Jamii isaidie Polisi kutokomeza uhalifu

KUMEKUWEPO na matukio ya mauaji ya wananchi na polisi katika wilaya za Kibiti, Rufi ji na Mkuranga mkoani Pwani, hali ambayo haiwezi kuachwa iendelee, kwani nchi hii ni ya amani kwa Watanzania wote.

Ni kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni akiwa katika ziara mkoani humo hivi karibuni aliwataka wananchi wa wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji kutoa taarifa za matukio ya uhalifu kwa Jeshi la Polisi bila woga wowote, ili jeshi hilo liwasambaratishe wahalifu katika maeneo hayo.

Masauni anasema ili jeshi hilo lifanikiwe katika mapambano yake na wahalifu, nguvu ya wananchi inahitajika katika utoaji wa taarifa ya matukio hayo. Ni vema wananchi wa wilaya hizi, kulifanyia kazi ombi hilo la Naibu Waziri kwa kuwa waathirika ni wananchi wenyewe.

Wananchi wanaouawa ni ndugu, jamaa na marafiki wa maeneo hayo. Maofisa wa polisi waliouawa ndio walinzi wa usalama wa maisha na mali zao. Hivyo, hakuna namna nyingine zaidi ya wananchi ambao ndio wanaokaa na wahalifu, kujitoa kwa moyo kutoa taarifa ambazo zitaliwezesha jeshi la polisi kufanya kazi yake na mwisho kuwatia nguvuni wahalifu hao ili kurudisha amani na usalama wa maeneo husika.

Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Bungu wilayani Kibiti, Masauni anasema jeshi hilo limejipanga kikamilifu kwa kupambana na wahalifu na litahakikisha wahalifu hao wanakamatwa wote ili wakazi wa maeneo hayo, waendelee kufanya shughuli zao za kuijenga nchi kama kawaida bila wasiwasi wowote.

Watu wengi wamekuwa hawajiamini, kwa kuwa taarifa wanazotoa zaweza kugeuka kuwa kaa la moto, endapo polisi wanaopewa taarifa hizo wanazirudisha kwa wahalifu. Masauni alilisemea hili na kuwahakikishia usalama wananchi watakaotoa ushirikiano kwa jeshi hilo.

Anasema ili amani hii iweze kudumu, wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, pale ambapo wanakuwa na taarifa na wasiwasi na mtu yeyote katika maeneo yao, ambaye hana nia nzuri na usalama wao.

Kwa mujibu wa Masauni, Jeshi la Polisi halipaswi kuogopwa na raia mwema, kwani ni rafiki kwa kila Mtanzania mwema ambaye ana uzalendo wa dhati na nchi yake. Anasema kwamba jeshi ni rafiki wa wananchi, hivyo wananchi wanapaswa kuwa karibu na Jeshi, kwa kuwa hao ndio walinzi wa wananchi pamoja na mali zao.