Hongera Zanzibar na karibuni Caf

BAADA ya muda mrefu kuomba uanachama wa kudumu katika Shirikisho la Soka la Afrika, Caf, hatimaye Zanzibar juzi lilitambuliwa rasmi kuwa mwanachama wa 55.

Kuanzia sasa Zanzibar inatambulika rasmi kuwa ni mwanachama halali wa Caf na itakuwa na haki sawa kama wanachama wengine ikiwemo nayo kuwa na kura yake yenyewe.

Mbali na kuwa na kura yake, Zanzibar pia kuanzia sasa itashiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) pamoja na yale ya Afrika kwa wachezaji wa nyumbani (Chan) kama inavyoshiriki Tanzania Bara.

Huko nyuma, Zanzibar ilikuwa ikiingizwa katika timu ya Tanzania Bara na kuifanya kuwa Tanzania, lakini sasa nao watasimama kama wanachama kamili.

Kuna faida nyingi Zanzibar kupata baada ya kupata uanachama kamili, kwani sasa nao watafaidika na misaada mbalimbali ya Caf, ikiwemo ya mafunzo na ile ya fedha.

Baada ya kupata uanachaka kamili wa Caf wakati umefika sasa kwa Zanzibar kujipanga ili kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa na kudhihirisha kuwa walistahili nafasi hiyo.

Hii ni fursa mpya sasa kwa Zanzibar kuonekana kama Zanzibar na sio kupitia Tanzania, hivyo kisiwa hicho kitaweza kutangaza vipaji vyake yenyewe tofauti na zamani.

Ni mataraji yetu kuwa Zanzibar itafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ya Afrika na baadae kuweza kuanza mchakato wa kuomba uanachama wa Shirika la Kimataifa la Soka (Fifa) na kuiwezesha kushiriki hata Kombe la Dunia.

Kupata uanachama wa Caf ni hatua moja itakayoiwezesha Zanzibar kupiga hatua nyingine na kuanza mchakato wa kuwa mwanachama halali wa Fifa siku za mbele.

Hakuna shaka kuwa kuwa mwanachama wa Fifa kutaiwezesha Zanzibar kupata misaada kama taifa huru linalojitegenea katika soka, tofauti na sasa, ambapo walikuwa wakitegemea ile misaa inayoletwa kwa TFF ndio nao wagawiwe.

Mchakato wa kusaka uanachama wa Fifa unatakiwa kuanza mapema ili kukiwezesha kisiwa hicho nacho kutambilika rasmi katika ulimwengu wa soka.

Ni matarajio yetu kuwa Serikali ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuweka nguvu yake ili kuwezesha kupatikana uanchana wa Fifa, kama ilivyofanya wakati ikiisaidia Zanzibar kupata uanachama wa Caf.

Tunapenda kuwapongeza wadau wote wa michezo waliofanya jitihada kuhakikisha Zanzibar inapata uanachama kamili wa Caf.

Moja ya sheria ya Fifa ya kuwa mwanachama ni kwa nchi kwanza kuwa mwanachama wa shirikisho la soka la bara lake kama ilivyo Zanzibar, hivyo ni matumaini yetu kuwa uanachama wa Fifa inanukia kwa kisiwa hicho cha marashi ya karafuu.

Tunapenda kuipongeza Wizara ya Habario, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa juhudi zao kuhakikisha Zanzibar inakuwa mwanachama wa Caf.

Wdau hao wa michezo walikuwa wakifanya kazi bila kuchoka pamoja na kukatishwa tamaa na baadhi ya nchi kuwa, kisiwa hicho kamwe hakiwezi kupata uanachama wa Caf.

Siku zote umoja ni nguvu na hilo ndilo limeiwezesha Zanzibar kupata uanachama wa Caf. Kila la heri Zanzibar kujiunga na Caf na huo ndio uwe mwanzo wa kupata uanachama kamili wa Fifa.