Hongera mameya kujitosa vita dawa za kulevya

WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ikiendelea na kampeni ya kupambana na dawa za kulevya nchini, Umoja wa Mameya wa Majiji na Manispaa Tanzania wa Kupambana na Kutokomeza Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi (AMICAALL), nao umetangaza kuunga mkono vita hiyo.

Wamesema dawa za kulevya ni mojawapo ya visababishi vikuu vya kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi, hasa kwa vijana, hivyo kuona umuhimu wa kushiriki katika vita ya kuwaokoa vijana hao ambao ni nguvu kazi ya taifa.

Uamuzi wa umoja huo ulitangazwa na Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo ambaye ni Mwenyekiti wa umoja huo, juzi mjini Morogoro ambako umoja huo unakutana kwa mkutano wake mkuu wa mwaka.

Hakika ni wazo la kuungwa mkono, kwani hakuna Mtanzania asiyejua madhara ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya nchini, yakiwemo ya kiafya, kijamii, kiuchumi, kimazingira, kisiasa na kiusalama.

Kiuchumi, matumizi ya dawa za kulevya huongeza mzigo kwa taifa kwa kuwa hupunguza nguvu kazi na husababisha uharibifu wa mali.

Pia, gharama za udhibiti zikiwemo utoaji wa elimu kwa umma, uteketezaji wa mashamba ya bangi, uendeshaji wa kesi, kuwatunza wafungwa magerezani na kuwatibu watumiaji huongeza mzigo kwa taifa na jamii kwa ujumla.

Pesa na nguvu kubwa inayotumika katika kampeni za udhibiti zingeweza kusaidia kufanya shughuli nyingine za maendeleo na ustawi wa nchi kwa ujumla.

Aidha, kwa upande mwingine, dawa za kulevya husababisha mfumuko wa bei unaotokana na fedha za biashara hiyo kuingizwa kwenye mfumo halali, hivyo kuwaongezea wananchi mzigo wa mfumuko unaojitokeza. Kijamii, dawa za kulevya zimeendelea kusababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Huchangia pia migogoro ya kifamilia katika jamii jambo linaloweza kuzisambaratisha kabisa. Wazazi ambao hutumia dawa za kulevya, huonesha mfano mbaya kwa watoto wao na jamii kwa ujumla.

Aidha, watumiaji wamekuwa wakijihusisha na tabia na vitendo viovu vikiwemo wizi, uporaji, biashara ya ngono na ubakaji.

Jamii imekuwa ikiamini kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni jambo la kujitakia, ndiyo maana serikali na jamii imekuwa ikipambana kuelimisha umma juu ya athari za matumizi ya dawa hizo.

Kuna athari pia hata kisiasa, kwani wafanyabiashara wa dawa za kulevya wakati mwingine huweza kushawishi wapiga kura kwa kutumia rushwa kuwachagua viongozi watakaosimamia maslahi yao pindi watakapokuwa madarakani.

Biashara ya dawa za kulevya huweza kuchochea machafuko ya kisiasa na mambo mengine hatari kwa amani na usalama wa nchini.

Kwa ujumla, athari za biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa kwa jamii kuliko faida zake, ndiyo maana, bila ya mashaka, tunathubutu kuwaunga mkono na kuwapongeza Umoja wa Mameya wa Majiji na Manispaa kuunga mkono vita iliyoanzishwa na Rais Magufuli dhidi ya dawa za kulevya.

Kwa kuwa vita hii ni ngumu, tunaamini kuna wengi watakaounga mkono juhudi hizi, ili mwisho wa siku Tanzania ibaki salama, lakini kama wakiachwa wachache wapambane, hakika hakutakuwa na mwisho mwema katika vita hii, kwani ni dhahiri wenye nia njema watashindwa.

Hatupendi tufike huko, lakini tukiamua, hakuna kitakachoshindikana.