Vijana wachangamkie ufadhili Ofisi ya Waziri Mkuu

ALHAMISI iliyopita, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, ilitoa tangazo la Machi 15, 2017 katika Gazeti la Daily News, Uk. 15 mintarafu nafasi 820 za mafunzo ya stadi za kazi katika sekta za ushonaji nguo, ufundi wa bomba, useremala, uchomeleaji; na teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).

Wakati Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ikitoa fursa hiyo muhimu kwa vijana, tangu mwaka jana imekuwa katika utekelezaji wa Programu ya Kukuza Stadi za Kazi Nchini kwa kipindi cha miaka mitano (2016- 2021).

Hii ni Programu inayolenga kuwezesha nguvu kazi ya taifa kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki ili kumudu ushindani katika soko la ajira.

Katika hili, Serikali inastahi pongezi na kuungwa mkono kwa ubunifu wake. Kwa mujibu wa tangazo hilo, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, imeingia makubaliano na Taasisi ya Don Bosco Net Tanzania ya Osterbay jijini Dar es Salaam ya kutoa mafunzo katika fani zilizotajwa pamoja na ufundi wa kompyuta kupitia Tehama.

Katika tangazo hilo, Serikali inawatangazia vijana wa Kitanzania wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 wanaopenda kujiunga na mafunzo katika moja ya fani zilizotangazwa.

Jumla ya vijana 820 watafadhiliwa na Serikali kwa kulipiwa ada na nauli ili kuhudhuria mafunzo hayo yatakayofanyika katika vyuo vya Don Bosco, Dar es Salaam.

Kijana atakayenufaika na ufadhili huu atatakiwa kuchangia mafunzo hayo kwa kujilipia gharama za malazi na mahitaji mengine ya kujikimu wakati wa mafunzo yatakayoanza mwezi Aprili mwaka huu katika vyuo vya Taasisi ya Don Bosco Net Tanzania.

Sisi tunasema, tunaipongeza Serikali kwa kutambua kuwa, mafunzo hayo ni muhimu kwa vijana, lakini pia kutambua na kuzingatia kuwa wapo vijana wenye sifa na watakaohitaji, lakini wakashindwa kumudu gharama za usafiri na ada.

Kwa kuliona hilo, Serikali inabeba mzigo wa vijana wote 820 kuwalipia ada na nauli kama tulivyosema awali. Hili ni jambo jema, la kupongez ana hata kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano.

Tunasema kinachopaswa sasa kwa vijana wenye sifa na wanaohitaji, ni kuandaa maombi yao na kuyatuma yakiwa na viambatanisho vilivyotajwa kati ya Machi 18- 30, 2017.

Tunapenda kuwakumbusha waombaji kuwa viambatanisho vinavyohitajika kwa waombaji, ni barua ya maombi ikiwa na anwani kamili, namba za simu na barua pepe, nakala ya cheti cha elimu aliyohitimu mwombaji, nakala ya cheti cha kuzaliwa au kadi ya mpiga kura, barua ya utambulisho toka Serikali ya mtaa anaoishi mwombaji pamoja na na picha nne za pasipoti.

Sifa zinazohitajika kwa waombaji ni elimu ya sekondari au zaidi, wakati fani ya ufundi wa kompyuta ni elimu ya sekondari. Sisi tunasema, tunaipongeza Serikali kwa kudhamiria kweli kuifanya Tanzania kuwa uchumi wa viwanda na kuwajali vijana.