Tukaze kamba zaidi kukuza viwanda nchini

SERIKALI ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Mgufuli imepania kuendedesha uchumi wa viwanda kwa lengo kuu la kuifikisha nchi katika uchumi wa kati.

Katika mikakati ya kuelekea katika utekelezaji wa azma hiyo, serikali imeweka mkazo maalum katika kukuza miundombinu ya usafiri wa barabara kwa kuunganisha mikoa na miji mbalimbali na pia kujenga reli ya kisasa itakayotumia umeme na tayari uzinduzi wa ujenzi wake umefanyika.

Sambamba na hayo Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imeongezewa uwezo kwa kununua ndege mpya na nyingine ziko mbioni kuwasili hapa nchini kurahisisha usafiri wa wananchi ikiwa ni pamoja na watalii kuja kufurahia fursa za utalii, mambo ya kale, utamaduni na mbunga mbalimbali za taifa.

Lakini habari zilizotolewa bungeni jana na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Kaijage juu ya kuanza kung’ara kwa sekta ya viwanda tunayoisubiri kwa hamu ni jambo la kutia moyo na nguvu ya aina yake.

Waziri Mwijage alisema kwa mwaka jana pekee sekta ya viwanda imetoa ajira 146,892 ikilinganishwa na ajira 139,895 zilizotolewa mwaka 2015, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.1.

Aliendelea kutoa ufafanuzi kwamba baadhi ya viwanda ambavyo vimeanzishwa katika kipindi cha mwaka 2016/17 kuwa ni pamoja na viwanda vya uzalishaji chuma, saruji, vigae, nguo, mavazi, ngozi na bidhaa za ngozi.

Vingine ni vile vya kusindika nyama, vyakula, mbogamboga na matunda, maziwa na mafuta ya kula ambavyo vyote vina fursa kubwa ya kutoa ajira kwa Watanzania.

Ni kweli kwamba bado hatujafikia lengo letu lakini hatuna budi kujidai pia kwamba tupo katika njia sahihi ya kuelekea tunakotaka kwenda na hivyo kila mmoja wetu kwa nafasi yake bila kufanya ajizi aweze kushiriki kikamlifu katika mikakati ya kuelekea katika uchumi wa viwanda.

Hapa tungependa kutoa pongezi za awali kwa serikali kwa kuonyesha mwanga wa mwelekeo wetu katika uhalisia wake na kwamba wote tushirikiane katika kufikia lengo hilo la uchumi wa kati kupitia viwanda.

Serikali, wanasiasa na wananchi kwa ujumla wao wawe tayari kutoa ushirikiano unaohitajika kwa kuendelea kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi yetu ili waje kwetu kuwekeza katika sekta hii ambayo inaonyesha kila dalili ya kuweza kuwapatia watu wetu suluhisho la tatizo la ajira.

Hakuna ubishi kwamba iwapo viwanda vitaendelea kuwekezwa nchini licha ya kutoa ajira, vitaongeza thamani ya mazao yetu mbalimbali yatokanayo na madini, kilimo na malighafi nyingine na hivyo kupata soko na bei bora zaidi kuliko hivi sasa.

Jambo la muhimu katika mikakati hiyo ya viwanda tuwe tayari kutoa kila ushirikiano kwa wenzetu wawekezaji watakaopenda kuja kushirikiana nasi katika hili bila kuwakatisha tamaa bila sababu.

Hapa tunasisitiza kwamba wao wapate kama wawekezaji na sisi pia tunufaike kama washiriki katika suala zima la kuwapatia rasilimali tulizokuwa nazo ili kuwekeza viwanda. Inawezekana tujipange sawia kwa hili.