Changamoto Ligi Kuu Bara zifanyiwe kazi

MSIMU wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kwa mwaka 2016/17 unamalizika leo, huku timu zote 16 zikishuka dimbani katika viwanja nane tofauti. Ligi hiyo iliyoanza Agosti mwaka jana, inamalizika baada ya mikimiki ya takribani miezi 10 ya kuchuana kwa timu hizo.

Mechi za leo zitawakutanisha mabingwa watetezi Yanga wakicheza na Mbao FC mjini Mwanza, huku Simba wakiwa wenyeji wa Mwadui ya Shinyanga katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mechi zingine ni kati ya Azam FC dhidi ya Kagera Sugar huku Majimaji ikiikaribisha Mbeya City, Stand United watatoana jasho na Ruvu Shooting, Prisons wataoneshana kazi na African Lyon na Ndanda watakuwa wenyeji wa timu iliyoshuka daraja ya JKT Ruvu.

Katika kipindi chote cha kufanyika kwa ligi ya msimu huu, tumeshuhudia changamoto kibao ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kuboresha zaidi ligi ya msimu ujao.

Kuna mambi mengi ya kuangaliwa kwani ligi inayomalizika ilikuwa na baadhi ya mapungufu ukiwemo uamuzi mbovu, upanguaji ratiba ovyo na mambo mengine, ambayo kama yakirekebishwa tutapata bingwa wa ukweli.

Siku zote ligi bora hutoa timu bora ya taifa, ambayo hufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, tofauti na Taifa Stars, ambayo imekuwa msindikizaji katika kila mashindano. Pamoja na changamoto zilizojitokeza, lakini TFF imejitahidi kuwafungia baadhi ya waamuzi walioshindwa kuchezesha kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za soka.

Ni matumaini yetu kuwa TFF pamoja na timu, ambazo zitaendelea kuwemo katika ligi hiyo, zitajitahidi kurekebisha makosa yaliyojitokeza msimu unaomalizika ili msimu ujao uwe na msisimko zaidi. Ligi yetu ikiwa bora na imara bila shaka tutapata bingwa mwenye uwezo wa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa atakayotuwakilisha.

Kwa sasa klabu zetu zimekuwa zikitolewa mapema katika mashindano ya kimataifa kutokana na kushindwa kupambana na wenzao wenye uwezo mkubwa wanaokutana nao kimataifa. Sio kwa timu ya taifa au klabu, Tanzania haina rekodi nzuri katika soka la kimataifa na hii inatokana na kutokuwa na ligi bora yenye kutoa timu imara.

TFF ambayo ndio yenye timu za taifa, yenyewe haina wachezaji na badala yake imekuwa ikiwategemea wachezaji hao wa klabu, ambao inawapata kupitia mashindano mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa hiyo ni matarajio ya wadau wengi wa soka nchini kuwa, msimu ujao wa Ligi Kuu utakuwa mzuri kwa timu kujiandaa vizuri na TFF kuwa makini zaidi ili kutoa bingwa mwenye uwezo kupambana kimataifa.