JICHO: Madiwani na wabunge Dar, mnaziona barabara za mitaa?

NIANZE kwa kumshukuru Mungu kwa neema ya mvua katika maeneo mbalimbali nchini baada ya kipindi cha mvua kuchukua muda mrefu na kuwa tishio. Wasiwasi ulitanda kuwa huenda mvua haitanyesha.

Joto likawa kali hususani jijini Dar es Salaam. Watu wakafanya dua na maombi ya mvua. Mungu akasikia sala. Kwa takribani miezi miwili, tumeshuhudia mvua kubwa jijini hapa. Wakazi wa Dar es Salaam ‘wakasherehekea’ mambo kadhaa ambayo ni nadra kuyapata.

Hali ya hewa ya baridi kidogo ni miongoni. Makoti na masweta yakaanza kuvaliwa. Waliokuwa wamekunja mablanketi, wakaanza kuyatumia usiku. Miavuli nayo ikapata soko na wafanyabiashara wakatumia fursa kutengeneza faida ndani ya kipindi hicho kifupi cha mvua. Wengine wakapandisha maradufu bei ya bidhaa hiyo baada ya kubaini mahitaji yameongezeka.

Uchomaji wa mahindi nao ukashika kasi jijini ! Mara nyingi nimekuwa nikijiuliza uhusiano uliopo kati ya mahindi ya kuchoma na mvua/baridi!. Maana ikifika majira haya, utashuhudia wachoma mahindi ya kuuza kila mahali hususani maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu. Wakazi wa maeneo yenye shida ya maji, nao wakawa miongoni mwa washerehekeaji wa ujio wa mvua.

Wakavuna maji na kuondokana na adha ya kununua au kuyafuata mbalii. Inawezekana kwa watu wanaoisikia Dar es Salaam wakawa na dhana kuwa wakazi wa jiji hili wana huduma zote za jamii na zinapatikana kirahisi. La hasha! Kwa taarifa yao (wasilolijua jijiji),hapa jijini yapo maeneo ambayo maji ya bomba ni anasa. Fikiria, katika maeneo ambayo ndoo ya lita 100 inauzwa kati ya sh 300 na 500, unadhani familia inaishije kama siyo kuyatumia kwa ubahili?.

Pamoja na faida za mvua zilizofanya watu kusherehehea kunyesha kwake, kama ilivyo kawaida, hakuna kitu au jambo lisilo na faida na hasara. Wakati upande mmoja ukisherehekea mvua, upande mwingine ukaanza kuichoka. Wapo waliokumbwa na mafuriko na wengine ambao nyumba zilianguka. Lakini pia hali mbaya ya miundombinu ya barabara ikawa sababu nyingine ya watu kuichoka mvua mpaka wakasahau jinsi ambavyo walipiga magoti kwa Mungu kuiomba!

Hali ya barabara, hususani za mitaa, si nzuri. Hazipitiki kutokana na ama utelezi au mashimo yaliyojaa maji. Yapo baadhi ya maeneo ambayo hata magari ilikuwa ni vigumu kuyapitisha. Wakati huo huo ni adha kubwa kwa waenda kwa miguu.

Kero hii ya kutopitika kwa barabara inatoa changamoto kubwa kwa mamlaka zinazohusika pamoja na viongozi, kuangalia tatizo hili kwa jicho la tatu. Inahitajika mipango madhubuti ya kuhakikisha barabara hizi zinapitika wakati wa kiangazi na masika.

Zipo barabara ambazo zinategemea moja kwa moja bajeti ya halmashauri kuzikarabati. Ushauri wangu ni kwamba, halmashauri kupitia kwa madiwani, wahakikishe inatengwa bajeti ya kutosha itakayowezesha kutengeneza barabara hizi kwa umadhubuti .

Lakini pia, zipo barabara za ndani ya mitaa ambazo viongozi wa serikali wa mitaa kupitia wajumbe, hawana budi kushirikiana na wananchi kwa kuwahimiza suala zima la kujitolea ikiwa ni pamoja na kumwaga vifusi.

Wakati mwingine, wananchi wakihamasishwa , wana uwezo wa kushiriki wenyewe kutatua kero zao bila kusubiri fedha au nguvu kutoka kwenye mamlaka. Lakini inapokuja wakawa na viongozi wanaoishia maofisini, wasioitisha vikao wala kutembelea maeneo yao kuona kero zao, wananchi nao hubweteka na kuamini kuwa kila kitu lazima kifanywe na serikali.

Wapo viongozi ambao wameshaanza kuchukua hatua. Hawa ni mfano mzuri wa kuigwa na kila. Wanaonesha ukaribu wao kwa wananchi. Kwa mfano, katika eneo ninaloishi, diwani (Kata ya Kibamba, Ernest Mgawe) ametoa matangazo kwa wananchi wa eneo lake akiwataka wawasilishe taarifa za barabara mbovu.

Akawataka wajumbe wa serikali za mitaa wafanye kazi hiyo ya kupokea taarifa zote za barabara zilizoharibike, ziwasilishwe kwenye ofisi yake ili mvua itakapokoma, zianze kufanyiwa ukarabati. Naamini suala hili la ubovu wa barabara linapaswa kuwa kipimo cha viongozi wanaofaa.

Madiwani na wabunge ndiyo mdomo wa wananchi. Ni mategemeo yangu kuwa wameshaona kero hii ya barabara za mitaa na watasimamia kidete utatuzi wake. Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.