MC GLOTE: MC epuka lugha za dharau na kuudhi

NI wakati wa kukumbushana kuwa, kila kazi kinahitaji staha, heshima na uvumilivu katika kuifanya ili ikupe riziki za kila siku.

Kuna wakati washereheshaji (MC) wanakumbwa na mambo yanayoudhi na badala ya kutafuta hekima ya namna ya kuyakabili, wanapatwa na hasira na kuanza kuwajibu wahusika wa shughuli vibaya na ubaya unavuka mipaka hadi kwa wageni waalikwa.

Unakuta MC anazungumza kwa dharau akionesha kamati ya maandalizi haijui kazi yake, anadharau mpaka maharusi na hata wazazi wao kutokana tu na kuudhiwa ama na mwana kamati mmoja au baadhi ya wanakamati.

Tunakumbushana kuwa, ikiwa kuna mtu katika shughuli fulani amekuudhi, ujitahidi kuzuia hasira isitoke nje hadi kuonekana kwa wageni waalikwa ambao kwa namna yoyote hawapaswi kujua kama kuna tofauti baina ya wenye shughuli na MC.

Wakati wote ukiona unataka kuudhika, ni bora ama ukaacha kuzungumza na mtu husika au ukanyamaza kimya ili shughuli ya watu iende vizuri na siku nyingine uweze kupata kazi nyingine nyingi.

Nimewahi kushuhudia katika harusi moja MC aliwafokea wanakamati hadharani na kuwaeleza kuwa wasidhani ana kazi moja tu ya U-MC bali ana kazi nyingi anazofanya na nyingine kwa uwezo aliyonao anaweza kuwafunga jela.

Maneno hayo aliyasema mbele ya wageni waalikwa na hii iliharibu kabisa sherehe nzima, MC aliendesha shughuli ile kwa kisirani tu, hakukuwa na furaha tena, hali ya hewa ilibadilika kabisa na kuna wakati mwenyekiti alitaka kumnyang’anya kipaza sauti na kidogo wapigane.

Ni kweli kuna mambo yanaudhi sana, lakini ipo njia ya busara kujiepusha na kero hizo ili kuhakikisha kazi inamalizika salama. Hakuna atakayejua kuwa mwenyekiti au kamati ndio yenye makosa, mwisho wa shughuli anazungumzwa zaidi MC alifanya kazi vizuri au aliharibu.

Ma-MC wenzangu, chonde chonde tusiwe sababu ya kuharibu shughuli za watu kwa dharau zetu, majivuno au hasira hata kama zimesababishwa na wenye shughuli waliotupa kazi, tujizuie na kuendesha shughuli vizuri na tukimaliza, tuombane msamaha ili maisha yaendelee.

MC usisusie kazi katikati ya sherehe na kuondoka kisa mwanakamati kakuudhi, vumilia maana unapaswa kujua mwenye kushikilia usukani wakati huo ni wewe MC na si mwingine, usilipeleke gari mtaroni tafadhali. Nawatakia kazi njema. Ukiwa na maoni au maswali, niandikie MC GloTe 0715022555