Viongozi wengine muigeni Majaliwa

TANGU alipoapishwa kushika wadhifa huo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametembelea maeneo mengi nchini na kuzungumza na wananchi.

Tunapongeza ziara hizo za Waziri Mkuu kwa sababu ameweza kutatua kero nyingi papo hapo, anazoelezwa na wananchi, hasa zile zinazohitaji ufumbuzi wa haraka. Lakini, kero zinazohitaji ufumbuzi wa muda mrefu, Waziri Mkuu amekuwa akiwaahidi wananchi kufuatilia, kisha baada ya muda mfupi serikali huzitatua.

Ni wazi ziara zake hizo zimeleta neema katika maeneo mengi na matumaini kwa wananchi. Kwa mfano juzi, Majaliwa alitembelea mradi wa ujenzi wa daraja la mto Lukuledi, lenye urefu wa kilometa 30.45, linalounganisha mikoa ya Lindi na Mtwara na kusema kwamba ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake.

Alitembelea daraja hilo katika Kijiji cha Nandanga, alipowasili wilayani Ruangwa akiwa katika ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Lindi. Ujenzi wa daraja hilo utakaogharimu Sh bilioni 5.4 ni mkombozi kwa wananchi wa mikoa hiyo, hasa wa wilaya za Ruangwa na Masasi, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana katika masuala mbalimbali yakiwemo kilimo na huduma za kijamii. Watu wengi wamepoteza maisha kwa kuliwa na mamba, walipokuwa wakikatiza katika eneo hilo.

Ujenzi wa daraja hilo utawezesha watu wengi wa Ruangwa, kuvuka kufuata matibabu katika Hospitali maarufu ya Ndanda wilayani Masasi na wakazi wa Ndanda watavuka na kufanya shughuli za kilimo wilayani Ruangwa.

Hali kadhalika, jana Majaliwa alifanya ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa na kukabidhi magari mawili ya kubeba wagonjwa. Moja ya magari hayo ni kwa ajili ya hospitali hiyo ya wilaya na lingine litapelekwa katika Kituo cha Afya cha Mandawa.

Kwa hakika magari hayo mawili yatarahisisha usafiri kwa wagonjwa wa maeneo hayo, wanaohitaji matibabu ya dharura katika hospitali kubwa. Pia, magari hayo ya kisasa ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali ya Rais John Magufuli wa kuboresha huduma za afya kuwaondolea wananchi kero mbalimbali, hasa akina mama na watoto.

Hivyo, kutokana na manufaa mengi na makubwa ya ziara anazofanya Waziri Mkuu, tunahimiza viongozi wengine wa serikali wa ngazi za mikoa na wilaya, kutembelea maeneo yao mara kwa mara na kutatua kero za wananchi. Tunawasihi waache kusubiri ziara za viongozi wa kitaifa, ndipo watembelee maeneo yao kwa sababu wananchi wana kero nyingi na zinaongezeka kila siku.