Marekebisho Sheria yatamkomboa Mtoto

JUZI Juni 16, ilikuwa Siku ya Mtoto wa Afrika. Kitaifa iliadhimishwa mkoani Dodoma ikiwa na kaulimbiu isemayo, “Maendeleo endelevu 2030: Imarisha ulinzi na fursa kwa watoto wote.”

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamishina wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Salma Ali Hassan, siku hii inaikumbusha dunia kuhusu mauaji ya watoto wapatao 2,000 wa kitongoji cha Soweto, Afrika Kusini, waliouawa kikatili miaka 41 iliyopita na iliyokuwa Serikali ya Makaburu wakati wakidai haki zao ikiwamo ya kutobaguliwa.

Ili kumlinda mtoto, Tanzania imeridhia na kubuni sera, mipango na mikakati mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, ikiwemo: Sera ya Mtoto (2008), na Mpango-kazi wa Kitaifa wa Kuzuia na Kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (2017- 2022).

Kimataifa imeridhia na inatekeleza Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG’s) yaliyopitishwa mwaka 2015 yanayobainisha haki ya mtoto kuishi, kulindwa, kutobaguliwa na kushirikishwa kwa usawa ili kuhakikisha kuwa wanapata fursa sawa katika jamii. Hata hivyo, bado zipo changamoto mbalimbali zinazoathiri malezi ya watoto na kuwanyima fursa katika jamii.

Hizi ni pamoja na umasikini, migogoro ya wanandoa, mila potofu, utandawazi, majukumu ya kijinsia katika jamii na ukosefu wa haki ya elimu ya afya ya uzazi. Wakati jamii ikiadhimisha siku hii, bado Watanzania wanashuhudia vitendo vya ukatili na udhalilishaji wanavyofanyiwa watoto.

Kwa mfano, Juni 13, Peter Semango wa Kijiji cha Kimagai wilayani Mpwapwa, Dodoma alimlawiti mtoto wa dada yake mwenye umri wa miaka minane. Jamii inashuhudia watoto wakiingizwa katika ajira mbaya, wakitelekezwa, kuteswa na kufanyiwa ukatili ukiwamo wa kuchomwa moto na wazazi au walezi.

Katika mazungumzo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mkoani Dar es salaam, Makamu wa Rais, Samia Suluhu aliwataka wanajamii kuungana kupiga vita dawa za kuleva, utumikishaji watoto, ubakaji na aina zote za udhalilishaji, ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto.

Makamu wa Rais alisema, vitendo hivyo ni miongoni mwa mambo yanayosababisha magonjwa ya akili na mengine yasiyoambukiza yanayowaathiri watu wazima, vijana na hata watoto.

Ndiyo maana tunasema, ili kuhakikisha tunalinda usalama na haki za watoto wote, Watanzania wanapaswa kuzifanyia marekebisho sheria zote baguzi, kandamizi na zinazopingana na sheria nyingine.

Hizo ni pamoja na Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inayowaruhusu wavulana wenye miaka 18 kuoa, lakini imeweka umri wa miaka 15 kwa wasichana kuolewa kwa ridhaa ya wazazi.

Tunashauri pia jamii iweke mfumo utakaowezesha watoto wa kike wanaopata mimba wakiwa shuleni kuendelea na masomo yao, baada ya kujifungua. Wadau wa haki za watoto wahakikishe ulinzi, usalama na haki za mtoto vinaimarishwa.

Tunasema, watoto wote wapate malezi bora yanayotoa fursa sawa kwa wote ili kuhakikisha kuwa ndoto zao katika maisha zinafikiwa. Wadau wahakikishe aina zote za ukatili na ubaguzi dhidi ya watoto zinaondolewa na kuwapa haki na fursa sawa katika umiliki wa rasilimali na nyanja zote za kimaisha.