Tuzungumze Biashara: Vilio vingi vya wateja ni hatari kwa biashara yako

MFANYABIASHARA unapaswa uelewe kuwa, machozi ya wateja wako yanayotokana na hasara unayowaletea, kwa kutumia huduma yako au kwa kununua bidhaa yako isiyofaa ni mkosi na huyastahili.

Inaelezwa kuwa, kufanya kazi kwa jambo linalotajwa kuwa sababu mbaya ya mfanyabiashara au hata mtu wa kawaida kutofanikiwa kunategemea na imani ya mtu mwenyewe, lakini, kutokana na ukweli kuwa machozi ya uchungu wa kupoteza kitu au fedha kwa uzembe wa mwingine, huambatana na malalamiko yenye kujutia.

Mtandao wa www.answers.com unasema, ikishafikia hatua mteja anajuta na kusema sitarejea tena dukani pale, kwa mfanyabiashara inakuwa ni mwisho mbaya, unaoweza kutafsiriwa kuwa ni mkosi. Mtandao huo unaeleza kuwa maneno hayo ya mteja yanakuwa ni kama mkosi au neno la kutakia biashara husika mwisho mbaya.

Ni msemo unaolaani, kubomoa, badala ya kujenga. “Mteja anapaswa ashawishiwe kwa ubora wa huduma na bidhaa ili arudi tena kuifuata. Akiudhiwa na kusababishwa anyanyue mikono juu kuonesha kutotaka tena kwenda kufuata huduma au bidhaa mahali alipohudumiwa vibaya,inakuwa ni jambo linaloondoa neema kwenye biashara husika,” www.answers.com, inasema.

Cha msingi, inaelezwa kuwa, wafanyabiashara hawanabudi kukwepa kusababisha mazingira ya wateja kujuta kuzifahamu biashara zao na kuzinunua.

“Katika huduma ndio kabisa, wafanyabiashara wanapaswa kuhakikisha wateja wanapo zitumia wanatoka kwenye eneo la biashara wakitabasamu na kuahidi kurudi wakati mwingine wakiwa wameongozana na wenzao wapya,” www. answers.com inasema.

Katika safu hii, Jumatano ya wiki iliyopita nilizungumzia uaminifu katika biashara ya bidhaa na huduma, ambapo, nilieleza kisa cha wahudumu wa hoteli moja mkoani Mbeya walivyoonesha kukosa uaminifu, hivyo kuhatarisha biashara yao.

Baada ya kuandika nilichokiandika, nilipigiwa simu na kupata ujumbe wa maandishi kupitia barua pepe, inayosomeka chini ya safu hii, nikielezwa aina nyingine ya kukosa uaminifu, ambayo, wahudumu katika hoteli za kati na nyumba za kulala wageni mijini, wanaitumia ‘kuliza’ wateja.

Wasomaji wa safu hii, akiwemo Bonaventure Gasper wa Mbeya, Kamugisha (alitaja jina moja) kutoka Kigoma na Asnath Kileo wa Morogoro, wameeleza walivyo poteza mali katika nyumba hizo, walipofikia kupata malazi. Kila mmoja alikuwa safarini kivyake. Walituma ujumbe kwa siku na muda toauti kueleza yaliyowakuta.

Ni watu wasio na uhusiano, ukaribu na hawafahamiani. Wawili kati yao visa vyao vinafanana na mwingine kisa chake kina tofauti. Nikianza na Gasper, yeye anasema wakati akihamia Mbeya kikazi, alilazimika kukaa katika nyumba ya kulala wageni kwa wiki moja huku akifanya maandalizi ya kuhamia kwenye nyumba aliyopangiwa na ofisi yake, kwani ilipaswa kufanyiwa ukarabati.

Anasema, kwa maana hiyo, alikuwa akiishi kwenye nyumba hiyo ya wageni ambapo, asubuhi alilazimika kwenda ofisini na kurejea jioni kulala. Kwa maelezo yake, wakati akienda kazini alikuwa akiacha vifaa vyake, zikiwemo nguo na viatu katika chumba alichokilipia kwa wiki nzima.

Gasper anaeleza kuwa, kama kawaida, saa tatu hadi saa nne, mhudumu huingia chumbani hapo kufanya usafi, jambo ambalo hakuwahi kulipinga kwa sababu ni utaratibu wa nyumba za wageni na ni haki ya mteja kubadilishiwa shuka na vifaa vingine vinavyostahili kubadilishwa.

Anasema kuwa, kumbe ilikuwa ni mchezo kwa baadhi ya wahudumu katika nyumba hiyo ya wageni kukikodisha upya chumba kile kwa wateja wa chap chap (wa haraka haraka) wanaofika kupata vyumba kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kimapenzi zaidi.

“Kama miujiza ya Mungu, kwa kuwa ilizoeleka kwamba nikitoka saa 12 asubuhi narudi saa 2:30 au saa 3:00 usiku, siku moja nilirudi ghafla saa 7:23 kwa ajili ya kufuata karatasi yangu fulani, nikasumbuliwa sana kupewa ufunguo wa chumba na mhudumu niliyemkuta..,”Gasper anasema.

Anasimulia kuwa ilimchukua takriban dakika 45 kabla ya kushuhudia kwa macho yake mwanamke na mwanamume mmoja wakitoka chumbani hapo na kupacha wazi, huku mizigo yake ikiwa ndani bila uangalizi wowote, kuhakikisha kuwa ilikuwa salama.

Kwa maelezo yake, kazi siku hiyo ilivurugika kwa sababu alilazimika kuendelea kupoteza muda kukagua vitu vyake ambapo, aligundua kuwa marashi yake yaliibwa pamoja na kifurushi cha vitambaa vipya vya mkono (leso za rangi ya brown).

Anasema bahati nzuri ni kwamba hakuwahi kuacha fedha ndani ya chumba kile na hakuwa na nguo nyingi wala kitu kingine cha thamani zaidi ya marashi ambayo hadi anahama mahali hapo, hakujua kuwa aliyeiba ni mhudumu au wale wateja wa chap chap.

Kwa upande wake, Kamugisha anasema, uaminifu kwa baadhi ya wafanyabiashara wa hoteli na nyumba za kulala wageni ni sifuri kwa sababu wamekuwa wakitumia vyumba vilivyokwisha lipiwa kuhudumia watu wengine.

Huyo anasema yeye fedha zake ziliibwa na wateja wa chap chap waliyopewa chumba chake, na aligundua hivyo muda mfupi baada ya kurejea na kukuta nguo zake zilivyokuwa zimepangwa katika begi sivyo zilivyokuwa wakati akirejea.

Anasema, “Uzuri ni kwamba, nilipolalamika kuwa fedha zangu zimeibwa mhudumu aliwaita wahusika aliowapa chumba cha chap chap, kwa kuwa walikuwa katika eneo la baa mahali hapo wakinywa bia, na kuomba wakaguliwe na walinzi. Ukaguzi ulifanikisha kupata fedha zangu kwa kuwa walizichukua zikiwa kwenye wallet (pochi ya wanaume)”.

Kileo yeye anasema wahudumu walimtumia wezi akagundua mapema na kuhama. Ushauri wangu kwa wahudumu; badilikeni.

Kwa maoni wasiliana na mwandishi kupitia 0784 779 090 au Barua pepr; namsp2000@yahoo. com