Waliombeza Rais Magufuli wakubali kumwita shujaa

JUMATATU iliyopita Kamati ya Pili aliyoiunda Rais John Magufuli, kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusu mchanga wa madini unaosafirishwa nje ya nchi, iliwasilisha ripoti kwa Rais ikibainisha “madudu mengi makubwa.”

Kama ilivyo kwamba kwenye msafara wa mamba kenge hawakosekani, wapo baadhi ya Watanzania waliojivisha ukenge na kuendelea kuibeza Kamati na kuwajaribu kuwakatisha tamaa Watanzania na kuwasaliti katika suala hili wakipambana kuwalinda wezi wa rasilimali za taifa.

Hata hivyo, sauti ya Mungu. Shimo walilomchimbia Mkuu wa Nchi kumwombea akwame katika vita hii ili walipwe posho, wametumbukia wenyewe. Kitendo cha baadhi ya wapinzani kujitokeza kumpongeza Rais, kinaonesha wameanza kuelewa na kutoka katika giza lililowazingira na sasa wanauona ukweli, umakini, ujasiri na ubora wa uongozi wa Rais Magufuli.

Wengine waige mfano. Sisi tunasema umakini, ujasiri na msimamo wa Rais Magufuli, ndio umewafanya Wazungu hao wanaopigiwa magoti na wasaliti wa Tanzania, kuja kumpigia magoti Rais Magufuli wakiomba yaishe ili mazungumzo na taratibu nyingine zianze kama alivyoagiza Rais.

Ikumbukwe kuwa Acacia ilibainika kutokuwa na kibali na wala haijasajiliwa, lakini shughuli zake nchini zimelisababisha taifa kupoteza shilingi trilioni 108. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Nehemiah Osoro alisema kiasi hicho ni sawa na bajeti ya sasa ya Serikali kwa miaka mitatu pamoja na kujenga Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa kiwango cha ‘standard gauge.’

Tunampongeza Rais kwa kufungua milango ya mazungumzo, hali inayotoa fursa ya mali za Tanzania kurudi, lakini pia kudumisha uhusiano na wawekezaji ambao ni muhimu kwa uchumi wa nchi hasa wanapofanya kazi kiadilifu.

Tunampongeza Rais kwa uwazi, ukweli, umakini na msimamo usioyumba uliomwinua Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation, mmiliki mkubwa wa Acacia Mining Limited, Profesa John Thornthon kutubu kwa Watanzania na kusema wapo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ili kulipa fedha ambazo Tanzania imepoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake nchini.

Thornthon aliyefika juzi kutoka Canada, alitubu mbele ya Rais Magufuli, hali iliyoibua utayari wa kufanyika mazungumzo kwa kuzingatia maslahi ya pande zote. Hili ni jambo jema la kupongeza.

Sisi tunawashauri wote waliombeza Rais, wajitathmini uzalendo wao kisha wamuunge mkono kwa dhati Rais na Watanzania wengine ili kuongeza nguvu katika vita hii ngumu ya kiuchumi.

Hao, wajikosoe, wajisahihishe na kuanza upya huku wakimtambua Rais Magufuli kama shujaa wa Afrika, ambaye ni somo kubwa kwa Waafrika wengi. Ndiyo maana tunasema, tuache yaliyopita, tuvae uzalendo sasa tuunganishe nguvu tuilinde Tanzania, tulinde rasilimali, maliasili na maslahi ya Tanzania, tuijenge Tanzania yetu bila usaliti, bali kwa uzalendo wa pamoja maana silaha yetu imara ni umoja, ukweli na haki.

Wawekezaji walio nchini, wafanye kazi kizalendo, kama ambavyo Mwenyekiti huyo alivyokubali pia kuwa watashiriki kujenga mtambo wa kuchenjua dhahabu hapa nchini. Ndiyo maana tunasema, “Waliombeza Rais Magufuli, Wamwite Shujaa.”