Uwekezaji: SportPesa wameonesha njia

WACHEZAJI na viongozi wa timu ya soka ya Everton ya Uingereza wameondoka juzi usiku baada ya mchezo wao na Gor Mahia ya Kenya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wameondoka huku wakiacha kumbukumbu kubwa katika vichwa vya Watanzania na hasa mashabiki wa soka ya kumwona mbashara mshambuliaji wao nyota, Wayne Rooney. Rooney aliiongoza Everton kushinda Gor Mahia kwa mabao 2-1 katika mechi ya kirafi ki ya kimataifa akiwa amefunga bao la kwanza kwa shuti kali umbali wa mita 30.

Wameondoka wakiacha watu wakiendeleza mjadala kuhusu ujio wao uliodhaminiwa na Kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa, wadhamini wa Everton na pia Gor Mahia, Ligi Kuu Kenya na timu za Yanga na Simba katika Ligi Kuu Bara.

Tunaungana na wanamichezo wote nchini na duniani kote kueleza kufurahishwa kwetu na ujio huo wa moja ya timu kubwa Uingereza na duniani kwa jumla. Pia tungependa kuwasilisha shukrani zetu kwa Serikali ya Tanzania iliyokubali na kuratibu ujio wa mabalozi hao wa soka na kuhakikisha usalama wao kwa muda wote.

Lakini pia shukrani zetu ziende kwa uongozi wa SportPesa ya Uingereza na Tanzania hususan Mkurugenzi wa Utawala na Uendeshaji, Tarimba Abbas kuandaa ziara hiyo wakilenga kukuza soka na utalii.

Tunawashukuru pia wafanyakazi na uongozi wa Shirika la Misaada la Kimataifa la Uingereza (DFID) kwa misaada linayotoa kwa watoto wa Tanzania waliobahatika kutembelewa na wachezaji wa Everton walipowasili.

Hayo na mengine mengi yaliyofanywa na Everton kama klabu, wachezaji binafsi na SportPesa kama kampuni ni kielelezo tosha cha nia njema ya kuleta maendeleo ya sekta mbalimbali, elimu, utalii, soka n.k.

Tunaomba taasisi na makampuni mengine yaige kilichofanywa na Sport- Pesa kuleta maendeleo katika maeneo ya kisekta. Tunaipongeza SportPesa kwa kuguswa na eneo la utalii na soka na kutumia fursa hii kuionesha dunia, mambo mazuri yaliyo nchini mwetu katika kuvuta watalii zaidi.

Ni matumaini yetu kuwa, baada ya ujio huu, watalii zaidi watakuja nchini kutoka Uingereza na maeneo mengine ambako wamekuwa wakifuatilia ziara ya Everton. Kwa wanaohusika na masuala ya utalii, tunaomba watumie fursa hii kuboresha zaidi huduma zao ili wageni wanapokuja, waoanishe yale waliyoambiwa na wenzao.

Kwa watu wa mpira, tunaamini watakuwa wamejifunza mengi kutoka kwa viongozi na wachezaji wa Everton na hivyo kuwa kwenye nafasi ya kuendesha soka kisasa. Wachezaji watakuwa wamejifunza pamoja wenzao wanavyowajibika kwa shughuli za jamii bila kuchoka licha ya safari ndefu wakitekeleza nadharia ya Hapa Kazi tu.

Kwa makampuni mengine, hii ni fursa ambayo imewafumbua macho jinsi gani Serikali ilivyo tayari kushirikiana nao. Haitoshi tu kwa makampuni kutangaza wametumia mamilioni ya fedha kama huduma kwa jamii wakati kiasi hicho hakiakisi mapato yao na thamani ya rasilimali walizokabidhiwa kuvuna.

Hili lililofanywa na SportPesa limegusa nyoyo za mamilioni ya Watanzania na hata nje ya Tanzania, Afrika na duniani. Huu ndiyo aina ya uwekezaji tunaotaka, unaogusa maisha ya watu wengi na kuakisi faida zake kwa kila mtu iwe kwa furaha au mapato. Hongera Tarimba.