Wachochea vurugu wasipewe nafasi

KATIKA habari muhimu zilizochapishwa na gazeti hili jana ni pamoja na ile iliyobeba kichwa cha habari ‘Wanaotoa matamshi ya kichochezi kukiona.’

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa ibada ya mazishi ya mke wa Waziri wa Habari, Utamadani, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe yaliyofanyika wilayani Kyela mkoani Mbeya juzi.

Waziri Mkuu alisema serikali haitavumilia kuona baadhi ya watu, wakitoa matamshi ambayo hayana tija kwa jamii na badala yake kulenga kuwavuruga wananchi na kuchochea migogoro.

Sisi tunamuunga mkono Waziri Mkuu kwa angalizo hilo muhimu la kuimarisha amani, utulivu na mshikamano wa Watanzania, uliokuwa umejengeka tangu tupate uhuru wetu kutoka mikononi mwa ukoloni wa Uingereza.

Katika tamko lake, Waziri Mkuu alisema kuwa serikali itawashughulikia watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi popote walipo, bila kujali uwezo wao, vyeo vyao na mamlaka waliyonayo.

Hapa tungependa kuwakumbusha Watanzania kwa ujumla wake kwamba yeyote anayelenga kuwatenganisha Watanazania kwa kutumia mbinu yoyote ile, ikiwa ni pamoja na uchochezi ili kuharibu utamaduni wetu, tulioujenga kwa muda mrefu wa kuishi kwa amani na utulivu asipewe nafasi asilani katika taifa letu.

Tanzania ni moja ya nchi chache barani Afrika, ambazo zimekuwa zikipiga vita kwa vitendo ubaguzi wa aina yoyote ile ndani ya jamii, ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa rangi, ukabila, dini na itikadi na badala yake kuhimiza ushirikiano na mshikamano katika nyanja za kujiletea maendeleo endelevu.

Uchochezi ukipenyeza katika jamii yoyote ile makini au nchi, suala la utulivu na amani hutoweka na badala yake hubakia vilio na kusaga meno. Hapa tungependa kuwakumbusha yaliyotokea nchi jirani ya Rwanda mwaka 1994, ambayo kutokana na uchochezi ulioanzishwa na baadhi ya viongozi, vikundi, vyama vya siasa na makabila, uliitumbukiza nchi hiyo katika mauaji ya kimbari, yaliyoacha watu zaidi ya 800,00 kupoteza maisha na wengine kwa maelfu kulazimika kukimbia nchi yao.

Kutokana na hali hiyo, dunia iliunda Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) ili kuwashughulikia walioitumbukiza nchi yao katika dhahama hiyo, ambapo watu zaidi ya 80 walitiwa hatiani na kuadhibiwa kutumikia vifungo vya muda mbalimbali hadi vya maisha jela. Mahakama hiyo ingawa imeshakamilisha majukumu yake na kufungwa 2015, ilikuwa na makao yake makuu mjini Arusha nchini Tanzania.