Taratibu zifuatwe kujaza nafasi za vyeti feki

JUHUDI za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, kukabiliana na uovu mbalimbali ndani ya utumishi wa umma, unaendelea kuleta matokeo chanya likiwemo la kupatikana kwa ajira 10,184, ambazo awali zilikuwa zinashikiliwa na watu waliojipatia ajira hizo kwa kutumia vyeti feki.

Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, juzi ilitangaza kutoa vibali kwa ajira hizo kujazwa. Tunapenda kuipongeza serikali kwa kuligundua na kulisimamia hilo na kutoa nafasi kwa Watanzania wanaostahili kushika nafasi hizo kwa sifa stahiki walizonazo.

Hakuna ubishi kwamba nchi yetu kwa hivi sasa, wamo wataalamu wengi waliosomea ujuzi katika sekta mbalimbali hadi kufikia ngazi ya vyuo vikuu, vyuo vya kati na vingine vinavyotoa ufundi katika nyanja mbalimbali.

Hapa tunapenda kutoa wito kwa watakaohusika na suala zima la kuajiri watumishi, watakaoziba nafasi hizo kwa kuweka umakini, unastahiki katika zoezi zima kuwapata na kuwaajiri wafanyakazi watakaoziba nafasi hizo.

Hakuna sababu ya kurudia makosa ya kuajiri watu wasiokuwa na taaluma ya fani, inayohusika katika ajira kwa kuhakikisha kwamba vigezo na sifa za kwa kazi husika zinafuatwa kwa ukamilifu unastahiki.

Tunafahamu kwamba kazi ndani ya serikali, taasisi, kampuni na mashirika yake, zina utaratibu unastahiki kufuatwa ili kupata watumishi wake wanaostahiki na hivyo kukumbusha kwamba ni busara wahusika katika zoezi hili wakafuata taratibu hizo bila kufanya ajizi.

Moja ya sababu ya kukosekana kwa ufanisi katika utendaji wa kazi ni pamoja na kuwepo waajiriwa wasiokuwa na sifa na kazi husika na wale ambao walikuwa na vyeti feki. Kwa hili tusilipe tena nafasi katika ajira hizo.

Tunapenda pia kuwapongeza watumishi 450, walioshinda katika rufaa zao katika zoezi la vyeti feki kwani bila shaka wanastahili sifa na haki imetendeka katika kupata ushindi huo, kwani wenzao 600 wameshidwa na hivyo kutorejea tena kazini.

Washindi hao wachukulie zoezi hilo, kama changamoto katika maisha yao ya kazi na tunawatakia heri na warejee kazini kwa ari mpya ya kuchapa kazi bila kufanya ajizi. Kwa watumishi ambao hawakukumbwa na sakata hilo la vyeti feki na kuendelea na kazi, tunatoa wito kwamba wawapokee wenzao hao wanaorejea kwa kuwapa ushirikiano unaostahili.