuwa siwezi kuwa kipofu,” anasema.

Grace anasema yeye ni wakili wa kukataa ‘vifo visivyotarajiwa’ na anaongeza kuwa ukitaka kufa kuna saini fulani ambazo unaweza kuziona na kuwa, siku zote aliwaeleza watu ukisikia hali ya kufa pambana, maana kifo huwa kinakuja na taarifa na mwanadamu ana nafasi ya kuchagua ndio maana kama ni Mkristo na unafuatilia dini, Mtume Paulo katika Biblia alisema, “ basi nitachagua kuishi maana kuishi ni Kristo, kufa ni faida na kusema kwa sababu yenu nyie nitachagua kuishi kwa maana nyingine kuna nafasi ya kuchagua, sema roho ya mauti inakuja na ushawishi mkubwa.”

“Ndio maana wenzetu wazungu wana tabia hata mtu akiwa ICU anamwambia apambane asikubali kufa...nakumbuka nikiwa ICU hali ilibadilika ikawa mbaya sana, nikawa natamani mtu aniambie Grace huwezi kufa, Grace utaishi kiukweli kuna wakati nilipigana sana huwezi kujua thamani ya pumzi kama hujaingia ICU, kila pumzi unayoivuta unashukuru na kila pumzi unayoitoa inaumiza,” anasema.

Mwanadada huyo anasema kuna taarifa ambayo aliisikia mbaya ikamuogopesha kuhusu macho yake, uso ulivimba sana madaktari wakawa wanashangaa, macho yalikuwa yanapoteza uwezo wa kuona na yakavimba sana.

“Kuna wakati ilifika siwezi kuzungumza nawasiliana kwa kuandika zaidi, lakini nilivyokua naandika havieleweki, ni kama watoto wadogo wanaojifunza kuandika makorokocho, mume wangu akajua naandika vile kwa vile nimepoteza uwezo wa kuona ila mi nilikuwa najiona naandika sawa. Sasa taarifa ya kupoteza macho ikanitisha na mbaya zaidi nilikuwa mtu akizungumza naelewa kwa hiyo kila walichokuwa wanazungumza kwa nini hali inakuwa mbaya inabadilika vitu kama hivyo vikawa vinanitia wasiwasi ilifika mahali nikamsikia kabisa daktari anasema, ‘This Patient is basically died’” anakumbuka .

Hata hivyo, Grace alikataa kauli ya madaktari nafsini na kumwambia Mungu kuwa alikuwa na mahusiano mazuri naye na kumhoji yale maono aliyokuwa akimuonesha kuwa atapona alikuwa anamdanganya?

“Nikamwambia Mungu kuna mambo mawil,i aidha wewe sio Mungu wa kweli niliyekuwa nakuabudu na kama ni Mungu wa kweli thibitisha hili sitakufa kwani nina ndoto zangu za maisha ambazo sijazitimiza…nikamwambia nisipokufa nitajua wewe ni Mungu wa kweli, na nikifa nitajua wewe sio Mungu wa kweli, nafsi yangu ikaniambia hutokufa Grace nafsi yako haitaonja mauti, na utakapoona hujafa utaniamini kwa kile kitu, nikapata nguvu na kuamini nitatoka salama na viungo vyangu vyote,” anasema.

Anasema alikaa ICU siku 15 na siku nane za mwanzoni alikuwa akipigania maisha lakini Mungu ni mwema alitoka salama.

“Ila shetani ni mjanja sana, nahisi ilikuwa ni mapepo kuna wakati sijalala lakini nilipata maruweruwe nilikuwa naona wauguzi walikuwa wananiwekea sumu, wananichoma sindano za sumu, wanaongea namna ya kuniua, kuna wakati TV ya ICU, filamu ni za kihindi za kawaida, lakini nikawa naona wanaoigiza ni wauguzi wananishawishi Grace kubali kufa, kufa ni kawaida hata mumeo Godfrey ameshakubali ufe tu, ni vitu vya ajabu siwezi kuelezea maruweruwe,” anasema .

Anasema alianza kuhisi kabisa pumzi ikinibana kila anapolishwa chochote, aliamini kuna sumu kawekewa na kuamua kuanzisha mgomo wa kutokula ilifikia wakati madaktari wakamwambia mume wake akiendelea kugoma kula itabidi wamtoboe tumboni maana atakufa kwa njaa.

“Katika sehemu nilizozichukua wakati wa ugonjwa ni ICU, hata kitabu nilichoandika Jipu Ndani ya Ubongo nimekiandika maalumu kwa wagonjwa wote waliopo ICU. Unajua unapokuwa pale wauguzi na watu wengine hawahisi ubinadamu wako, wanajua yule mtu aliyelala pale ni hopeless hajitambui, lakini kumbe unajitambua, unachokosa ni ule uhuru wa kupumua mwenyewe, natamani kuwaeleza kuwa mgonjwa anapokuwa kwenye hali ile mzungumze naye na kumueleza umuhimu wake mnavyomhitaji, muongee naye maneno ya kumtia moyo na kumfanya apambane,” anasema.

Grace anasema alitoka ICU akiwa haoni vizuri na alirudi na hali hiyo nchini na alikuwa akiona watu wawili wawili, kichwa kilimuuma sana na kilikuwa kimevimba kama mwenye mtindio wa ubongo na madaktari walisema hakuna uhakika wa kila kitu kutengemaa, ingawa baadhi ya viungo niliambiwa vitatengemaa taratibu.

“Kuna siku nililazimisha tutoke, nilitamani yale maisha ya zamani nimekaa kwenye gari ilibidi wanifunike na kanga usoni nilikuwa nahisi mwanga mwingi kwenye macho unaniumiza macho. Tulienda Mwenge na mama yangu mdogo, nakumbuka ilikuwa imeshapita miezi mitatu tangu nirudi India, nilipofika yani wale watu na zile kelele nilihisi kudata, unajua nilivyokaa ndani muda mrefu nilidhani nimepona kumbe ilikuwa bado, kuna mambo mengi mpaka nimekuja kukaa sana ni zaidi ya mwaka,” anasema.

Muujiza huu wa Grace ni mkubwa mno, yako mengi anatamani kueleza na ndio maana ameamua kuandika kitabu, kushuhudia ukuu wa Mungu na kuwatia moyo wengine wanaopitia katika changamoto nzito za maisha.

“Nashukuru Mungu amenisaidia nimerudi shule, nimefanya mtihani na nimefaulu vizuri, kuna mambo mengi ambayo bado natakiwa kuyashuhudia naandaa kitabu changu cha Jipu Ndani ya Ubungo kitaeleza kwa undani zaidi na nini ninachokifanya kwa sasa, ”anasema.