MAISHA YETU: Kuwa na mawasiliano mazuri kazini kwako

MSOMAJI, katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Jumamosi. Leo tutaangalia jinsi gani unaweza kuwa na mawasiliano mazuri katika ofisi unayofanyia kazi. Ni ukweli usiopingika kuwa, wale wote wanaofanya kazi maofisini, hutumia muda mwingi zaidi wakiwa ofisini kuliko nyumbani.

Hivyo ni muhimu kufurahia kazi ile unayoifanya na kuwa karibu na wale wote unaofanya nao kazi kwa muda huo, kwa sababu, wakati mwingine kazi tuzifanyazo husababisha msongo, hivyo kama unapata msaada kutoka kwa wenzako, inakusaidia kuondoa hali hiyo.

Lakini kwa upande mwingine, unaweza ukajikuta kuwa bila sababu ya msingi unapata upinzani katika shughuli zako unazozifanya kutoka kwa wafanyakazi wenzako. Na kwamba, pasipo sababu ya msingi unakuta watu wanakutendea matendo yanayokuudhi, unachotakiwa kukifanya ni kuwasamehe.

Unaweza ukawa mwema kwao, lakini wakakudharau, endelea kuwa mwema kwao. Unaweza ukawa mpole, wakatumia nafasi hiyo kukuhadaa, endelea kuwa mpole kwao. Ukiwa katika shughuli zako, unaweza ukaamua kutafuta furaha lakini wengine wakakuonea wivu, usivunjike moyo, endelea kuwa na furaha hiyo unayoitafuta.

Au unaweza kujikuta kuwa, mambo mazuri unayoyafanya leo, kesho yanaweza yakawa yamesahauliwa, Endelea kufanya vilevile bila kupunguza. Pamoja na upinzani unaoweza kukutana nao katika ofisi yako, elewa kuwa na mawasiliano ni muhimu katika eneo lolote la kazi.

Kuzungumza na kusikiliza wasimamizi wako na wafanyakazi wenzako ni muhimu, si tu kwa ajili ya mafanikio yako, bali kwa ajili ya mafanikio ya kampuni yako pia. Jifunze njia sahihi za kuwasiliana na wafanyakazi wenzako kwa njia mbalimbali, pia weka mazingira bora ya kazi kwa kila mmoja.

Penda kujifunza kusikiliza kwa makini, kusikiliza mtu ni jambo la muhimu sana, ni zaidi ya kuzungumza. Kwa kuwa, kusikiliza kunakufanya kuwaelewa wafanyakazi wenzako, mawazo na thamani yao. Kuwa na tabia ya kumsikiliza mwenzako na uliza maswali ili uwe na uhakika wa kile anachokizungumza na matarajio yake.

Pili, watendee wenzako vile unavyotaka wakutendee wewe. Kila mmoja mheshimu jinsi alivyo. Usimwingilie anapofanya shughuli zake, usimbughudhi na wala usigombane naye kuhusiana na vifaa vya ofisini. Unapohitaji kufanya jambo mwombe na ukimaliza mshukuru, usisite kumpa sifa zake pale anapostahili.

Kuwa mwangalifu na ishara za mwili unazotaka kuzitumia. Kamwe hata kama hupendi kusikiliza jambo unaloambiwa na mfanyakazi mwenzako, epuka kushika shika mikono yako, kugonga gonga miguu yako au kuzungusha macho yako.

Kwa kufanya hivyo itaonesha dhahiri kwamba hauna utayari wa kumsikiliza mtu huyo, na kufanya mawasiliano yenu kuwa magumu kwa siku zinazofuata. Kuwa na mwonekano wa tofauti katika shughuli zako.

Pokea simu unazopigiwa, jibu barua pepe unazotumiwa na fanya kazi zako kwa wakati. Utaheshimika na jaribu kujenga mahusiano mazuri na baada ya muda nao watakuwa wema kwako. Tukutane wiki ijayo kwa mawasiliano simu na: 0713 331455 au barua pepe Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.