IMEPENYA: Kamati ya tuzo iweke mbele uzalendo

KAMATI inayohusika na utoaji wa tuzo za mwezi za mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ambayo ipo chini ya Shirikishola la Soka Tanzania (TFF), imekosa uzalendo.

Ndiyo sababu kubwa ya kusema hivyo ni katika tuzo za mchezaji bora kwa miezi mitatu walizotoa hakuna hata mchezaji mzawa aliyeshinda tuzo hiyo. Kamati hiyo imeona mabao ya Emmanuel Okwi, mchango wa Shafiq Batambuze wa Singida United na Obrey Chirwa wa Yanga na kuamua kuwapa tuzo hiyo pamoja na kuzawadiwa kitita cha Sh 1,000,000.

Hivi kweli kwamba katika kipindi chote cha miezi mitatu hakuna mchezaji mzawa ambaye alionesha kiwango cha juu na ambacho kiliwazidi wachezaji hao watatu ambao ndiyo washindi wa tuzo hizo.

Katika hilo sitaki kuamini na ninachoweza kusema hapo jopo la makocha na watu ambao ndiyo huchagua mchezaji bora wa mwezi husika wamekosa uzalendo na kwa kiasi fulani wanaua ari ya wachezaji wetu wazawa.

Hebu tuangalie sevu za Aishi Manula akiwa na kikosi chake cha Simba ameokoa hatari ngapi hata baadhi ya makocha wa timu pinzani kusema kwamba yeye ndiyo alikuwa kikwazo kwa timu yake isipate ushindi.

Vipi kwa Erasto Nyoni ambaye kwa msimu huu ndiyo beki na mchezaji pekee anayeongoza kwa kutoa pasi za mwisho za mabao yalipofungwa na Simba, lakini katika hili utamwachaje mfalme mpya wa Yanga, Ibrahim Ajibu, ambaye ndiyo kinara wa mabao kwa timu yake na katika pointi ilizonazo timu yake amechangia kwa asilimia 10 tena akiwa kwenye viwanja vya ugenini.

Siyo hao pekee wapo kina Mohamed Issa na Benedict Tinoco wa Mtibwa Sugar yupo pia Mudathir Yahya na wengine wengi ambao wanafanya vizuri na wanastahili tuzo hii lakini pengine Utanzania wao umesababisha kutokuonekana.

Sijajua vigezo ambavyo vinazingatiwa ili mchezaji kushinda tuzo hiyo zaidi ya vile vinavyoelezwa kuwa katika mwezi husika aliisaidia timu yake kushinda mechi kadhaa na yeye kufunga idadi ya mabao fulani.

Kwangu Mimi hivyo peke yake havitoshi kumpa mchezaji tuzo ya heshima kama hiyo ni lazima awe na vitu vingine vya ziada ndani na nje ya uwanja na siyo kufunga mabao pekee.

Nyota wa Tanzania, Mbwana Samatta kabla ya kujiunga na KRC Genk ya Ubelgiji alifanya vizuri akiwa na TP Mazembe ya DR Congo lakini hata siku moja hakuwahi kupewa tuzo ya mchezaji bora katika ligi ya ndani zaidi ya wachezaji wazawa.

Wenzetu walifanya hivyo kwa sababu waliwaza mbele uzalendo na lengo lao ilikuwa kuwatangaza kimataifa wachezaji wao leo hii Trousa Mputu ameondoka zamani Mazembe anacheza Ulaya kwa muda mrefu.

Ubishi wa Samatta ndiyo uliomfanya kutwaa tuzo ya mchezaji bora Afrika na hiyo ilitokana na michuano ya kimataifa siyo ligi ya ndani ambayo naamini angepewa kipa Robert Kidiaba.

Kamati hiyo inatakiwa kuiga mfano wa wenzetu kwa kutumia nafasi ya tuzo hizo kuwatangaza wachezaji wetu kwani kufanya hivyo kutawaongezea ari ya kucheza kwa kujituma ili mwezi ujao aweze kushinda tuzo hiyo.

Pia kutamrahisishia kazi kocha wa timu ya taifa katika uchaguzi wake wa wachezaji bora wa kuunda kikosi hicho ambacho sisi wenyewe ndiyo tumekuwa wa kwanza kukosoa pindi anapoita wachezaji tofauti au anapopata matokeo mabaya.

Nichukue fursa hii kuipa ushauri wangu kamati hii ambayo naamini inaongozwa na watu wenye weledi mkubwa na ufahamu wa juu katika mchezo wa soka kuitumia nafasi waliyonayo kwa kuwatangaza wachezaji wazalendo kwani kufanya hivyo siyo kuwabeba bali uwezo wanao na hilo halina ubishi